SERIKALI BADO YAMNG'ANG'ANIA NA KUMKOSESHA RAHA PROF MUHONGO.
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema baadhi ya viongozi wanaodaiwa kusafishwa na Ikulu, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, bado wanachunguzwa na vyombo vingine, ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).
Akijibu hoja za wabunge jana kabla ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kupitishwa na Bunge, Pinda alisema baada ya wabunge kudai kuwa kuna viongozi wamesafishwa na kutaka wengine nao wasafishwe, Pinda alisema vyombo vinavyoendelea na uchunguzi vikipata ushahidi dhidi yao, wanaweza kufikishwa mahakamani.
Viongozi wengine wanaodaiwa kusafishwa na Ikulu mbali na Profesa Muhongo, ni pamoja na mawaziri wanne waliojiuzulu baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu operesheni ya kupambana na ujangili maarufu Operesheni Tokomeza.
Viongozi hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Akifafanua kilichotokea kikaibua suala la kusafishwa kwa viongozi hao, Pinda alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alikuwa akitoa taarifa mbili ambazo zilikuwa ni matokeo ya uchunguzi.
Taarifa ya Kwanza ilikuwa ya Tume iliyochunguza suala la Operesheni Tokomeza na nyingine ilikuwa ya Kamati ya Makatibu Wakuu, aliyounda yeye kuhusu sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi. Katika taarifa hizo, Pinda alisema Balozi Sefue alisema kuwa ingawa mawaziri hao hawakuwa na kosa la moja kwa moja, lakini haikuzuia kuwajibika kisiasa.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari kuhusu ripoti hizo, Pinda alisema Balozi Sefue aliulizwa swali kuhusu Profesa Muhongo, ndio akajibu kuwa Tume ya Taifa ya Maadili ya Viongozi wa Umma, haikumkuta na hatia.
“Nimezungumza na Tume ya Taifa ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wakaniambia ndivyo walivyomuona Profesa Muhongo lakini uchunguzi wao hauzuii vyombo vingine kuendelea kumchunguza na vikipata ushahidi dhidi yake, haizuii kufikishwa mahakamani.
Alisema hao wengine katika sakata hilo la Escrow, walioitwa katika Baraza la Maadili, akiwemo Mbunge wa Bariadi Mashariki, Endrew Chenge (CCM), Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) na aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, wamekutwa na kesi ya kujibu.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment