BENKI YA NBC YAWANEEMESHA WAISLAMU
Ofisa Fedha Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Jaffari Matundu (kushoto) akiwaongoza baadhi ya wateja wa benki hiyo mjini Zanzibar kuchukua mlo wa futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake wa Zanzibar mwishoni mwa wiki. (Na Mpigapicha Wetu).
BENKI ya NBC imesema imeongeza huduma zinazofuata masharti na kanuni za kiislamu katika akaunti husika visiwani Zanzibar, kukidhi mahitaji ya kibenki kwa makundi mbalimbali, wakiwamo wafanyakazi wa serikali na wafanyabiashara.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kibenki zinafuata Kanuni na Misingi ya Kiislamu wa Benki ya NBC Tanzania, Nassir Masoud alisema hayo juzi kwenye futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake visiwani Zanzibar.
Alisema, kupitia huduma hiyo ya kibenki, wameanzisha huduma na bidhaa mpya kwa ajili ya wateja wa kada tofauti, mfano mmojawapo, ikiwa ni akaunti ya ‘Islamic Affluent Current Account’ kwa ajili ya wateja wenye ukwasi.
Nassir alisema benki hiyo itaendelea kutoa huduma kwa kiwango cha juu katika kuweka na kutoa fedha zikiwemo akaunti tofauti ndani ya Islamic Banking ya NBC kwa nia ya kumtoa Mzanzibari kwenye dimbwi la umaskini.
“Ni takribani miaka mitano tangu kuanzishwa kwa huduma hii ambapo Waislamu nchini wamepata fursa ya kupata huduma za kibenki zinazoendana na masharti na kanuni ya dini ya kiislamu na tunaendelea kupata mafanikio makubwa kwa idadi ya wateja na miamala inayoendelea kufanyika kila siku,” alisema.
Alisema kwamba benki hiyo imepiga hatua kubwa kwenye kupata wateja wengi zaidi ndani ya visiwa vya Zanzibar baada ya kuweza kupata wateja wapya kutoka Wizara ya Elimu na Afya mjini Zanzibar.
Kwa upande wake, Ofisa Fedha Mkuu wa NBC Tanzania, Jaffari Matundu alisema kwamba benki hiyo itaendelea kutoa huduma kwa Wazanzibari kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia masharti ya dini ya kiislamu ili kuwawezesha kufikia malengo yao ya kibiashara na ya kijamii.
Alisema NBC itaendelea kutoa huduma na bidhaa zote kwa minajili ya kuwafikia Waislamu wote na wasio waumini wa dini hiyo mjini Zanzibar huku wakiendelea kusukuma gurudumu la maendeleo.
Huduma ya Islamic Banking ya Benki ya Taifa ya Biashara, ilianzishwa mwaka 2010 na kwa mujibu wa benki hiyo mikopo ya takribani Sh bilioni imekwishatolewa tangu ilipoanza kutolewa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment