Walinzi wa timu ya Watukavu FC, Yahaya Kapela na Anald Mitti wakichauan na mshambuliaji wa Salange FC, Mbaraka Shabaan kulia kuwania mpira wakati wa ligi ya kuwania pea 15 za viatu vya kuchezea mpira katika hatua ya 16 bora, michezo inayoendelea kufanyika uwanja wa Saba Saba Manispaa ya Morogoro.Watukavu ilishinda bao 2-0. Juma Mtanda.
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Klabu ya Burkina FC ya Morogoro inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara katika msimu wa mwaka 2015/2016 imeshindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya The Gunners Bonanza Cup 2015 baada ya kutandikwa bao 2-0 na Tumbaku FC katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo kwenye uwanja wa Sabasaba mkoani hapa.
Kiungo mshambuliaji wa Tumbaku FC, Andendeksye Mwalupanga ndiye aliyekatiza ndoto za Burkina FC kusonga mbele baada ya kufunga bao pekee dakika ya 51 kwa mpira wa adhabu ndogo kufuatia mlinzi wa Burkina kufanya madhabu nje ya 18 ambapo mpira huo ulijaa katika nyavu.
Jitihada za Burkina FC kutaka kusawazisha hazikuweza kuzaa matunda licya ya kuongozwa na beki mkongwe Lulanga Mapunda na kujikuta wakitupwa nje ya mashindano.
Timu nyingine zilizofuzu ni pamoja na Kilakala FC iliyomtandika Wales FC bao 3-0 huku Sarange FC wakikung’utwa bao 2-0 na Watukavu FC kupitia mabao yalipachikwa wavuni na mshambuliaji Keneth Mzulu.
Lubungo FC iliwatambia Gereji kwa kuila jumla ya bao 5-4 kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoa sare ya bao 1-1 katika dakika za kawaida wakati Mavaza yenyewe ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Maskani.
Katika michezo mingine ya hatua hiyo ya 16 bora vijana wa Moro Kids FC iliwatoa nishai Jamaika kwa kuicharaza bao 2-1 huku Kaizer Chief ikipata ushindi mnono mbele ya Don Bosco kwa kuilaza bao 3-1 ambapo jana michezo ya hatua ya robo fainali ilitarajia kuchezwa kwenye uwanja huo wa Sabasaba.
Afisa Habari wa The Gunners Bonanza Cup 2015, Hamad Bakari alisema kuwa mashindano hayo yamekuwa na msisimko na timu kuonyesha ushindani wa kiwango cha juu.
“Haya mashindano yana ushindani wa hali ya juu na tunatarajia kumpata bingwa halali aliyepata ushindi kwa jasho lake.”alisema Bakari.
Bakari alitaja zawadi za mshindi wa kwanza kuwa akatabidhiwa pea 15 za viatu huku mshindi wa pili akiondoka na zawadi za seti tatu za jezi wakati mshindi wa tatu atakabidhiwa mipira mitatu na wa nne ataambulia mipira miwili.
Mchezaji bora atakabidhiwa pea moja za viatu huku Kipa bora akiondoka na glovisI pea moja.
0 comments:
Post a Comment