BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HIZI NDIZO MBINU WALIZOPEWA WANAWAKE ILI KUJIKWAMUA KIUCHUMI.

 

Wanawake wakiwa wamebeba kichwani Uwele katika ndoo maalum baada ya kuvuna shambani.

WANAWAKE katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujiunga na vikundi vya ujasiriamali, hatua ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuleta mapinduzi ya kimaendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Same, Padri Filbert Richard wakati wa kuvunja Mzunguko wa Kikoba cha kikundi cha Maendeleo-Jauma kilichopo wilayani Mwanga mkoani hapa, ambacho kipo chini ya usimamizi wa kanisa hilo, Idara ya Maendeleo Kitengo cha Maendeleo ya Wanawake na Jinsia.

Padri Richard alisema, wanawake wana uwezo mkubwa wa kuleta mapinduzi ya kimaendeleo katika jamii, hivyo ni vyema wakahakikisha wanajiunga katika vikundi na kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo, ambayo itawasaidia kuinua vipato vyao na kuwaondoa katika hali ya utegemezi.

"Akina mama tambueni kuwa ninyi ni watu muhimu sana katika jamii, mnaweza kuleta mabadiliko na mapinduzi makubwa ya kimaendeleo, sasa niwaombe msiridhike na hapo mlipofika, endelezeni juhudi na kuhakikisha mnajiunga katika vikundi, ili kusonga mbele zaidi na kujikwamua kiuchumi,"alisema.

Akizungumza Mwalimu Juma Mmbaga, aliwataka akina mama kuwalea watoto wao katika misingi na maadili mema, hatua ambayo itasaidia kupunguza tatizo la watoto wa mitaani, ambalo limekuwa likiongezeka kila kukicha.

"Ndugu zangu akina mama, ninyi ndio walezi wakubwa wa familia, niwaombe muwalee watoto wenu katika misingi na maadili bora na msikubali kuwaacha wawe wazururaji na ombaomba mitaani, kwani hali hiyo imekuwa kikwazo na tishio katika jamii nyingi,"alisema.

Awali akisoma risala ya Kikundi cha Wanawake cha Maendeleo, Hidaya Mmasa, mbali na kulishukuru Kanisa Katoliki Jimbo la Same kwa kuwawezesha kuanzisha kikundi hicho cha Vikoba, walisema kwa sasa wanalengo la kuanzisha duka kubwa la bidhaa mbalimbali, ambalo litawawezesha kuongeza vipato vyao na kusonga mbele zaidi.

Jimbo Katoliki la Same kupitia Idara ya Maendeleo Kitengo cha Maendeleo ya Wanawake na Jinsia, mpaka sasa lina vikundi 38 vya ujasiriamali na vikoba vya wanawake, katika Wilaya ya Same na Mwanga, ambavyo wamevianzisha, kwa lengo la kuwakwamua wanawake kiuchumi na kuwaondoa katika hali ya utegemezi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: