MGOMBEA URAIS WA CCM APACHIKWA JINA LA TINGATINGA NA RAIS JAKAYA KIKWETE, NI KUJAZA MAFUTA ILI LIFANYE KAZI BILA KUCHOKA.
Dar/Dodoma. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.
Rais Kikwete alisema hayo baada ya Magufuli kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliopigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kuzoa kura 2,104, sawa na asilimia 87.08, ushindi ambao alisema unaakisi kumalizika kwa makundi yaliyoibuka kwenye mbio za kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Balozi Amina Salum Ali alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 253 (sawa na asilimia 10.4), wakati Dk Asha Rose Migiro alikuwa wa mwisho kwa kupata kura 59 (asilimia 2.4). Jumla ya kura zilizopigwa kwenye mkutano huo mkuu zilikuwa 2,422 na kura sita tu ndio ziliharibika.
“Kila mtu anaitwa jembe,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akianza kutaja sifa za Magufuli ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na pia Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
“Lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumili ujinga, ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza.”
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na makubaliano.
“Tunaamini kuwa utawaongoza Watanzania vizuri,” alisema Kikwete akimgeukia mbunge huyo wa Chato.
“Tulikuwa na wagombea 338 lakini sasa tunaye mmoja na tuna kundi moja tu la CCM. Timu Magufuli imeshaondoka. Wengi walidhani CCM itafia hapa, lakini ushindi huu ni ishara kuwa CCM ni moja.
“Tunatakiwa kuacha kuteuwa watu kwa urafiki na kujuana ili tushinde kwa sababu imani huzaa imani. Sina shaka kuwa tutashinda lakini ushindi hauji hivi hivi lazima tuwe na mikakati mizuri, mipango thabiti na utekelezaji makini,” alisema.
Rais Kikwete ni mmoja kati ya watu wengi waliohojiwa na Mwananchi kuhusu mteule huyo wa CCM, ambaye hakuwa akitajwa kama kinara kwenye mbio za urais kabla ya kufikia hatua hiyo ya kujadiliwa na vikao vya juu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
Iyombe alisema kwa kipindi alichofanya kazi na Magufuli ameshuhudia kuwa hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na mwenye umakini mkubwa kwa kila anachofanya.
“Ninachoweza kusema ni kuwa huyu hataki mchezo, kwa hiyo wale wavivu wavivu najua watashindwa kuendana na kasi yake ya utendaji kazi,” alisema.
Iyombe alimmwagia sifa Magufuli kuwa hapatani na wazembe na wavivu, jambo ambalo alisema liliwahi kuwakimbiza baadhi ya wahandisi walioajiriwa wizarani hapo.
“Tangu alipoingia wizarani 2005, kama naibu waziri alianza kufanya kazi vizuri, sina sifa zaidi kuwa ni mchapa kazi, hawezi kuwa na upendeleo kulingana kabila, wala undugu. Hajali kitu, ukiharibu kazi atakuponda tu,” alisema.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Segolena Francis alimsifu Magufuli kuwa ni mtu anayejali muda, anayependa kazi yake na asiyetaka mtu legelege.
“Nimejifunza mambo mengi kwake na ninatumaini kuwa kama atakuwa Rais, basi Taifa litakuwa limepata mchapakazi. Anafuatilia kila kitu yeye mwenyewe, hana makundi, hana ukabila wala udini,” alisema.
Segolena alisema Magufuli ni miongoni mwa viongozi ambao hawapendi kupindisha mambo na wanataka kila kitu kiende kama kilivyopangwa.
Aliyesoma naye alonga
Sifa kwa Dk Magufuli pia zilitolewa na Ndyesumbilai Florian, mmoja wa watu waliosoma naye Shule ya Sekondari ya Katoke Biharamulo na ambaye sasa ni mhariri msanifu wa gazeti la Mwananchi.
“Magufuli aliwahi kusema kuwa siku moja atakuwa kiongozi mkubwa na hivyo ndoto hizo zinaweza kutimia baada ya kuteuliwa kuwania urais kupitia CCM,” alisema Ndyesumbilai.
Ndyesumbilai alisema hata walipokuwa kidato cha tatu, Magufuli alizungumzia nia ya kugombea Jimbo la Biharamulo wakati huo likishikiliwa na Chief Kasusula.
“Nafikiri aliwahi kugombea lakini hakufanikiwa, lakini mara kadhaa alikuwa akisema kuwa anatamani majimbo ya ubunge yashikiliwe na vijana,” alisema.
Ndyesumbilai alieleza zaidi kuwa hata baada ya kufanikiwa kuwa mbunge wa Chato, bado Magufuli aliendelea kusema kuwa safari ya uongozi bado ni ndefu kwake.
Wananchi wamkubali
Ushindi wa magufuli pia ulikuwa gumzo na faraja kwa baadhi ya wananchi, akiwamo wakuru Sinde warioba, ambaye aliamua kujipongeza kwa kupata bia mjini Dodoma.
“Magufuli hajanipa chochote, lakini tangu niliposikia anagombea urais nilikuwa nasali siku zote ili ashinde na bila shaka Mungu kanisikia kwa sababu ni masikini mwenzangu, ametoka kwenye kwenye tabu kama mimi. Sina hela ila nimekuja kunywa pombe kwa sababu Magufuli kapita,” alisema Warioba (60) mkazi wa Samora.
Dereva wa teksi mjini hapa, Chausi Katuma alisema Dk Magufuli ni mtu asiye na makundi na kwamba atasaidia kukirudisha chama hicho, lakini anatakiwa kujipanga zaidi kwa sababu ana changamoto kubwa sana.
“Dk Magufuli ni mtu “neutral’ (asiyefungamana na upande). Ukiangalia tangu awali hakuwa na kambi na hata kama ilikuwepo haikuwa kali. Lakini lazima ajipange kwa sababu asije akawa kama JK, wakati anaingia tulikuwa na matumaini makubwa lakini alichokifanya sicho tulichotarajia,” alisema Katuma.
Uteuzi huo unaonyesha kubadilisha upepo kwa baadhi ya vijana waendesha bodaboda ambao juzi baada ya kukatwa Lowassa waligadhabika na kutishia kuwa hata kama walikuwa ni makada wangehamia upinzani.
Omari Haule, mwendesha bodaboda wa Area D mjini hapa, alisema uteuzi huo si mbaya kwa sababu Magufuli hakuwa na kundi na utendaji wake ni mzuri hivyo kidogo CCM imeonyesha kutafuta mtu anayekabiliana na mtu waliokuwa wanamtaka.
“Nafsi kuridhika sana baada ya Lowassa kukatwa bado kwa sababu hatuwezi kujua huyu aliyeteuliwa bila kujali chama chake. Hatuwezi kujua kuwa atatusaidia kama tulivyotarajia kwa Lowassa,” alisema Haule.
Hata wakati wengine wakifurahia kukamilika mchakato huo, baadhi hawataki kuamini kuwa mambo yameshakamilika.
Mkazi wa Nkuhungu, Alex Kilatu alisema mchakato haujenda vizuri kwa sababu inaonekana kwa makusudi walimuandaa Dk Magufuli kushika cheo hicho lakini “aliyestahili alikuwa Edward Lowassa”.
“Sina mashaka na Dk Magufuli kuteuliwa kuwa Rais, lakini kwa sababu yametokea basi ndiyo hivyo. Ila kutoka moyoni sijafurahi asilimia 100 kwa kuwa mchakato haukuwa sawa kwa sababu hata wajumbe wa NEC (Halmashauri Kuu) walionyesha wazi mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuwa walimtaka Lowassa,” alisema Kilatu.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment