MOSHI MWEUSI WATANDA KATIKA VIKAO VYA KUWAJADILI NA KUWACHUJA WAGOMBEA URAIS CCM MJINI DODOMA
MOSHI mweusi umezidi kukikumba Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya makada wa chama hicho wakiwemo wagombea urais kushindwa kuelewa ni nini kinachoendelea katika suala mzima la vikao vya kuwajadili na kuwachuja wanaowania kuteuliwa na chama kupeperusha bendera ya CCM.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wale wa Mkutano Mkuu kuendelea kujadili kinachoendelea kila wanapokutana kwenye vikundi na kwenye baa.
Awali ilitarajiwa kwamba Kamati Kuu ingetangaza majina ya makada watano waliopitishwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye NEC ili kupigiwa kura, lakini hali iliendelea kutawaliwa na ukimya mkubwa, huku wengi wakiwa hawajui kinachoendelea.
Kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imetangazwa na CCM Kamati Kuu ilitarajiwa kumaliza kazi zake jana, lakini hadi saa mbili usiku, hakuna aliyekuwa akijua kinachoendelea.
Baadhi ya wadadisi walisema ratiba tayari imevurugika, kwani baada ya kumalizika kikao cha Kamati ya Maadili, ilikuwa zamu ya Kamati Kuu kuja na majina hayo na kuondoa 33, lakini kinyume chake hali imezidi kuwa kimya.
Habari ambazo zilipatikana mjini Dodoma jana, zilieleza kuwa Kamati Kuu ilitarajia kukutana mara baada ya Rais Kikwete kuvunja Bunge. Baada ya Bunge kuvunjwa waumini wa dini ya Kiislamu walienda kufuturu, huku kukiwa na uvumi kwamba kikao hicho kitafanyika baada ya kufuturu.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu majina ya waliopitishwa na CCM kwa ajili ya kupelekwa kikao cha NEC yanatarajiwa kutangazwa leo.MAJIRA.
0 comments:
Post a Comment