UTEUZI WA MGOMBEA KWA UPENDE WA URAIS NDANI YA CCM, ANAPITA KATIKA NJIA NYEMBEMBA, WALIONDISHWA UNENE UMEWADHURU !.
Aliyekuwa mmoja wa wagombea katika kinyang'anyiro cha urais ndani ya CCM, Mhe Edward Lowassa ambaye hakuweza kuvuka hatua ya pili katika vikao vya mchujo kati ya watia nia 38 mjini Dodoma.
Ndugu wasomaji wangu leo, siku ambayo CCM inatarajiwa kumteua na kumtangaza mgombea wake wa urais, nimeona niendelee kuandika kuhusu chaguo lao litakuwaje bila kuathiriwa na mgogoro wa vizazi, Edward Ngoyai Lowassa, makundi na mitandao, ubara na uzanzibari na mwisho kabisa ukanda.
Leo nimeona nichague mambo makuu saba ambayo yanaweza kuifanya njia ya CCM kuteua mgombea makini wa urais kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa mwaka huu 2015 kuwa nyembamba sana kwa sababu mambo haya ni nyeti sana kwa siasa za Tanzania.
Yanaweza kuamua nani awe mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM ikizingatiwa kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi nchini, mwaka huu muungano wa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), yaani Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na NLD utasimamisha mgombea mmoja katika nafasi zote kuanzia udiwani, ubunge na urais. Sasa hebu twendeni pamoja kuyajua haya mambo.
1.0.Bila kuathiriwa na mgogoro wa vizazi
Nimeandika mara mbili kwenye kolamu yangu hii kuwa uchaguzi wa mwaka huu utataliwa na uzee na ujana na ndio maana kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania na CCM vijana wengi sana wamejitokeza kugombea nafasi ya urais.
CCM ina wakati mgumu kuukwepa mtego huu wa vijana ambao wanasema kuwa huu ni wakati wao kuingia na kuendesha nchi yao huku wazee nao waking’ang’ania kuendelea kuongoza usukani wa nchi yao. Ukiteua mzee, vijana watanuna na ukiteua kijana wazee watanuna.
2.0. Bila kumteua Lowassa
Hiki ni kitanzi kwa CCM kwamba unawezaje kuteua mtu mwingine nje ya Lowassa ambaye tumeambiwa ana watu wengi sana wanaomuunga mkono kuanzia wanachama wa kawaida hadi viongozi katika ngazi zote za chama.
Ukiangalia sana kwa makini unaweza kudiriki kusema kuwa Lowassa ni chama ndani ya chama au anaweza kuwa mkubwa kuliko hata CCM kwa kuungwa mkono, hivyo ni lazima ateuliwe yeye ili CCM kibaki salama. Utaweza kushindwa kumteua Lowassa ambaye ni mlima na wengine ni vichuguu.
3.0.Bila kuathiriwa na makundi na mitandao
Ndani ya CCM kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 tulianza kuona mitandao ikianza kuota ndani ya CCM na mtandao uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani uliongozwa na Lowassa na hata sasa kuna mitandao mikuu na midogo midogo ikiendelea ndani ya CCM. Unapataje mgombea wa kupeperusha bendera ya CCM bila kuathiriwa na mitandao au makundi ya wagombea na ukabaki salama kama chama kimoja na kushinda uchaguzi.
Mtu anayekusudiwa kuteuliwa lazima awe ni yule ambaye atakuwa mwenyekiti wa chama baada ya uchaguzi na ana uwezo wa kukiunganisha chama kuwa kimoja na kuondokana na mitandao na makundi yaliyopo sasa kwa ajili ya uteuzi wa mgombea.
4.0. Bila kuathiriwa na ubara na uzanzibari
Kuna kanuni ambazo hazijaandikwa katika siasa za hapa Tanzania ambazo zina nguvu sana kwani marais hupokezana kati ya Tanganyika na Zanzibar ingawaje wakati mwingine zinavunjwa kulingana na mazingira kama mtakavyoona hapo mbele kwani Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere (1961-1985) akitokea upande wa Bara, wa pili alikuwa Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) akitokea Zanzibar, wa tatu alikuwa Benjamin William Mkapa (1995-2005) ambaye alitoka Bara na sasa ni Jakaya Kikwete (2005-2015) anayetoka Bara akiwa amevunja mwiko wa kubadilishana viongozi kati ya Bara na Visiwani.
Mtindo huu unafaa tu kama ni mfumo wa chama kimoja cha siasa, lakini katika mfumo huu wa ushindani wa vyama vingi vya siasa unaweza usiwe na nguvu sana ingawaje CCM wanajaribu kutaka kutumia karata hii kwamba zamu hii ni ya Wazanzibari na ndipo hoja ya Mzanzibari Mkristo inakuja kuwa na nguvu sana.
5.0. Bila kuathiriwa na ukanda
Kuna maeneo kadhaa ya nchi kwa maana ya kanda ambayo yametoa marais hapa nchini. Rais Nyerere alitoka Kanda ya Ziwa, Rais Mwinyi alitoka Kanda ya Zanzibar, Rais Mkapa alitoka Kanda ya Kusini na Rais Kikwete ametokea Kanda ya Pwani.
Kwa hiyo kama hoja ya ukanda itakuwepo hatutarajii kuwa CCM itateua wagombea kutoka kwenye kanda hizi tena kwani walishakula kota zao za marais. Sasa matarajio ni wagombea kutoka Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Magharibi baada ya wa Kanda ya Nyanda za Juu na Kanda ya Kati kuenguliwa.
6.0. Bila kuathiriwa na Ukristo na Uislamu
Tangu nchi huru za Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964 na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumekuwa na kanuni nyingine ambayo haijaandikwa na ambayo ina nguvu sana katika siasa za Tanzania kwamba marais wamekuwa wakibadilishana kwa kufuata dini mbili kuu za Ukristo na Uislamu.
Rais Nyerere alikuwa Mkristo, Rais Mwinyi (Muislamu), Rais Mkapa (Mkristo) na Rais Kikwete (Muislamu).
Kama kanuni hii itaendelea kutumika, basi mgombea urais wa CCM ajaye lazima awe ni Mkristo na vyama vya Ukawa vitalazimika kuteua mgombea ambaye ni mkristo ili kukidhi matakwa na matarajio ya wapigakura. Chama ambacho hakitafuata kanuni hii kitakuwa kinajichimbia kaburi kwenye uchaguzi wa mwaka huu, maana wananchi wanatarajia wagombea Wakristo.
7.0. Kwa kujua kuwa kuna Ukawa
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii vyama vichache na vyenye nguvu vimeungana kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu, hili si jambo dogo hata kidogo ni jambo kubwa na siuoni Ukawa ukivunjika kabla ya kutimiza azma yao ya kuchukua dola.
Kama CCM ni chama makini katika kufanya mambo yake hasa katika kugombea mamlaka ya dola ambacho kina uzoefu nalo wakati wa kufikiria hoja zote nilizoziorodhesha hapo juu pia kitafikiria kuhusu mshindani wake mkuu, yaani muungano wa Ukawa angalau hata kwa kubashiri tu kuwa ni nani kinakusudia kumsimamisha kwenye nafasi hiyo hiyo na kitajibu vipi mapigo kama kitamteua huyu au yule.
Hivyo basi Ukawa ni hoja nzito sana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ya kuzingatiwa na CCM katika uteuzi wa mgombea wake kuelekea uchaguzi huu.
Hitimisho
Kwa kuhitimisha niseme tu kwamba ebu wasomaji wangu mtumie makala hii kama orodha ya vigezo vya kuzingatiwa wakati mnaangalia mgombea aliyeteuliwa na CCM kujua walitumia vigezo gani hasa au walikuwa wanakwepa viunzi gani hasa ili watimize jukumu lao la kuteua mtu makini na mahiri atakayepeperusha bendera yao. CCM wana kazi kubwa sana kwasababu wako madarakani na kwa kuwa madarakani muda mrefu wamefanya makosa mengi sana ambayo yanawatafuna wanapoanza kufikiria kuteua mgombea wao kati nafasi hii.
Jambo jingine muhimu ni huo muungano wa Ukawa ambao haujawahi kuwepo tangu kuanzanishwa kwa vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992, hivyo chaguzi zote nne yaani wa 1995, 2000, 2005 na 2010 CCM imepata wepesi kushinda chaguzi hizo kutokana na sababu kubwa ya kugawanyika kwa vyama vya upinzani na kila kimoja kwenda peke yake kwa kudhania kuwa unaweza kushinda bila kumtegea mwingine. Kitendo cha Ukawa kuamua kuweka mgombea mmoja katika kila nafasi ya udiwani, ubunge na Urais sio jambo dogo kwa CCM hata kidogo.
Kitendo cha vyama vilivyoko kwenye muungano wa Ukawa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Desemba 2014 imewapa mafunzo mengi ambayo wanaweza kuyazingatia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuyakwepa makosa yaliyotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kutegemea kufanya vizuri zaidi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015.
*Mwandishi wa makala hii ni kiongozi katika sekta ya kiraia kwa miaka 25, mchambuzi wa kisiasa na kijamii, msomaji wa gazeti la Mwananchi pia ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) katika sayansi ya siasa na anapatikana kwenye simu namba 0713 612681 na baruapepe: mwakagendah@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment