BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WASEMAVYO WALIOTINGA 5 BORA YA URAIS CCM, ASHA-ROSE MINGIRO.

 

Asha-Rose Migiro 


Ingawa hakuwa akitajwa mara kwa mara kwamba ni mmoja wa wagombea tishio, kupitishwa kwa jina la Dk Asha-Rose Migiro kuingia katika tano bora ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, siyo jambo la ajabu.


Rekodi yake kitaifa na kimataifa lakini pia jinsia, ni mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa Waziri huyo wa Katiba na Sheria, kuvuka hatua hiyo ya kwanza.


Dk Migiro ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM, alijitosa katika safari ya kuelekea Ikulu Juni 15 pasi na mbwembwe za aina yoyote.


Mtanzania huyo ambaye aliweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza mwanamke kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), alikuwa akitajwa kuwa anaweza kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.


Hakuwahi kutangaza nia kama ilivyokuwa kwa makada wengine waliotumia fursa hiyo kuelezea mikakati yao lakini pia, hakuwa na mbwembwe katika kutimiza sharti la kusaka wadhamini mambo ambayo pengine yalimwongezea sifa za kupitishwa miongoni mwa wagombea 38 waliokuwa wamechukua na kurejesha fomu kuomba nafasi hiyo ya juu kabisa katika utawala wa nchi.


Lakini kigezo kingine kilichomvusha ni umakini wake na kutokulengwa na mishale ya kashfa ambazo ziliwakumba mawaziri kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Tano na yote hayo yanampa fursa kubwa ya kufika mbali katika safari yake hiyo hasa ikiwa hoja ya nafasi ya wanawake kushika urais kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa Spika wa Bunge la 10 itatiliwa maanani.


Dk Migiro alianza kutajwatajwa miongoni mwa wanaoweza kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza mkataba wake Umoja wa Mataifa na kurejea nchini na mara moja kuteuliwa kuwa mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria.


Msimamo wake
Wakati akizunguka katika mikoa mbalimbali kusaka saini za wadhamini, Dk Migiro alikuwa makini katika kuzungumza huku akisisitiza kuwa anasubiri Ilani ya CCM... “Na mimi nitaweka mikakati ya kuendeleza yale ambayo yameshafanyika. Sasa endapo nitapata ridhaa ya chama changu, nyenzo yangu kuu itakuwa ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM.”


Alisema kwa kuwa uchumi umeendelea kukua awamu hadi awamu, naye atahakikisha kukua huko kunawafikia wananchi wengi zaidi: “Nitahakikisha kuwa mambo haya yaliyofanywa na awamu za uongozi zilizopita yanakuwa stahamilivu na endelevu na kuwafikia wananchi walio wengi zaidi.”


Wasemavyo alikozaliwa
Gazeti hili limefanya mazungumzo na kaka yake, Ally Shaban Mtengeti (79) ambaye anasema, Asha ni wa sita kuzaliwa katika familia yao.


Anasema mdogo wake huyo hana makuu na anapenda watu lakini asiyependa kuonewa.


Mtengeti anasema Asha ana nyota ya uongozi kwa kuwa alianza kuongoza tangu akiwa chuo kikuu ambako alikuwa mbunge kwenye baraza la vyuo vikuu.


Wananchi wengi wa Tarafa ya Usangi wilayani Mwanga, Kilimanjaro anakotokea, hawamfahamu kwa sura japo wamekuwa wakimsikia kupitia vyombo vya habari.


Migiro anaishi zaidi nje ya Mwanga kwa sababu mama yake ni mtu wa Dar es Salaam na kwa kiasi kikubwa amelelewa na mama na Mwanga alifika baada ya kifo cha baba yake.


“Sijawahi kumuona lakini nimekuwa nikisikia jina lake kwenye vyombo vya habari na hata huku anafika mara chache, lakini kutokana na shughuli za hapa na pale sijawahi kufika kwake kumuona” anasema Mohamed Kabewa, mkazi wa Kijiji cha Mshewa, Kata ya Chomvu.


Kauli ya Kabewa ya kutomfahamu kwa sura au kutowahi kuzungumza na Dk Migiro ilizungumziwa na majirani zaidi ya watano wanaozunguka nyumba ya Shaban Mtengeti ambaye ni baba mzazi wa Dk Migiro.


Licha ya kutomfahamu, wananchi wa Chomvu na Tarafa ya Usangi wanasema anazo sifa za kuongoza kwa kuwa amewahi kuwa kiongozi katika maeneo mbalimbali na kote alikoongoza hajakumbana na kashfa yoyote.


Kabewa anasema licha ya mfumo dume katika jamii, wananchi wanatakiwa kuangalia utendaji wa mtu na uwajibikaji wake.


Hata hivyo, wananchi wengine, Hussein Mkodo na Rose Mfinanga wanaonyesha shaka kama mwanamke akipewa nafasi hiyo ya ngazi ya juu nchini ataweza kuongoza kutokana na hali ya nchi ilivyo.


Wananchi hao walizungumzia kukithiri kwa vitendo vya ufisadi na kuelezea shaka yao kama Dk Migiro ataweza kukemea hasa ikizingatiwa kwamba hilo limewashinda viongozi wengi.


Mkodo anasema wenye fedha wanaonekana kuvinunua baadhi ya vyombo vya dola na hivyo kuwa na nguvu kuliko vyombo hivyohivyo hali ambayo anasema hata Dk Migiro akipewa nafasi hiyo ya uongozi wa juu, itamuwia vigumu kupambana na wala rushwa.


“Dk Migiro ni msafi hatujasikia akituhumiwa popote lakini


Tuna shaka kama hao wanaosema Sh10milioni ni fedha ya mboga, ataweza kuwashtaki maana watu hao wapo ndani ya chama, ”alihoji Mkodo.


Mkodo alisema kwa sasa Watanzania wanatakiwa kufanya mabadiliko kwa sababu kwa miaka 50 wana kunywa pombe ileile, wanachokifanya ni kubadili chupa tu.


Anasema Watanzania wanaishi kwa mashaka kwa kuwa viongozi wameshindwa kusimamia masuala nyeti na kusababisha wananchi kuishi ya taabu, huku wanasiasa wakijinufaisha kupitia mgongo wa wanyonge.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: