Mgombea urais kwa tiketi ya CCM,Dk John Magufuli akihutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Mbalizi, Mbeya jana. Picha na CCM
Songwe/Arusha. Mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amewashauri Watanzania kutoharakisha kutaka mabadiliko na mapinduzi yasiyo na mipango kwa kuwa baadhi ya nchi zilizofanya hivyo, sasa zinajutia uamuzi wao.
Mgombea huyo jana alitumia sehemu kubwa ya mikutano yake kuwaeleza wananchi kuwa anao uwezo wa kukidhi kiu yao ya mabadiliko wanayoitaka, hivyo hakuna haja ya kuhadaiwa na watu wanaolazimisha ukombozi na mabadiliko bila kufanya tathmini ya kina.
Akiwahutubia wakazi wa Mbalizi, Mbeya Vijijini, Dk Magufuli alisema mabadiliko bora yanaweza kuja hata bila kubadilisha chama kwenye uongozi. Akisema hiyo ilitokea kwa Chama cha Kikomunisti cha China ambacho kilifanikiwa kuifanya nchi hiyo ikue kwa kasi kiuchumi duniani kiasi cha kuishinda Marekani.
Alisema nchi kama Libya, Tunisia, Iraq na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wananchi wake walilazimisha mabadiliko lakini leo wanajuta.
“Msitoe hukumu ya jumla, zipo nchi zilifanya hivyo zinajuta. Libya ya (Hayati Muammar) Gadaffi ulikuwa ukioa unapewa nyumba, unatafutiwa mtaji, maji, elimu na umeme bure lakini wananchi walichoka raha,” alisema.
“Wakasema anaondoka lakini leo hii hakuna raha na wale vijana waliotaka ukombozi wa haraka ndiyo wa kwanza kuvuka Bahari ya Mediterranean kwenda Ulaya.”
Aliwaomba Watanzania wamwamini na kumpigia kura kwa kuwa akiingia Ikulu hatakuwa na deni la kulipa kwa sababu hakupata nafasi ya kugombea urais kwa kuwalipa watu ili wamteue.
Alisema mchakato wa uteuzi aliufanya kwa mwongozo wa Mungu ndiyo maana hata fomu za uteuzi wa mgombea urais ndani ya CCM alichukua na kurudisha kimyakimya. “Wapo watu wengine walitumia pesa ili wachaguliwe, lakini walipoona mimi nimechaguliwa wameanza kukimbia wenyewe,” alisema Dk Magufuli.
Alisema wapo baadhi ya watu wanamchukia kutokana na misimamo yake ya kiutendaji na kukemea rushwa ndiyo maana alipoteuliwa baadhi yao ndani ya CCM walikimbia mapema.
Mgombea huyo ambaye ameendelea na kampeni zake katika mkoa mpya wa Songwe, alisema akiingia madarakani atakomesha ujangili wa wanyamapori kwa kuboresha masilahi ya askari wa wanyama hao.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona tembo wanauawa kila siku na meno yao kushikwa nje ya nchi, licha ya kuwapo askari wenye bunduki za SMG wakati Wamasai wanachunga ng’ombe wao kila siku bila kuibiwa.
“Hivi kwani hakuna uwezekano wa kuwapanga maofisa kutokana na makundi ya tembo? Unampa tembo 30 kila askari halafu unamwambia nikute hata jino moja limeng’oka wewe na mimi na unampa mshahara mzuri,” alisema Dk Magufuli akiwa Mkwajuni wilayani Songwe huku akishangiliwa.
Alisema kuna watendaji wachache wanaofanya wananchi waichukie Serikali kwa kuiba fedha za maendeleo za halmashauri na kwamba akiingia wakurugenzi wote wa Manispaa na halmashauri ambao ni wazembe watakiona.
Waziri huyo wa Ujenzi, kila alikohutubia aliahidi kujenga barabara za lami na kumwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mbeya kutangaza zabuni za ujenzi wa barabara hizo haraka iwezekanavyo.
Akiwa Mbalizi, aliahidi kujenga kilomita moja ya barabara ya lami wakati Mkwajuni na Makongorosi aliahidi kujenga kilomita nne za ndani na kumalizia ujenzi wa Barabara ya Mbalizi – Chunya kwa lami kwa kuwa Songwe imeshakuwa wilaya.
Katika siku yake ya tano ya kampeni, Dk Magufuli aliahidi kuanzisha mfuko maalumu wa fedha za kutoa pensheni kwa wazee ili waweze kuishi vizuri na kutoa ushauri kwa vijana.
Samia Suluhu
Wakati Dk Magufuli akiwa mkoani Mbeya, mgombea mwenza wake, Samia Suluhu jana alikuwa mkoani Arusha ambako akiwa wilayani Longido Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Esuvat Naikala alisema jamii ya kifugaji inahitaji elimu zaidi ili ibadilike...
“Jamii ya wafugaji inaamini CCM imefanya haki katika hatua za udiwani na ubunge na watawachagua ila nafasi ya urais watamchagua mgombea urais wa Ukawa, najua bado nafasi ipo ya kubadili fikra hizo ili chama chetu kipate ushindi.”
Mbunge wa Longido aliyemaliza muda wake, Lekule Laizer alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo, lakini akawataka wana CCM kuwachagua wagombea wa chama hicho ili wawaletee maendeleo.
Alisema katika kupata mgombea urais wa CCM, taratibu na katiba vilifuatwa na Dk Magufuli alichaguliwa, hivyo wanachama wote wana wajibu wa kumuunga mkono mgombea aliyekubalika zaidi na kuvunja makundi.
“Kuhama kwa Edward Lowassa ni hiari yake, haina maana kila mtu amfuate huko alikoenda, kila mtu alijiunga CCM kwa mapenzi yake kwa kuamini ni chama bora kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu na kuleta maendeleo,” alisema Lekule
Kwa upande wake, Samia alisema Serikali imetenga kiasi cha Sh13 bilioni kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji kutoka Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Katika mkutano huo mgombea ubunge wa CCM, Dk Steven Kiruswa alitambulishwa, huku akitabiriwa kupata ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa Chadema, Onesmo Ole Nangole aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / siasa /
slider
/ MGOMBEA URAIS WA CCM AWAPASULIA JIPU KWA WANAOTAKA MABADILIKO NA MAPINDUZI KUWA YANA HASARA ZAKE KWA TAIFA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment