WAZIRI MKUU AWAMU YA TATU, FREDIRICK SUMAYE AJIONDOA CCM NA KUTIMUKIA ZAKE UKAWA JIJINI DAR ES SALAAM.
Video ya Fredirick Sumaye akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 22 hoteli ya Bahari Beach Dar es Salaam.
Historia imeendelea kuandikwa katika siasa za Tanzania baada ya leo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kujitoa CCM na kujiunga na chama kimojawapo kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi-(Ukawa).
Sumaye anakuwa Waziri Mkuu mstaafu wa pili kujiondoa chama tawala katika historia ya Tanzania, ambapo waziri mkuu wa kwanza kuhama CCM ni Edward Lowassa aliyejiunga Chadema miezi michache iliyopita.
Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam leo katika mkutano na wanahabari Sumaye amesema chama alichojiunga miongoni mwa vinne (Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD) vinavyounda Ukawa kitajulikana baadaye.
Waziri Mkuu huyo aliyehudumu Uwaziri Mkuu miaka yote 10 ya utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema amejiunga Ukawa kwa kushirikiana na viongozi wa umoja huo awatumikie Watanzania kwa kasi kubwa baada ya uchaguzi kwa kuwa anaamini Ukawa utashinda.
Amesema kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM na kuvurugwa kwa mchakato wa uchaguzi kumechangia wananchi kukata tamaa hali iliyochochea uungwaji mkono wa upinzani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
“Na sasa kuzuia wimbi la mabadiliko ni kazi kubwa sana. Naamini Ukawa watashinda uchaguzi huu, CCM wamezubaa wakidhani watashinda wakati wananchi wamechoka, wanahitaji mabadiliko” alisema na kuongeza.
“Sijajiunga Ukawa kwa kuwa mgombea wake wa urais anatoka Kanda ya Kaskazini, wala kwa kuwa viongozi wengi waandamizi wanatokea huko la hasha bali kutaka kutoa uzoefu wangu nikishirishiana na Lowassa katika uongozi wa nchi, alisema na kudai dhana kwamba hakuna maisha ya kisiasa nje ya CCM imepitwa na wakati.CHANZO: MWANANCHI DIGITAL
0 comments:
Post a Comment