DK MAGUFULI MTISHA EDWARD LOWASSA JUU YA AFYA, APIGA PUSH-UP NNE MKUTANO WA KAMPENI KAGERA.
MOJA, MBILI, TATU, NNEE !. Ndivyo anavyoashiria mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli kwa kufanya zoezi la ‘push up’ muda mfupi kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara mjini Kayanga, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera jana.
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli jana alifanya mazoezi ya viungo jukwaani kwa kupiga ‘push up’ kuthibitisha nguvu na uwezo alionao kuwatumikia Watanzania akichaguliwa. Alifanya mazoezi hayo katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika mjini Kayanga wilayani Karagwe.
Alisema wapo watu wanaosema ‘people’s power (nguvu ya umma) na kutaka hiyo nguvu apewe kwa kuwa anayo nguvu ya kutosha kuwatumikia Watanzania. “Nina power ya kufanya kazi,” alisema Dk Magufuli na kuanza kurukaruka kisha akasema, “Au nipige push up,” aliuliza na kuanza kufanya zoezi hilo na kushangiliwa na watu.
Aidha, akihutubia mkutano mjini Bunazi katika Wilaya ya Missenyi, Dk Magufuli alimfagilia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwa utendaji wake. Dk Magufuli alikuwa akizungumzia namna atakavyotatua kero ya kutolipwa fidia watu walioathiriwa na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wilayani Missenyi mkoani Kagera.
Alisema suala hilo litatatuliwa kwa kuzingatia haki huku akisifu kuwa Lukuvi ni waziri mzuri anayejitahidi katika utendaji wake. Alisema yeyote anayefuatwa na barabara au uwanja wa ndege ni lazima alipwe fidia.
Dk Magufuli ambaye jana alifanya mikutano katika majimbo yote ya wilaya za Karagwe, Kyerwa na Ngara, alisisitiza umuhimu wa wanasiasa kuahidi ukweli wakati wa kuomba kura. “Ni vyema nikahukumiwa vingine, lakini kusema uongo hapana! Ukisema ukweli unabarikiwa, lakini ukisema uongo unalaaniwa,” alisema Magufuli akiwa mjini Bunazi katika Jimbo la Nkenge.
Akiwa mjini Nkwenda wilayani Kyerwa, Magufuli alieleza kuguswa na umati wa wananchi uliojitokeza. Aliwaahidi, “sitawaacha, sitawatupa na sitawasahau...makaribisho haya makubwa nimebakiwa na deni, baada ya kuchaguliwa nisibaki na deni,” alisema.
Aliendelea kuzungumzia tatizo la bei ya kahawa na kuahidi kuhakikisha inapaa kwa kupunguza kodi. Aliahidi pia kuupatia mji wa Nkwenda barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano, sambamba na ahadi ya kuhakikisha barabara ya Omurushaka-Murongo inajengwa.
Katika hatua nyingine, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi amevitaka vyama vya siasa na wagombea wao kutowapa hofu wapiga kura ya kuwepo wizi wa kura baada ya kukamilika kazi ya kupiga kura.
Amevitaka vitambue kuwa jukumu la kulinda kura ni la kisheria na litafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Jaji Mutungi katika mahojiano na gazeti hili jijini Mwanza, alivitaka vyama vyote vya siasa viondoe “dhana hasi” ya kuibiwa kura hali aliyosema ndiyo imeleta matatizo ya kuundwa kwa vikundi vya ulinzi kwenye vyama hivyo.
“Jeshi la Polisi na Tume yaTaifa ya Uchaguzi wana jukumu la kisheria la kulinda kura hadi matokeo ya uchaguzi yatakapotangazwa, tusitake kuwaaminisha Watanzania kuwa vyama visivyoweka vikosi vyao vya ulinzi vitaibiwa kura,” alionya Msajili huyo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment