KOCHA MKUU WA KLABU YA SIMBA SC DYLAN KERR AFICHUA SIRI YA KUTANDIKWA BAO 2-0 NA WATANI ZAO YANGA SC MCHEZO WA LIGI KUU TANZANIA BARA.
Beki wa Yanga, Kevin Yondani (kushoto) akimdhibiti mshambuliaji wa Simba, Hamisi Kiiza wakati wa mechi ya Ligi Kuu iliyozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi. Yanga ilishinda 2-0. Picha na Said Khamis.
Dar es Salaam. Wakati kocha wa Simba, Dylan Kerr akiwatupia lawama mabeki wake kwa kukosa umakini, mwenzake Hans Pluijm wa Yanga amesema aligundua udhaifu huo na kutumia mbinu ya kucheza mipira mirefu iliyowapa ushindi wa mabao 2-0 juzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti muda mfupi baada ya mchezo huo, makocha hao kwa pamoja walieleza udhaifu wa mabeki wa Simba.
Kerr alisema: “Nimeumizwa mno na matokeo haya, mabeki wangu wamefanya makosa ya ajabu tena ajabu kubwa, tulitawala tukatengeneza nafasi nyingi mwanzo, lakini matokeo yake tumefungwa sisi.
“Viungo wangu walikuwa vizuri sana pongezi kwao vivyo hivyo kwa washambuliaji na ndiyo sababu mwanzo tulimiliki mipira, beki ilikuwa dhaifu, hakukuwa na maelewano baina yao, kila mmoja alicheza alivyojua yeye.
“Malengo yetu yalikuwa kuizua Yanga kucheza tangu mwanzo na kutawala katikati, lakini mabeki wameniangusha kwa kufanya uzembe, ukiangalia hata mabao ya Yanga ni ya uzembe wao.
“Tambwe (Amisi) shuti lake la kwanza alilopiga kipa (Peter Manyika) alilicheza na shuti lake la pili likazaa bao la kizembe kabisa, kukaba ilikuwa tatizo kwenye timu yangu,” alisema kocha huyo raia wa Uingereza.
Alisema japo kukosa pointi tatu si mwisho wa ligi, wanajipanga upya katika mechi yao ijayo na kusisitiza kuwa mchezo huo haujawakatisha tamaa katika harakati zao za kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa msimu huu.
Wakati Kerr akibainisha udhaifu huo, mwenzake Pluijm alisema alitumia dakika 30 za awali kuisoma Simba na kisha kubadili mfumo wa kikosi chake kwani kwa mfumo walioanza nao wasingeweza kupenya kwa viungo wa Simba.
Pluijm alisema Simba walikuwa vizuri katika safu yao ya viungo na ndiyo sababu waliutawala mchezo huo mwanzoni, lakini ilikuwa dhaifu upande wa mabeki na aliliona hilo na kuamua kucheza mipira mirefu.
“Kwa uwezo wa viungo wa Simba tusingeweza kupenya, tulichokifanya ni kucheza mipira mirefu kwa washambuliaji wetu baada ya kubaini udhaifu wa beki ya wapinzani wetu, mbinu ambayo imetupa ushindi,” alisema Pluijm.
Makocha hao ambao baada ya mchezo huo walizungumza kwa dakika 10 wakibadilishana uzoefu wa soka katika timu zao huku Kerr akimpa pongezi Pluijm kwa ushindi huo na kumwambia kuwa kuna vitu amejifunza licha ya kufungwa.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kucheza na timu yao, ushindani wa timu hizi mbili ni mkubwa sana, nimejifunza vitu vingi katika siku hii, pia hongera kwa ushindi,” yalikuwa ni baadhi ya maneno yaliyosikika Kerr akimwambia Pluijm, ambaye pia alimuelezea uzoefu wake na timu hizo mbili tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa Yanga.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika baada ya mkutano wa makocha hao na wanahabari muda mfupi baada ya mchezo wa timu zao.
Vituko vya mashabiki
Kabla ya mchezo huo, mashabiki wa timu zote mbili walionekana kutambiana hasa wale wa Simba ambao walionekana kuiamini timu yao ingeibuka na ushindi.
Mwananchi ilishuhudia baadhi ya mashabiki wa Simba wa tawi la Karume wakiwa wamechimba shimo mfano wa kaburi katika eneo hilo na kuweka boksi mfano wa jeneza pembezoni ya shimo hilo huku juu yake wakiweka mafiga na chungu kilichokuwa kimechorwa ishara ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga.
Katika kusherehesha ushabiki, mashabiki hao ambao walivalia jezi nyekundu waliandika bango lililosomeka kuwa kifo cha Yanga kimefika na tayari wameandaa kaburi kwa ajili ya mazishi licha ya kwamba baada ya dakika 90 matokeo yakawa kinyume.
Maeneo ya Veta mataa, mashabiki wa Yanga waliwaacha wapita njia vinywa wazi saa tatu kabla ya mchezo huo baada ya kuanza kucheza mduara katikati ya barabara mbele ya askari wa usalama barabarani waliowakamata kufuatia gari yao aina ya Coastal kuvuka kwenye taa nyekundu.
Wakati trafiki akiwahoji na kutaka kuwaandikia, mashabiki hao walianza kupiga ngoma huku baadhi wakicheza mduara mbele ya askari hao wakiimba nyimbo za kuisifia timu yao kabla ya kuachiwa dakika chache baadaye.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment