MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameahidi kushughulika na mmoja wa mawaziri aliyegawa ranchi za mifugo kiholela.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, alipohutubia mikutano ya kampeni iliyofanyika katika miji ya Muleba na Kamachumu mkoani Kagera.
Alisema hawezi kukubali kuona wananchi wanaendelea kuteseka wakati watu fulani wanamiliki ranchi hizo, huku migogoro isiyomalizika ikiendelea kufukuta.
Hata hivyo, katuika mkutano huo, Dk. Magufuli hakumtaja waziri huyo wala alikuwa katika serikali ya awamu gani, isipokuwa alisisitiza kupambana naye akiingia madarakani.
“Ninajua hapa kuna mgogoro wa ranchi ya Rutoro ambayo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela amesema anaushughulikia. Nawaambia mkoa wenu una ranchi 52 ambazo zimegawiwa kiajabuajabu.
“Hakuna jambo linalomuumiza kichwa Rais Kikwete, kama uamuzi huu wa mtu mmoja kugawa ovyoovyo maeneo haya kwa watu ambao hawana ng’ombe wala mbuzi…nasema hili hapana.
“Sitawaangusha, tutakwenda kupambana na watu hawa ambao wameharibu,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema hayuko tayari kuona wananchi wanaumia kwa makosa yaliyofanywa na watu walioaminiwa katika utendaji serikalini.
“Kama mtanichagua kuwa rais, tutagawa baadhi ya maeneo na kuwapa wananchi ili wapate maeneo ya malisho ya mifugo na kilimo,” alisema Dk. Magufuli.
SOKO LA KAHAWA
Kuhusu soko la kahawa, mgombea huyo alisema anatambua changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Alisema anashangazwa na bei ya kahawa inayotoka Kagera kwenda Uganda kuwa na soko kubwa, wakati nchini bei imezidi kushuka kila kukicha.
“Ikulu ni ya Magufuli na CCM, wengine wasindikizaji. Msiwasikilize, ninaomba kura zenu zote Watanzania,” alisema.
Alisema anaomba urais kwa ajili ya kuwatumikia wananchi ambao wanaonekana kukatishwa tamaa na baadhi ya watendaji wa serikalini ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao.
AHADI YA MELI
Alisema ahadi iliyotolewa na Rais Kikwete kila ziwa kubwa kuwa na meli iko palepale.
Aliwaasa wananchi wa Kagera kuepuka kauli za wanasiasa kufanya ajenda ya meli kuwa mtaji wa kuombea kura.
TIBAIJUKA APIGA MAGOTI
Katika hatua nyingine, mgombea ubunge Jimbo la Muleba Kaskazini kupitia CCM, Profesa Anna Tibaijuka, aliwavunja mbavu wananchi baada ya kuomba kura akiwa amepiga magoti.
Akiwa mbele ya Dk. Magufuli, Profesa Tibaijuka aliomba asaidiwe kupata barabara ya lami.
“Ninaomba nikipiga magoti kwako mgombea urais, pamoja na maendeleo mengine kupatikana, naomba barabara ya lami kuelekea Hospitali ya Rubya…yaani imekuwa kero wakati mvua zinapoanza kunyesha,” alisema Profesa Tibaijuka huku akishangiliwa.
AOMBA KUTETEWA
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli, amewaomba Watanzania wamtetee kutokana na uamuzi atakaochukua dhidi ya viwanda vya umma visivyoendelezwa.
Alisema kutokana na uamuzi huo, watu wasiomtakia mema wageuza ajenda hiyo na kudai atawanyanyasa wafanyabiashara.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano aliofanya Jimbo la Bukoba Vijijini jana na kusema dhamira ya kuchukua viwanda visivyoendelezwa ipo palepale na hatorudi nyuma.
“Watanzia niteteeni kwa kunichagua kwa kura nyingi, niliposema tutachukua viwanda vilivyoshindwa kuendelezwa, kuna watu wanageuza maneno na kusema nitawaonea wauza maduka.
“Siwezi kufanya hivyo, wenye maduka wengi wao ni wanyonge ambao mimi ndiyo mtetezi wao wa kweli.
“Leo viwanda vyote walivyobinafsishiwa watu, wameshindwa kuviendeleza, vimegeuka maghala ya mbuzi… hapa Bukoba tulikuwa na kiwanda cha chai kimekufa, vijana wetu hawana ajira wanaishi maisha magumu.
“Najua ninasimama hapa nikizungumza mafisadi hawanipendi na ninawaomba wana Bukoba na Watanzania mniombee.
“Najua hata hapa Bukoba wapo, wamekuwa wakileta hela zao ili msinichague, hela zao kuleni na mnichague kwa wingi,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa.
MAUAJI
Dk. Magufuli alilaani mauaji ya watu kwa kukatwa makoromeo, huku akisema suala hilo ni lazima likome kwani haliendani na ubinadamu.
“Kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake, anatakiwa kulaani mauji ya aina hii. Leo mtu unatoka kupata lubisi unakutana na mtu anakukata koromeo, huu ni utamaduni gani ndugu zangu?” alihoji Dk. Magufuli.MTANZANIA
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / siasa /
slider
/ MGOMBEA URAIS KUMSHUGHULIKIA KIKAMILIVU WAZIRI ANAYESABABISHA MIGOGO YA WAFUGAJI NA WAKULIMA BAADA YA KUGAWA ARDHI KIHOLELA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment