BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UKAWA NI URAFIKI THABITI AU ULAFI WA MADARAKA ?.

 
Katika siku za karibuni, kumejitokeza sintofahamu katika baadhi ya majimbo kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushindwa kuachiana viti vya Ubunge na Udiwani.

Mtafaruku mkubwa zaidi upo katika kuachiana nafasi za udiwani katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kuwapo waraka wa ushirikiano wenye mwongozo na vigezo uliotiwa saini Agosti 13,2015.

Makubaliano haya yalitiwa saini na Dk. George Kahangwa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu NCCR-Mageuzi, John Mnyika Naibu Katibu Mkuu Chadema na Tozzy Matwanga katika mkuu NLD.

Pia yalitiwa saini na Naibu Katibu mkuu wa Cuf, Magdalena Sakaya. Viongozi hawa waliotia saini makubaliano haya ni watu wazito kiuongozi kwani ndio watendaji wakuu ama Naibu watendaji.

Kwa mujibu wa mkataba huu, moja ya kigezo kitakachotumika kupima ni chama gani kinastahili kusimamisha mgombea Udiwani katika kata husika ni matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Chini ya mkataba huu, kata iliyo chini ya chama mshirika wa Ukawa kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, basi chama hicho ndicho kitakuwa na haki ya kusimamisha mgombea.

Lakini, kwa kata iliyopo CCM, idadi ya kura ambazo vyama washirika wa Ukawa vilipata katika uchaguzi huo ndio itatumika kukipa chama washirika wa Ukawa fursa ya kusimamisha mgombea.

Kigezo kingine muhimu zaidi ni matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, kwamba chama kilichoongoza kupata wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji ndicho kitapewa kipaumbele.

Pamoja na vigezo hivyo vikuu vipo vigezo vya ziada kama mtandao wa chama kwa eneo husika, mila,desturi na utamaduni wa Jimbo au kata husika na uwepo wa mgombea nayekubalika na jamii.

Hali ikoje ?.
Jimbo la Vunjo kwa mfano ni moja ya majimbo mengi nchini ambayo vyama vinavyounda Ukawa vimesimamisha wagombea hivyo kata moja kuwa na wagombea wawili ama zaidi wanatokana na vyama vya Ukawa.

Katika jimbo hilo, zipo jumla ya kata 16 ambapo chama cha NCCR-Mageuzi kimesimamisha wagombea Udiwani kata zote na Chadema nayo imesimamisha wagombea. Vyama hivi ni Ukawa.

Wagombea Udiwani kwa tiketi ya Chadema, wanatoa hoja nyepesi sana kwamba “Ukawa wamekubaliana kugawana kata”, bila kueleza vigezo vya kuachiana kata vikoje au vinasemaje.

Hemed Msabaha ambaye ni kampeni meneja wa mgombea Ubunge Jimbo hilo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, James Mbatia anasema kwa vigezo vya makubaliano, chama chao kilistahili kata 13.

Kwa mujibu wa Msabahaha, kwa kutumia kigezo cha uchaguzi mkuu wa 2010, Chadema kilikuwa na Madiwani wawili hivyo kata zilizokuwa chini yao zilikuwa hazina ubishi kuwa zilistahili waachiwe.

“Ukiondoa hizo kata mbili, ina maana kata 14 zilizobaki zilistahili kugawanywa kwa vigezo vya uchaguzi mkuu wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana,”anasema Msabaha.

“Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa NCCR-Mageuzi tulifanya vizuri katika vitongoji na vijiji katika kata 10 dhidi ya kata mbili za Chadema. Kwa hiyo kata 14 zilikuwa hazina mgogoro,”alisema.

Msabaha alifafanua kuwa kwa kigezo hicho cha uchaguzi wa Serikali za mitaa 2014, NCCR-Mageuzi ilipewa kata 10 na Chadema kata mbili lakini kukawa na ubishani katika kata mbili.

Kata hizo ni Makuyuni na Kirua Vunjo Kusini na makubaliano yakawa ni kwamba vyama hivyo viwili vigawane kata moja moja ambapo NCCR-Mageuzi ichukue Makuyuni na Chadema Kirua Vunjo.

Moshi mjini nako, Chadema kimesimamisha wagombea udiwani katika kata zote 21.

huku NCCR-Mageuzi ikisimamisha wagombea kata za Kiusa na Korongoni na Cuf ikasimamisha kata ya Kaloleni.

Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro leo hii, NCCR-Mageuzi wamesimamisha mgombea Ubunge na Chadema nao wamesimamisha mgombea. Kwanini viongozi wa Ukawa wanafumbia macho hili?.

Viongozi wa Ukawa na wagombea wao warudi kwenye makubaliano waliyoafikiana Agosti 13, 2015 vinginevyo tutawaona ni watu wasioitakia mema nchi bali makubaliano yao yanasukumwa na ulafi wa madaraka.

Daniel Mjema ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoa Kilimanjaro. Anapatikana 0769600900
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: