WANANCHI WAMKATAA MGOMBEA URAIS WA UKAWA EDWARD LOWASSA, DK MAGUFULI NA CCM WAKUBALIKA KWA ASILIMIA 65.
Asilimia 62 ya wananchi wamesema wako karibu na CCM huku asilimia nyingine 65 wakisema watamchagua mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano, matokeo ya utafiti wa Twaweza yaeleza leo.
Akisoma matokeo ya utafiti huo uliotolewa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema, Chadema kimeendelea kushika nafasi ya pili kwa umaarufu na kuviacha mbali vyama vingine vya upinzani.
Katika utafiti huo uliofanyika Agosti mwaka huu, wananchi walipoulizwa moja kwa moja jina la mgombea watakayemchagua kuwa rais Oktoba 25, asilimia 65 walisema ni Dk. Magufuli, wakati asilimia 25 ikitaja jina la mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
Hata hivyo, walipoulizwa sababu za kuona wagombea hao wanafaa kushika wadhifa huo, asilimia 26 walisema Dk. Magufuli anafaa kuwa rais kwa kuwa ni mchapakazi huku asilimia 12 ya wananchi wakieleza kuwa Lowassa anaweza kuleta mabadiliko ambayo nchi inayahitaji kwa sasa.
ACT-Wazalendo na vyama vingine havikuhusishwa katika kipengele hiki kwa kuwa vilikuwa havijaamua mtu atakayesimamishwa katika nafasi ya urais.
Utafiti huo umeendelea kuonyesha; asilimia 60 ya wapigakura watachagua wabunge wa CCM na idadi kama hiyo hiyo itachagua madiwani wa chama hicho tawala.
Katika nyadhifa hizo, asilimia 26 ya walioshiriki katika utafiti huo wamesema watachagua wabunge wa Chadema, Cuf (3%) na NCCR-Mageuzi (1%).
Akiendelea kusoma matokeo ya utafiti huo, Eyakuze amesema asilimia 49 ya wananchi wanaamini kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni chama cha siasa kilichosajiliwa rasmi kitu ambacho si kweli.
Katika muktadha huo, asilimia 57 ya wananchi wanaamini kuwa jina “Ukawa” litakuwepo katika karatasi ya kupigia kura.CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment