JESHI LA POLISI LAFICHUA SABABU ZA KITAALAMU ZA KIFO CHA MCHUNGAJI CHRISTOPHER MTIKILA, ALIVUNJIKA MBAVU NANE KISHA DAMU KUVUJA NA KUINGIA KATIKA MFUMO WA KUPUMUA.
Kibaha/Dar. Polisi mkoani Pwani, imeweka bayana sababu za kitaalamu za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ikisema alivunjika mbavu nane upande wa kushoto, damu kuingia kwenye mfumo wa hewa na kushindwa kupumua.
Mchungaji Mtikila alifariki dunia juzi alfajiri baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Njombe kwenda Dar es Salaam, likiwa katika mwendo mkali, kuacha njia na kupinduka. Alirushwa nje kupitia kioo cha mbele kutokana na kutofunga mkanda.
Katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Msolwa, Chalinze mkoani Pwani, watu wengine wawili waliokuwa kwenye gari hilo dogo walijeruhiwa na dereva anashikiliwa na polisi akitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed alisema jana kuwa baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, madaktari katika hospitali Teule ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi walibaini kuwa sababu hizo ndizo zilizosababisha kifo chake.
Ilikuwa ajali ya pili
Pia imegundulika kuwa, kabla ya ajali hiyo kutokea, Mtikila na abiria wenzake ambao waliondoka Dar es Salaam Oktoba 2 jioni kwenda Njombe na kufika Oktoba 3 alfajiri kwa ajili ya kampeni za chama chake, wakiwa huko walipata ajali kwa kugonga magari mawili yaliyokuwa pia yamepata ajali na kusababisha uharibifu wa gari lao hilo.
“Kulingana na taarifa ya mkaguzi wa magari ya Oktoba 3, huko Njombe, walishauriwa watengeneze gari lao kwanza kabla ya kulitumia tena. Saa 3.30 usiku waliondoka Njombe kurudi Dar es Salaam na ilipofika saa 11.45 alfajiri Oktoba 4 ndipo wakapata ajali,” alisema Kamanda Mohamed.
Sababu za ajali
Alisema uchunguzi uliofanywa kwa kukagua tukio zima la ajali na kuwahoji majeruhi, umeonyesha kuwa ajali hizo zimesababishwa na mambo manne.
Kamanda Mohamed aliyataja mambo hayo kuwa ni ubovu wa gari kwa kuwa lilipopata ajali Oktoba 3, moja ya sehemu muhimu ziliyoharibika ni mfumo wa usukani, hivyo inawezekana halikupata matengenezo kikamilifu na hivyo kuchangia ajali hiyo ya pili.
Jingine ni Mtikila kutofunga mkanda wa usalama na hivyo kusababisha arushwe nje kupitia kioo cha mbele, uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu ya kuendesha gari mchana na usiku na kabla ya safari kurudi alikuwa akishughulikia matengenezo ya gari hivyo hakupata muda wa kupumzika.
Alisema pia kuwa mwendo kasi pia ni chanzo kingine cha ajali na kwamba dereva wa gari hilo, George Steven amekiri kuwa walikuwa mwendo kasi licha ya kuwapo alama zinazoelekeza mwendo na hivyo baada ya gari kuacha barabara lilikwenda umbali wa mita 105 kabla ya kupinduka.
Wataalamu wakusanyika
Kamanda Mohamed alisema: “Baada ya ajali, timu maalumu ilifika eneo la tukio kwa ajili ya ufuatiliaji ikiongozwa na Mkuu wa Utawala wa Trafiki Makao Makuu Dar es Salaam, Johansen Kahatano, mimi, mkuu wa upelelezi makosa ya jinai mkoani hapa na daktari wa maabara ya kisayansi inayohusu uchunguzi wa makosa ya jinai.
“Walishirikiana na wataalamu wa sayansi ya makosa ya jinai kutoka Makao Makuu ya Polisi wakafanya ukaguzi na uchunguzi wao ukabaini mambo hayo yalichangia ajali hiyo,” alisema Kamada Mohamed.
Mwili wa Mtikila tayari umekabidhiwa ndugu zake kwa taratibu za mazishi wakati dereva Steven akisubiri kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Baraza laahirisha
Kutokana na msiba huo, Baraza la Vyama vya Siasa limeahirisha vikao vyake ili kumuenzi Mtikila mpaka baada ya maziko yake. Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray alisema kifo hicho ni pigo kwa maendeleo ya demokrasia nchini.
Kikwete atuma salamu
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Mchungaji Mtikila. Katika salamu hizo Rais alisema: “Kifo hicho ni pigo kwa medani za siasa katika Tanzania na kimetunyang’anya mmoja wa viongozi hodari na wazalendo, aliyekuwa na msimamo thabiti na usioyumba katika kutetea mambo ambayo aliyaamini katika maisha yake yote.
“Ni jambo la kusikitisha pia kuwa tunampoteza Mchungaji Mtikila katika kipindi cha mchakato muhimu wa kisiasa nchini ambako mchango wake ulikuwa unahitajika sana. Hakika, tutamkosa mwenzetu katika uwanja wa siasa za nchi yetu.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment