"Ikulu ni ya Magufuli. Ninasubiri tu kuapishwa...hata wapinzani wangu wanajua kwamba wao wameshashindwa na vyombo vya habari siku ya kuapishwa viripoti hivyo kwamba mimi ndiye mshindi."
Dkt. Magufuli alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, mkoani Dodoma jana.
"Naenda Ikulu nikapambane na mafisadi wanaozuia hela zikae juu zisiwafikie Watanzania," alisema Dkt. Magufuli na kusisitiza kwamba anachukia rushwa na ufisadi kwani ndivyo vinavyokwamisha maendeleo ya Watanzania.
Alisema akiingia Ikulu atahakikisha anajenga kiwanda kikubwa kila mkoa ili kutengeneza ajira kwa vijana na kutokana na tabia ya kuuza bidhaa ghafi.
"Hili nitalisimamia kwa nguvu zangu zote na akili zangu na nitawapa fursa wawekezaji waweke pesa za kutosha nchini ili kutengeneza fursa za ajira na kuwapa watu maendeleo.
Kuhusu ardhi, alisema akiwa madarakani itakuwa marufuku mtu kuchukua ardhi ya mtu bila kumlipa fidia, kwani kufanya hivyo ni kukwamisha maendeleo ya Watanzania wa hali ya chini. Alisema yeye anaheshimu sheria na anapenda kusimamia sheria ili kuhakikisha Watanzania wanatendewa haki.
Aliongeza kuwa CDA wanachukua mashamba au viwanja vya watu hawalipwi fidia zao wanazostahili; hivyo katika Serikali yake ni marufuku kuchukua ardhi ya mtu bila kulipa fedha anayotaka.
"Tatizo kubwa ni kwamba halmashauri na mamlaka hiyo wote wanataka kipima viwanja; na kusababisha mgongano wa kimasilahi miongoni mwao," alisema Dkt. Magufuli. Alisema Serikali yake itakuwa ya viwanja na kupunguza vifaa vya ujenzi.
Kuahirishwa mkutano wa UKAWA
Wakati huo huo, Shirika la Huduma ya Kwanza Tanzania Ofisi ya Tanga, limesema viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walifanya uamuzi wa kuahirisha mkutano wao uliofanyika uwanja wa wazi wa Tangamano, mkoani Tanga kwa sababu zao na si kwa sababu ya msongamano kama ambavyo iliripotiwa kwenye vyombo vya habari.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo kwa vyombo vya habari na gazeti hili kupata nakala Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa;
" Hakuna watu walioumia katika mkutano huo na hakuna ripoti ya tukio hata moja la maafa kwenye hospitali yoyote au kwenye kituo cha afya Tanga kutokana na mkutano huo."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ilieleza kwamba viongozi wa UKAWA waliamua kuahirisha mkutano huo bila kuwahusisha wao wala jeshi la polisi, ambao ni wataalamu kwenye mambo yanayohusu usalama wa raia.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba pamoja na kutolewa tamko la kuahirisha mkutano, mgombea urais wa UKAWA (Edward Lowassa) alihutubia kwa muda mfupi na hakukutokea maafa, hivyo angeweza kuendelea kama angependa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Shirika hilo limewataka wanasiasa kuacha kutumia shughuli za kitaaluma kwa manufaa ya kisiasa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Shirika hilo limesisitiza kwamba katika kipindi cha uchaguzi litaendelea kusimamia usalama wao katika mikutano yote ya kampeni. "Wananchi waendelee kuhudhuria bila kuwa na woga kuhusiana na usalama wao,"ilisema taarifa hiyo.
Shirika hilo limesema lina wafanyakazi na vitendeakazi vya kutosha kuweza kumudu shughuli za aina yoyote.
Shirika hilo limesisitiza kuwa katika mkutano huo katika Uwanja wa wazi Tangamano, haukuwa na msongamano mkubwa kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Jaji Warioba
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, amesema tatizo kubwa la nchi hii ni ufisadi; hivyo mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, ana uwezo mkubwa wa kusimamia na kuongoza taifa kutokana na uadilifu wake.
Pia alisema Dkt, Magufuli ana uwezo mkubwa wa kuunganisha Watanzania na kwamba kitendo chake cha kuhubiri na kudumisha amani ni wazi kuwa ni mzalendo wa kweli katika nchi hii.
"Ndugu zangu wananchi, kama wengine hawajui, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo imefanikiwa kulinda amani na utulivu ndani ya miaka 54 ya uhuru wa nchi yetu, hivyo ni muhimu sana kuendelea kuhubiri amani katika nchi," alisema Jaji Warioba.
Aliwataka vijana kulinda amani na kuongeza kuwa waliopambana kuleta amani iliyopo ni vijana, huku akimtaja Mwalimu Julius Nyerere wakati akidai uhuru wa nchi.
Alisema kuwa kama kuna kiongozi yeyote hajui historia ya nchi hii basi huyo hafai kuwaongoza Watanzania, huku akidai zamani kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya ilikuwa shughuli kufika, lakini leo baadhi ya wanasisa wanadai katika kipindi cha miaka 54 hakuna kilichofanyika.
Mzee Malecela
Naye Makamu Mwenyekiti mstaafu na waziri mkuu mstaafu wa awamu ya pili John Malecela aliwataka Watanzania kumpigia kura Dkt. Magufuli kama kweli wanahitaji aende Ikulu. Alisema kuwa hawezi kwenda Ikulu kama hawajashikamana na kuhimizana kwenda kupiga kura itakapofika Oktoba 25, mwaka huu.MAJIRA
0 comments:
Post a Comment