LALA SALAMA !, DK MAGUFULI NA LOWASSA WACHUANA VIKALI: VYAMA VYA SIASA VINAVYOCHUANA KATIKA UCHAGUZI MKUU VYAWEKA MIKAKATI YA KUKUBALIKA ZAIDI KWA WANANCHI KABLA YA OKTOBA 25.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni mjini Mkuranga mkoani Pwani jana. Picha na Mpigapicha Wetu
Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku kumi na moja kupiga kura, vyama vya siasa vinavyochuana kwenye Uchaguzi Mkuu vimeweka mikakati mipya ya kukubalika kwa wananchi wengi zaidi.
Kampeni zilianza Agosti 23, ikiwa ni siku moja baada ya tarehe rasmi iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kumekuwa na mchuano mkali kwa wagombea urais, hasa kati ya Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR Mageuzi. Vyama vingine ni ACT-Wazalendo, Chama cha Ukombozi na Maendeleo (Chaumma), TLP na UPDP.
Mpango wa kumaliza kampeni kwa kishindo ilianza kwa CCM kutangaza mkakati wake unaojumuisha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, katibu mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na kutumia helkopta nne, wakati Ukawa imeamua kutoa elimu ya mpigakura.
Chama Cha Mapinduzi (CCM)
CCM imempangia Mkapa mikutano atakayohutubia kushawishi wananchi kumpigia kura Dk Magufuli na Kinana amepangiwa majimbo 64, huku makada wengine kama katibu mkuu wa zamani, Yusuf Makamba na mjumbe wa Kamati Kuu, Emmanuel Nchimbi wakipangiwa baadhi ya mikutano ili kuhakikisha CCM inaonekana sehemu nyingi kadri inavyowezekana.
“Tangu tuanze kampeni hadi sasa ushindi unajidhihirisha, hata hivyo katika kujihakikishia ushindi na kuongeza kiwango cha ushindi katika ngwe hii ya mwisho tumeanza kampeni za nguvu,” alisema msemaji wa CCM wa kampeni za uchaguzi, January Makamba.
“Katibu mkuu ameanza ziara ya kampeni katika majimbo 64, vilevile viongozi wengine wa CCM akiwamo Rais na mwenyekiti mstaafu, Benjamin Mkapa nao wataanza safari za kuzunguka nchi nzima.”
Makamba alisema CCM ina imani na imejipanga kushinda na kwamba wataanza kutumia chopa nne ili kuwafikia wapigakura katika maeneo yote, lakini Dk Magufuli hatatumia isipokuwa watakapolazimika.
Mkakati wa Ukawa
Ukawa, ambayo imekuwa ikisisitiza kuwa huu ni mwaka wa mabadiliko na kuwataka wananchi wajiandae kisaiokolojia, imeamua kujikita zaidi katika elimu ya mpigakura, ikiwa inahitaji kura nyingi kama ambavyo Lowassa amekuwa akihimiza kwenye kampeni zake.
“Katika hiki kipindi cha mwisho tunawaandaa wananchi kisaikolojia ili wajiandae kuwa washindi na kuwataka wasiwe na wasiwasi,” alisema kaimu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu.
“Tunazunguka kutoa elimu kuhusu suala la upigaji wa kura na namna ya kuzilinda kura zetu.”
Alisema kitu kinachowapa nguvu ni mipango yao ya ndani ambayo hawezi kuiweka wazi na kwamba katika mikutano yao lala salama, wameweka kipaumbele katika kuhamasisha suala la amani na utulivu.
“Mikakati ya ushindi ya ndani siwezi kuisema, lakini tunachojivunia ni mikakati hiyo kusukwa vizuri. Mwamko wa wananchi kuhudhuria mikutano yetu ni mkubwa, tumejipanga vizuri kwa sababu tunajua wananchi wana hamasa ya kupiga kura ya mabadiliko,” alisema
Kuhusu matumizi ya chopa, Mwalimu alisema ni desturi ya chama hicho kutumia usafiri huo kila wakati wa uchaguzi na kwamba hawezi kutaja idadi ya helkopta wanazotumia.
“Ni desturi yetu kutumia chopa kwa sababu jiografia ya Tanzania huwezi kusafiri kwa gari ukaweza kuwafikia wapigakura wote. Tutatumia chopa kwa lengo la kuwafikia Watanzania wote,” alisema.
Mbali na kauli hiyo, akiwa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, Lowassa alimuomba mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wa NCCR Mageuzi, James Mbatia waimgie kwenye msafara wake ili kuongeza nguvu.
Mbowe anagombea ubunge wa Jimbo la Hai wakati Mbatia anagombea Jimbo la Vunjo, lakini Lowassa aliwaeleza kuwa wawaombe wananchi wawaelewe.
Pia kujiunga kwa kada mkongwe katika siasa nchini, Kingunge Ngombare-Mwiru ni silaha nyingine ya lala salama ambayo Ukawa inaitumia kutimiza azma yake ya kukiweka madarakani chama cha upinzani kwa mara ya kwanza.
ACT Wazalendo
Hali ni tofauti kwa chama kipya cha ACT Wazalendo, ambacho kimeunda makundi mawili zaidi ili kushambulia majimbo yaliyobaki, kwa mujibu wa katibu wake, Samson Mwigamba.
Mwigamba alisema kuongezeka kwa makundi hayo kutafanya idadi ya makundi kufikia matatu, baada ya lile linaloongozwa na mgombea wa urais, Anna Mgwhira.
Alisema kundi jingine litaongozwa na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na la tatu litaongozwa na katibu huyo na watajigawa katika maeneo tofauti ya nchi ili kuhakikisha wanawafikia wananchi na kukiongezea kura chama chao.
“Mgombea wa urais ataendelea na ratiba yake kama kawaida. Ila sisi tutakuwa tunafuata ratiba za mikutano ya wagombea ubunge ili tuhakikishe wanapata kura za kutosha sambamba na mgombea urais,” alisema Mwigamba bila kutaja maeneo hayo.
Pia, alisema chama chake hakina mpango wa kutumia helkopta badala yake wataendelea kutumia usafiri wa barabara ili kujua zaidi matatizo na kero zinazowakabili Watanzania.
UPDP ni kata kwa kata
Chama cha UPDP kitasaka kura kutoka kata moja hadi nyingine.
Mgombea urais wa chama hicho, Fahmi Dovutwa alisema mfumo huo utakiwezesha chama hicho kuwafikia wapigakura wengi.
“Mbinu yetu mpya ni kupita kata kwa kata ambako hakuna wagombea urais wanaopita huko. Tumeshamaliza kampeni kanda ya kusini hasa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Tunaendelea maeneo mengine kwa sababu wapigakura hawapatikani majimboni, wilayani au mikoani ila ni kwenye kata,” alisema.
“Tunachokifanya ni kuhakikisha tunauza sera kulingana na maeneo husika waliko wapigakura.”
Kampeni za kawaida TLP
Chama cha TLP, ambacho wiki iliyopita mwenyekiti wake, Augustino Mrema alimpigia debe mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli kwa madai kuwa ni mchapakazi, badala ya mgombea wake, Macmillan Lyimo, kitaendelea na kampeni za kawaida.
“Mgombea wetu wa urais ni mtu mzuri, muadilifu na anajituma. Kwenye kipindi hiki cha lala salama hatutatumia chopa lakini tunayo mikakati ya ushindi ili kuwafikia wapigakura,” alisema Mrema.
Wadau wataka nguvu zaidi
Pamoja na kubadilisha mikakati hiyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kunahitajika nguvu zaidi kwa vyama ambavyo vina nia ya kuingia Ikulu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa, Profesa Kitila Mkumbo alisema:
“Kama kweli chama kinataka kushika dola katika kipindi hiki cha lala salama lazima kukubali kuongeza nguvu ili kuwafikia wapigakura wote vinginevyo itakuwa vigumu kushinda.
“Wapigakura ambao tayari wana vyama vyao huwa hawawezi kubadilika, lakini kwa wale wenye tabia ya kuamua nani watampigia kura siku za lala salama na wenye tabia za kubadilika ni lazima wawaone wagombea husika.”
Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi, Afya na Tiba, (Muhas), Dk Avemaria Semakafu anashauri vyama kuhakikisha mbinu hizo mpya haziwaathiri wapigakura.
“Kila chama kijikite kukemea rushwa badala ya wao kuwa chanzo cha matumizi ya rushwa katika kuongeza wapigakura wake. Tunachotaka ni kuona uchaguzi unakuwa huru na wa haki ambao utamfanya kila raia kumchagua kiongozi kwa kutazama sera za wagombea,” alisema.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment