Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwamuru Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima awasilishe Mahakamani hapo vyeti vinavyoonesha kuwa ni mgonjwa.
Amri hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha baada ya Gwajima kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi inayomkabili.
Gwajima anakabiliwa na kesi ya kutumia lugha chafu dhidi ya Akofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinal Pengo.
Kesi hiyo ambayo tayari imeshaanza kusikilizwa ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo ambapo upande wa mashtaka ulitarajiwa kuwasilisha kielelezo cha ushahidi ambacho ni mkanda wa video unaodaiwa kumwonesha Gwajima akitoa lugha hiyo chafu dhidi ya Kardinal Pengo.
Hata hivyo Gwajima hakutokea mahakamani na badala yake, Wakili wake Peter Kibatala aliieleza mahakama kuwa mteja wake hakuweza kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa. Hata hivyo haikuweza kubainishwa kuwa Gwajima anaumwa nini.
Wakili wa Serikali Lilian Itemba aliiomba mahakama iagize mshtakiwa huyo awalishe mahakamani vyeti vinavyothibitisha kuwa anaumwa.
Hakimu Mkeha alikubaliana na ombi hilo la upande wa Serikali na kuamuru mshtakiwa huyo awasilishe mahakamani hapo vyeti hivyo, siku ya tarehe ya kuendelea kwa usikilizwaji wa kesi hiyo.Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 4, 2015.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment