Dar es Salaam. Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) limesema kuwa mgao wa umeme unaoendelea nchini umesababishwa na kushuka kwa uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya maji kwa asilimia 81.3.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema leo jijini dar es Salaam kuwa uwezo wa juu wa mitambo yote ya kuzalisha umeme wa maji ni megawati 561, lakini kwa sasa uzalishaji wote wa umeme wa maji ni megawati 105 ambazo ni sawa na asilimia 18.7.
Kuhusu umeme wa gesi, Tanesco walisema kuwa uwezo wa kuzalisha umeme kupitia Kampuni ya Pan Africa ulishuka kutoka megawati 340 hadi kufikia megawati 260. Shirika hilo limesema kuwa Pan Africa wanaendelea kuviboresha visima vyake ili kuhakikisha gesi zaidi inapatikana.
“Mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi ya bomba jipya iliyokwisha washwa ni ya megawati 190 na leo tunatarajia kuongeza mwingine wa megawati 35. Mwezi Septemba tuliwasha mtambo mwingine wa megawati 20 ya gesi ya bomba la Songosongo na kufikisha umeme ulioongezeka kufikia megawati 110,” walisema Tanesco.
Shirika hilo la umeme limesema kuwa mitambo mingine ya Symbion (Megawati 20), Ubungo II (Megawati 35), Songas (Megawati 20) na Kinyerezi (Megawati 70)inatarajiwa kuwashwa ndani ya wiki moja hadi mbili tangu sasa ili kukabiliana na tatizo la mgao.
Alisema uwezo wa uzalishaji umeme kwa mitambo ya mafuta ni megawati 230, lakini kwa sasa inazalisha megawati 190 tu.
0 comments:
Post a Comment