BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MGOMBEA UBUNGE WA CHADEMA NUSURA ALIPULIWE NA MILIPUKO NDANI YA GARI.


Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Musoma Mjini, Vincent Nyerere, amenusurika kulipuliwa kwa milipuko ndani ya gari lake.

Milipuko hiyo iliyotajwa kuwa ni aina ya ‘explogel 7M V6 watergel explosive’ ilikutwa ndani ya gari lake.

Polisi mkoani Mara tayari linawashikilia watu wawili, Goodlucky Msuya (42) na Salum Blen (49), kwa tuhuma za kuhusika na milipuko hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philip Kalangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Oktoba 17, mwaka huu, saa 11:00 jioni eneo la Nyabisare kata ya Bweri wakati mgombea huyo akiendelea kufanya mkutano wa kampeni eneo hilo.

“Milipuko hiyo ilikutwa ndani ya gari namba T720 ANP aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya Vincent Nyerere, linaloendeshwa na Godluck Msuya,” alifafanua Kamanda Kalangi.

Alisema kabla ya watuhumiwa hao hawajakamatwa, mlinzi wa Vincent, alikwenda jukwaani na kumtaarifu kuhusu gari lake kuwapo na boksi dogo linalodhaniwa kuwa na milipuko ambapo naye (Vincent), alimtaka alichukue na kulipeleka jukwaani.

“Vincent aliwatangazia wananchi kwamba kuna watu wanataka kumuua na wamemtegea bomu ndani ya gari lake,” alisema Kamanda Kalangi.

Alisema baada ya Vincent kuzungumza na wananchi hao, walivirudisha vitu hivyo ndani ya gari na kutoa taarifa kwa polisi waliokuwapo eneo hilo la mkutano.

Kamanda Kalangi aliongeza kuwa polisi walikwenda kukagua gari la mgombea huyo na kutoa taarifa kwa viongozi wao wa juu ambao waliwaagiza gari hilo lipelekwe kituoni pamoja na vielelezo vilivyokuwapo ndani yake.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi wa awali, walithibitisha ilikuwa ni milipuko.

Hata hivyo, Kamanda Kalangi alisema milipuko hiyo ilikuwa haijafikia wakati wa kuleta madhara.

MASHA MBARONI TENA
Wakati huo huo, kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lawrence Masha, ameangukia tena mikononi mwa Jeshi la Polisi mkoani Katavi, kwa madai ya kuingia bila kibali katika eneo la makambi ya wakimbizi Kasumba na kufanya kampeni.

Masha ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alikamatwa jana pamoja na makada wengine sita wa Chadema.

Kamanda wa Polisi mkoani Katavi, Dhahiri Kidavashari, alilieleza Nipashe kuwa watuhumiwa hao walikamatwa jana saa 4:00 asubuhi eneo la Kanogo katika kambi hiyo.

Kamanda Kidavashari alisema Masha pamoja na watu wengine sita, akiwamo mgombea ubunge wa Jimbo la Nsimbo kupitia Chadema, Gernald Kitabu, waliingia kwenye makambi hayo bila kibali.

Alisema kosa la pili, ni kwamba makada hao hawakuwa na ratiba ya kufanya mikutano katika eneo hilo la kambi.

“Masha na wenzake, waliingia kwenye kambi bila kibali na jambo hili ni kinyume cha sheria pia wamefanya kampeni kwenye kambi wakati hawana kibali cha kuingia wala kufanya mkutano na watu,” alisema Kamanda Kidavashari.

Alisema Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1998 kifungu cha 20 kipengele cha kwanza kwa kosa la jinai la kuingia kwenye kambi bila kibali na pia hakuwa na ratiba ya mkutano.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alithibitisha kukamatwa kwa Masha na kusema kuwa hizo ni njama za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema Masha anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuingia kwenye kambi ya wakimbizi, lakini sehemu hizo alizofanya mkutano ndizo ambazo viongozi wa CCM walitangualia kufanya mkutano.

“Hii ni hofu ya uchaguzi, wanasema wamemkamata kwenye maeneo yasiyo rasmi wakati eneo hilo hilo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitangulia kufanya mkutano hapo,” alisema Makene.

Alisema Chadema inafanya juhudi za kumtoa Polisi ili kuendelea na mikakati yake ya kampeni za ushindi.

Agosti 24, mwaka huu, Masha ambaye pia ni wakili, alikamatwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni jijini Dar es Salaam, alipokwenda kuwawekea dhamana vijana waliokamatwa kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria.

Inadaiwa kuwa Masha alitoa lugha ya matusi kwa askari aliowakuta katika kituo hicho, hivyo naye akakamatwa na kuwekwa mahabusu kabla ya kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako alinyimwa dhamana na kupelekwa katika Gereza la Segerea.CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: