MGOMBEA urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amewataka wananchi hasa wanawake, vijana na wazee kutotishika na maneno ya kuwazuia wasiende kumpigia kura na kuwataka waende vituoni kifua mbele, kumchagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Aidha, amesema kote alikopitia kuanzia Monduli hadi Pemba, amejiridhisha kwamba ushindi kwake na chama chake, utakuwa wa tsunami katika uchaguzi mkuu wa Jumapili wiki hii. Dk Magufuli alisema hayo wakati akiwahutubia wananchi wa Nkome wilayani Geita mkoani Geita katika mkutano wa kampeni, uliofanyika jana Ihumilo.
“Kuna watu wanapita na kuwatisha hasa wanawake kwamba wasiende kupiga kura kunichagua… nendeni kifua mbele, wanawake, vijana na wazee, nendeni kifua mbele mkamchague Magufuli, msiogope vitisho vyao, hakuna wa kuwadhulumu,” alisema Dk Magufuli na kushangiliwa na maelfu ya wananchi wa Nkome.
Aliendelea kuwaeleza, “Nimepita kote, Monduli, Hanang, Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar, Pemba, Kagera, Katavi, Dar es Salaam, Mbeya… nimezunguka Tanzania, nimejiridhisha kwamba ushindi wangu utakuwa ni wa tsunami na wale wataisoma namba. Ninajua hawa (wapinzani) wananisindikiza, Rais ni John Pombe Magufuli.”
Aidha, pamoja na kurejea kupambana na wavuvi haramu ambao alisema ni wachache, lakini pia mgombea huyo alisema atapunguza kodi na ushuru katika sekta ya uvuvi ili kuboresha na kuinua mapato ya wavuvi.
“Sekta ya uvuvi inatoa ajira milioni 6 nchini, tutaimarisha sekta ya uvuvi kwani wakazi wengi wa Kanda ya Ziwa wanategemea samaki. Tutatoa mikopo na kutoa zana za uvuvi kwa wavuvi wote ili kuleta mabadiliko katika sekta hiyo,” alisema Dk Magufuli, ambaye aliahidi kuwalinda Watanzania wenye ulemavu wa ngozi (albino).
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia dhana potofu, eti kwamba ukienda na kiungo cha albino ziwani unapata samaki wengi. Huo ni ushetani ingekuwa hivyo basi albino wangekuwa wakienda ziwani wanafuatwa tu na samaki,” alisema.
Alisema pamoja na sifa nyingi ilizonazo Tanzania, lakini jina lake limekuwa likichafuka inapofikia suala la mauaji ya albino kutokana na kuonekana kuwa watu hao wenye ulemavu wa ngozi, usalama wao ni mdogo na kwamba wakati umefika wa kuithibitishia dunia usalama wao.
“Kwa bahati mbaya suala hili limeenea sana huku Kanda ya Ziwa na kwa vile nipo huku naomba nitumie nafasi hii kukemea kwa nguvu zote. “Samaki tunawamaliza sisi wenyewe kwa kuvua kwa sumu.
Watu wanakwenda kumwaga thiodani ziwani halafu samaki na mayai wote wanakufa, lakini baadaye wanajidanganya kwamba wakienda na kiungo cha albino ndio samaki watakapatikana kwa wingi.
Ni lazima tumwogope Mungu ndugu zangu,” alisema Dk Magufuli ambaye pia aliahidi kuwalinda watu wenye ulemavu mbalimbali. Aidha, Dk Magufuli alisema tofauti na wagombea wengine wanaoahidi kutoa kila kitu bure kwa wananchi, serikali yake itazingatia dhana ya Mtaji wa Masikini ni Nguvu Zake.
Alisema katika uongozi wake, akichaguliwa kuwa Rais atakachofanya ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kuchochea uzalishaji, ikiwemo barabara na umeme, lakini akasema viongozi na wananchi watalazimika kufanya kazi usiku na mchana na si kuzembea.
Kaulimbiu ya Mtaji wa Masikini ni Nguvu Zake ilipata umaarufu mkubwa wakati Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alipokuwa akijinadi ili kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995 na ilichochea kwa kiwango kikubwa uchapakazi na uwajibikaji.
Mgombea huyo aliyasema hayo alipofanya mikutano ya hadhara katika miji ya Nyahunge wilayani Sengerema na Nkome wilayani Geita, akiwa katika ziara za kampeni kuomba kuchaguliwa kushika wadhifa wa urais.
Alisema pamoja na kwamba anaomba kura kutoka kwa wananchi, lakini hawezi kutoa ahadi za uongo kwa Watanzania na badala yake atasema ukweli ili awe kiongozi wa kuaminika. “Hakuna cha bure, tutafanya kazi wote kwa pamoja mimi, mawaziri wangu na nyie wananchi.
Mtaji wa Masikini ni Nguvu Zake Mwenyewe. Hata vitabu vya dini vinasema Asiyefanya Kazi na Asile. Nitajenga barabara, nitaleta umeme, nitatoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, lakini wajibu wote itakuwa ni Kazi Tu,” alijigamba.
Akizungumza na wananchi wa Nyahunge katika Jimbo la Buchosa, Dk Magufuli alisema wakati wa uongozi wake, kipaumbele kikubwa kitakuwa ni katika kuweka mazingira ya kuwawezesha Watanzania kunufaika na jasho litakalowatoka kutokana na kuchapa kazi badala ya kujutia kama ilivyo sasa.
“Nimesikia wapo wagombea wanasema kila kitu watawapa bure. Wanasema eti wanachukizwa na umasikini, hiki ni kiinimacho kwa wananchi. Nawaomba wananchi msije mkauziwa mbuzi kwenye gunia. “Huu si wakati wa kukubali maneno ya uongo kama hayo. Tumecheleweshwa sana kwa maneno kama hayo.
Watanzania tusifanye makosa mwaka huu. “Tumeibiwa sana fedha zetu na rasilimali zetu kwa maneno matamu matamu kama hayo. Hawa watu wanachukizwa na umasikini wa familia zao na si wa wananchi maana walikuwa viongozi wa juu na hawakufanya kitu, kwa nini wasingeanza kumaliza umasikini huko watokako?
Nipeni kura mimi tuijenge Tanzania ya mfano wa kuigwa,” aliongeza Dk Magufuli. Tofauti na mikutano iliyotangulia, katika mkutano wa jana mgombea huyo wa CCM aliwashukia wavuvi wanaovua kwa kutumia njia haramu, akisema ingawa anahitaji kura zao, lakini atawashughulikia ipasavyo kwa vile vitendo vyao vimesababisha kushuka kwa uzalishaji wa samaki.
“Sitakubali wavuvi kuvua kwa sumu. Ni kweli kura za wavuvi nazitaka lakini hili nitapambana nalo kwa nguvu zangu zote.Hivi leo unavua kwa sumu ili kesho ukavue wapi? Ukimuua samaki kwa sumu unampoteza yeye na mayai yake na hivyo lazima samaki watapungua ziwani,” alieleza.
Alisema kwa kawaida samaki huwa na mayai kati ya milioni moja na milioni moja na nusu na hivyo wanapovuliwa kwa sumu, mayai hayo hupotea. Alisema hatua hiyo imeviathiri viwanda vya samaki mkoani Mwanza, ambavyo sasa wafanyakazi wanaingia kwa zamu moja wakati miaka ya nyuma walikuwa wakiingia kwa zamu tatu.
Alisema ili wananchi wakulima, wafugaji na wavuvi wafaidike na nguvu watakazozitumia katika uzalishaji mali wakati wa uongozi wake, atahakikisha kunakuwepo na soko la uhakika na bei ya juu kwa bidhaa zote watakazozalisha huku akisema viwanda ni njia pekee ya kuongeza thamani ya bidhaa.
“Nasisitiza nitajenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ili kuinua uchumi na kukuza ajira kwa haraka. Tukiwa na viwanda vya maziwa, viwanda vya nyama, viwanda vya ngozi, viwanda vya nguo, viwanda vya viatu na vinginevyo, pamba itakuwa na soko na itapanda bei, samaki watakuwa na soko na watapanda bei, na ng’ombe na mbuzi wetu vile vile,” alisema.
Dk Magufuli aliyesafiri kwa barabara katika barabara ya Kamanga - Sengerema - Nyahunge - Nzera hadi Nkome ili kujionea adha wanayokumbana nayo wananchi kutokana na ubovu wake, aliahidi kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami akiingia Ikulu kutokana na kuanza kwa maandalizi ya awali.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment