Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amefichua kuwa vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi na vigogo wa serikali ndiyo sababu ya kuchukiwa kwa serikali ya chama tawala.
Kutokana na hali hiyo, amewaomba wananchi wampigie kura nyingi za ndiyo ifikapo siku ya uchaguzi, Oktoba 25, mwaka huu ili awachukulie hatua na kukomesha hali hiyo.
Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni mjini Hanang, mkoa wa Manyara jana, Dk. Magufuli alifafanua kuwa yeye ni tingatinga na Watanzania wakimpigia kura nyingi na kumuingiza Ikulu atawaonyesha namna atakavyosafisha mafisadi serikalini na mwishowe kuwezesha maisha bora kwa kila mmoja.
Dk. Magufuli alisisitiza kuwa akiingia Ikulu, kamwe hatakuwa na msamaha dhidi ya mafisadi na wala rushwa kwani mara zote wamekuwa chanzo cha kukwamisha huduma za jamii zinazotolewa na serikali na kusababisha wananchi waichukie serikali yao.
Alirudia kauli yake anayoitoa karibu katika kila mkutano kuwa ataanzisha mahakama ya mafisadi ili kuhakikisha analinda rasilimali za umma ambazo zimekuwa zikiibwa na watu wachache.
Alisema anatambua kuwa hivi sasa Watanzania wamechoshwa na maisha duni, hivyo wanahitaji kuwa na rais kama yeye ambaye atasimamia mabadiliko ya kweli ili kila Mtanzania afaidi maisha bora .
“Niombeeni ili nikiingia Ikulu nisiwe na kiburi... nataka niwatumikie Watanzania wote bila kujali vyama vyenu, maana mmeteseka sana na shida zilizosababishwa na mafisadi. Vitu vimepanda bei kwa sababu ya ufisadi. Nataka kukomesha yote hayo,” alisema.
Aliongeza kuwa anatambua mikakati ya mafisadi ambao wamejipanga kutoa rushwa ili kuwarubuni wananchi wawachague kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Fedha chukueni, lakini kura ni kwa Dk. Magufuli tu. Zile fedha watakazogawa ni zenu. Walizichukua kwa wizi walipokuwa madarakani, zichukueni, lakini tarehe 25 wataisoma namba,” alisema.
MAPOKEZI MAKUBWA
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaodai kuwa serikali ya CCM haijafanya lolote kwa muda wote tangu Uhuru.
Alisema miongoni mwa wanaoikejeli serikali walikuwa serikalini muda mrefu, lakini walishindwa kusukuma maendeleo na wanazunguka kuichafua serikali, baada ya kuangushwa kwenye chaguzi ndani ya CCM.
Akizungumzia mapokezi aliyopata, Dk. Magufuli alisema tofauti na maneno yaliyokuwa yakisambazwa kwamba hatapata mapokezi mazuri mkoani Manyara, mamia ya watu wamempokea na kumuahidi kumpa ushindi wa kishindo tofauti na yale yaliyokuwa yakisemwa hapo kabla.
“Pale Endasak ambako ndiko nyumbani kwa kiongozi mmoja aliyehamia Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), watu wengi walinisubiri kwa wingi barabarani. Nimezungumza nao na wameniahidi ushindi mkubwa,” alisema Dk. Magufuli bila kumtaja Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye Endasak ndipo nyumbani kwake.
Sumaye alihama CCM na hivi sasa yuko na timu ya kampeni ya Ukawa iliyomsimamisha waziri mkuu mwingine wa zamani, Edward Lowassa, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vyama vinavyounda Ukawa ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Katika hatua nyingine, mgombea ubunge wa Jimbo la Hanang (CCM), Dk. Mary Nagu, alimshukia Sumaye kwa kudai kwamba licha ya kuwa mbunge kwa miaka 20 na pia kutumikia nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka 10, bado alishindwa kuleta maendeleo yakiwamo ya kujenga barabara za lami.
Sumaye alimuachia Nagu jimbo hilo, baada ya kustaafu ubunge mwaka 2005 na kuomba uteuzi wa CCM kugombea urais, lakini alishindwa.CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment