BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MOTO NAMNA UNAVYOTEKETEZA SAFU YA MILAMA YA ULUGURU MOROGORO


Milima ya Uluguru yenye urefu wa mita 2,630 iko Mkoa wa Morogoro.Ndani ya milima hiyo, kuna Mlima wa Kimhandu wenye urefu wa mita 2,646 juu ya usawa wa bahari.Picha Juma Mtanda.

By Lilian Lucas, Mwananchi

Morogoro. Moto umeendelea kuiteketeza Milima ya Uluguru kwa zaidi ya siku tano sasa licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na wahifadhi za kuuzima kushindikana, huku wananchi wanaoishi na kufanya shughuli za kibinadamu katika milima hiyo wakiendelea kuchoma moto.

Wahifadhi wa milima hiyo kutoka Taasisi ya Uluguru Nature Reserve iliyo chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), wameendelea kupambana na kudhibiti uchomaji moto huo lakini juhudi zao zinaelekea kukwama kutokana na jiografia ya milima hiyo yenye miinuko mikali na mabonde pamoja na miamba mikubwa ya mawe.

Moto huo mkubwa ulioonekana katika eneo dogo tangu Oktoba 5, umeendelea kusambaa kwa kasi katika maeneo mengi ya milima hiyo, hali inayotishia uhaba zaidi wa maji kwa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani kutokana na milima hiyo kuwa chanzo cha maji kwa mikoa hiyo.

Mhifadhi wa Uluguru Nature Reserve, Karani Sekiete akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake, alisema kwa takriban miaka mitatu sasa, milima hiyo haijapata athari ya moto.

Sekiete alisema katika kipindi hicho chote, elimu imekuwa ikitolewa na wadau mbalimbali wa mazingira wakiwamo wakala huo, kwa wananchi wanaoishi jirani na milima hiyo.

“Tunashangaa kuona tabia hii inataka kuibuka tena,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuzidi kusambaa kwa moto huo kwa kasi kunatokana na kukauka kwa majani na upepo mkali unaovuma.

Alisema hali hiyo inawapa wakati mgumu wazimaji ambao wakati mwingine hushindwa kuyafikia maeneo yanayoendelea kuteketea.

Mhifadhi huyo alisema pamoja na kutowakamata watuhumiwa walioanzisha uchomaji wa moto hao, walibaini viashiria vilivyoonyesha chanzo,ikiwamo mashimo yaliyozungukwa na moto yanayoashiria ni uwindaji wa wanyama wadogo ambao huwindwa kwa kutumia moshi, jembe na shimo linaloashiria uchimbaji wa madini katika milima hiyo.

Alisema kwa jinsi hali ilivyo sasa, kitu pekee kitakachosaidia kuzimwa kwa moto huo ni mvua kama itanyesha.

“Nawaomba wananchi watambue kuwa jukumu la kulinda, kutunza na kuzuia hatari yoyote katika maeneo hayo ni la kila mtu.

Mwananchi lilifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na kumkuta Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Alfred Shayo ambaye alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwa sasa hadi moto huo utakapozimwa. “Tukifanikiwa kuuzima, nitakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kulizungumzia hili,” alisema Shayo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: