Rais Jakaya Kikwete akitoa hotuba yake ya mwisho katika kikao cha 70 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika ukumbi wa makao makuu ya Umoja huo jijini New York nchini Marekani jana. ( Picha na Freddy Maro).
RAIS Jakaya Kikwete ameombwa na amekubali kujiunga na kundi la watu mashuhuri duniani wakiwemo viongozi wa Afrika, matajiri wa Marekani na watu wengine mashuhuri katika kutafuta majawabu ya kufuta ugonjwa wa malaria duniani kwa kuanzia na Bara la Afrika.
Ombi kwa Rais Kikwete kujiunga na kundi hilo ambalo litaongozwa na tajiri mkubwa zaidi duniani, Bill Gates, liliwasilishwa kwa mara ya kwanza kwake wiki iliyopita na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Malaria, Ray Chambers, tajiri mwingine wa Marekani.
Ombi hilo liliwasilishwa kwake katika mkutano na Chambers kwenye Hoteli ya JW Marriot, Essex House, mjini New York, Marekani, ambako Rais Kikwete alikuwa amefikia wakati wa safari yake ya shughuli nyingi katika Marekani na akalikubali ombi hilo.
Katika mkutano wa kwanza wa kukutanisha wadau wa wazo hilo duniani kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa Jumatatu wiki hii mjini hapa, ilielezwa kuwa baada ya jitihada za kupunguza kwa kiwango kikubwa cha malaria duniani, na hasa katika Bara la Afrika kufanikiwa, sasa jitihada zinaelekezwa katika kufuta kabisa ugonjwa huo katika Bara hilo.
Miongoni mwa watu waliohudhuria chakula cha usiku ni Rais Kikwete, Gates na Chambers, Rais wa Liberia Mama Ellen Johnson Sirleaf, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemarian Desalegn na Katibu Mtendaji wa Umoja wa Viongozi wa Afrika wa Kupambana na Malaria, Mama Joy Phumaphi.
Waziri Mkuu Desalegn ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Viongozi wa Afrika Katika Kupambana na Malaria (Alma) na Mama Sirleaf ndiye mmoja wa makamu mwenyekiti wakati Rais Kikwete akiwa mwenyekiti.
Miaka 10 iliyopita, Rais Kikwete na Chambers walijadiliana na kukubaliana kuanzisha Alma na walikuwa viongozi hao wawili ambao walibuni wazo la kusambaza mamilioni kwa mamilioni ya vyandarua vya kupambana na malaria katika Afrika.
Katika Tanzania, kila familia ilipewa vyandarua vya kupambana na malaria kwa mujibu wa ukubwa wa familia. Chambers aliongoza mapambano ya kupunguza malaria katika Afrika ambapo vifo vyake vimepungua kwa asilimia 70 katika miaka 10 iliyopita, lakini chini ya mpango wa sasa Gates ataongoza mpango wa kufuta kabisa malaria duniani kwa kuanzia na Bara la Afrika.
Rais Kikwete aliondoka Marekani usiku wa Jumanne, kurejea nyumbani baada ya ziara ambayo ilishirikisha shughuli zake kama Mwenyekiti wa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani kupendekeza jinsi dunia inaweza kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana ma magonjwa ya milipuko kufuatia majanga ya ugonjwa wa ebola.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment