Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Abdallah Safari akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) leo vinatarajia kuwasilisha malalamiko yake kwa Umoja wa Mataifa (UN) Jumuia ya Madola na Mahakama ya Kimataifa ya The Hague kutokana na kile kinachodaiwa kuanza kujitokeza kwa viashiria vya kutaka kuvuruga uchaguzi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Makamu Mwenyekiti CHADEMA (Bara) Prof.Abdalah Safari, alisema wameamua kupeleka malalamiko hayo katika jumuiya na kimataifa na mahakama hiyo ya kimataifa kwa ajili ya kuwadhibiti walioanza kuonesha viashiria vya vurugu, mapema.
Alisema kauli ya Rais Kikwete kuhusu idadi ya wapiga kura na kutumia nguvu kuwaondoa watu watakaokaa mita 200 baada ya kupiga kura si ya kawaida na kwamba inaonesha wazi kuwa CCM ipo katika hali mbaya.
Alisema vyama vya siasa vilimtaka Rais Kikwete kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi na Tume Huru ya Uchaguzi baada ya Rasimu ya Jaji Warioba kukwama, lakini alikataa na badala yake alikubali kupitisha Sheria ya Gesi na Mafuta.
"Kesho (leo) tunaandika barua kwenda Umoja wa Mataifa (UN),Jumuia ya Madola na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC)" alisema na kuongeza watamshitaki Kikwete huko kwa vile anaingilia uhuru wa Tume, pamoja na mambo mengine.
Mwanasheria wa CHADEMA, John Malya, alisema suala la wananchi kukaa mita 200 baada ya kupiga kura lipo kisheria hivyo Rais Kikwete akitumia nguvu basi ICC itamuita, kwani hata Jumuia za Kimataifa zinafuatilia uchaguzi huu.
"Kwa mujibu wa Katiba,Sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 kifungu cha 104 mtu anaruhusiwa kuendelea na shughuli zake kuanzia mita 199, lakini sisi tunasema wakae mita 200 kulinda kura zao,"alisema Mallya.
Alisema suala hilo lipo kikatiba na kisheria na ni haki yao kwani vituo vingi vipo karibu na makazi ya watu sasa nao waondoke kwenye nyumba zao? Alisema wanaitaka NEC kutoa majibu mapema.
Daftari la BVR
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA, Reginald Munisi, alisema juzi NEC waliwapatia daftari hilo lakini wamegundua makosa 17 yakiwemo kuandikishwa kwa Watanzania wenye asili ya kiasia, hotel, pikipiki na maghala.
Alisema NEC iliamua kuchelewesha kuwapatia Daftari hilo mapema na kulihakiki kutokana na NEC kujua kila kitu.
"Serikali ya CCM inafanya utani na uchaguzi huu kwani katika kituo cha NEC imeandikisha Wachina, kuna majina ya maghala, mahoteli na pikipiki na mengine hayaeleweki yakiwa yametokea zaidi ya mara mbili na hicho ni kituo kimoja tu cha Azimio namba moja kilicho mjini mkoani Dodoma sasa bado vituo vingine zaidi ya 65,000...sasa tujiulize hali ikoje?"Alisema.
Alisema ikiwa NEC haitafanya hivyo basi watatoa taarifa za hatua gani za kuchukua kwa kuwa wanahitaji pia kukagua mfumo wa kujumlishia matokeo ili waujue na kijiridhisha.
"NEC wakikataa tusikague mfumo huo na kuruhusu tuweke mawakala wetu wa TEHAMA katika vituo vya kupokelea matokeo na kujumlisha matokeo basi sisi tutaususia mfumo huo na tutataka zihesabiwe moja moja,"alisema
0 comments:
Post a Comment