Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kumaliza salama utumishi wake serikalini kwenye ngazi za juu ambao umedumu kwa takriban miaka 15.
Akizungumza na waumini wa Kanisa Katoliki wakati wa Ibada ya Jumapili katika Parokia ya Mt. Anna iliyoko Hananasifu, Kinondoni jana, Pinda alisema anamshukuru Mungu kwa kumaliza salama nafasi aliyopewa ya kulitumikia taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na miezi tisa na katika ngazi ya uwaziri miaka miwili na nusu na miaka mitano akiwa Naibu Waziri.
“Ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kumaliza salama uongozi wangu serikalini. Ninamaliza uongozi wangu kwa amani na furaha. Katika ibada hii ya shukrani nimemuomba Mungu anisamehe kwa matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi… yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila mimi kujua,” alisema na kuongeza:
“Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu nisipomshukuru Mungu kwa uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu nikiwa Naibu Waziri hadi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.”
“Wito wangu kwa Watanzania wote ni kwamba msiache kumtaguliza Mungu maishani kwa sababu yeye ndiye mtoaji wa yote. Wote tuendelee kumtii na viongozi wetu wa kiroho kwa sababu wako hapa kumwakilisha yeye.”
Waziri Mkuu Pinda alisema wako baadhi ya watu ambao wakipata madaraka wanaona kwenda kanisani ni kero au ni kupoteza muda.
“Tatizo lao ni kutojijua, hawatambui kwamba bila Mungu hizo nafasi wasingezipata. Ninawaomba tujue kwamba kuna maisha hata nje ya utumishi wa umma na utumishi wa kisiasa,” alisema.
Alisema katika utumishi wake wa umma amejifunza mambo mengi, lakini kikubwa alichobaini ni kujua jinsi ya kuishi na watu.
“Elimu kubwa ni kujua jinsi ya kuishi na watu, hii ni elimu zaidi ya kitabuni,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kumshukru mke wake, Mama Tunu Pinda kwa kuwa nguzo ya familia na kuwalea watoto wote walionao wakati yeye akihangaika na masuala ya kitaifa.
Katika hatua nyingine, Abate Thadei, Mhagama, kutoka Abasi ya Hanga iliyoko Songea ambaye aliongoza ibada hiyo aliwataka waumini wote nchini wazidishe sala kwa kufunga na kuomba katika siku saba zilizobakia kabla ya uchaguzi mkuu kwa kile alichosema hali ni tete.
“Ninawaomba waumini wote tuzidishe sala ili kwanza pawe na amani na upendo na pia Mungu atuwezeshe kupata viongozi aliowandaa kwa maana ya Rais, wabunge na madiwani.”
Aidha, Mhagama alisema kila mwananchi anatakiwa kujiandaa kupokea matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) bila ya kuleta vurugu.
“Tumeambiwa mara kadhaa tuwe tayari kukubali matokeo, kwa vile tunamuomba Mungu kwa bidii itakuwa rahisi kukubali hayo matokeo tofauti na wale ambao wanaenda bila kuongozwa na Mungu.
Litakuwa jambo jepesi kwetu kukubali matokeo kwani tutasema Mungu amemleta yule aliyemuandaa, yule ambaye tumekuwa tukimuomba atuletee,” alisema.SOURCE: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment