ALIYESAMBAZA UJUMBE WA SAUTI KATIKA MTANDAO WA WHATSAPP, SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO YAMNASA NA KUDAKA WENGINE DAR ES SALAAM.
Dar es Salaam. Watu wanne juzi walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uwongo.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon akishirikiana na Mwanasheria Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungula mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, waliwataja washtakiwa hao kuwa ni Leila Sinare (36), Godfrey Soka (45), Deo Edmund Soka (40) na Monica Soka, wote wakazi wa Dar es Salaam.
Akiwasomea hati ya mashtaka, Wankyo alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa hayo kinyume na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Alidai kuwa kati ya Oktoba 20 na 30, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Leila alisambaza taarifa za uongo kwa njia ya sauti kupitia mtandao wa whatsapp kwenye ‘kundi la soka’, uliokuwa na lengo la kuupotosha umma katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Wakili huyo wa Serikali alidai shtaka la kwanza linamkabili Leila anayedaiwa kusambaza ujumbe usemao: “Ndugu zangu wa Kigango cha siasa, hakuna cha kutakiana uchaguzi mwema wala nini, nchi yetu inaingia kwenye machafuko muda wowote kuanzia sasa hivi.
“Kama tulivyoambiwa kwamba nchi hii itageuka kuwa nchi ya vita, ni kweli imeingia kwenye vita maboksi yenye kura feki yamekamatwa, Jimbo la Vunjo yamekamatwa maboksi matatu, tumekamata maboksi matatu feki Moshi Mjini, maboksi sita 6 Ilemela, maboksi 12 Hanang’.
“Kwa kifupi, uchaguzi umeshavurugika na Tanga nasikia magari yamesimama sehemu, makamanda wetu bado wanaendelea kufuatilia, lakini inasemekana kuna maboksi ya kura na mpaka sasa hivi hali siyo nzuri, CCM wameingiza kura nyingi feki na niseme kutokana na hali halisi ambayo ipo, hatuponi, hatuponi kwa sababu Mwanza vijana wameshaanza kuuawa, wameshakufa vijana wanne.
Watano mpaka sasa hawajulikani walipo na hali hiyo inaendelea, CCM jamani tunaomba mtuachie nchi kwa amani, kweli ingelipaswa kutuua angalau kwa sumu mkabaki wenyewe, msitutese msitutese.”
Washtakiwa Godfrey, Deo na Monica, wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 20 na 30, 2015 kwa pamoja, walisambaza taarifa za uongo kwa njia ya mtandao wa whatsapp ujumbe kama aliousambaza Leila kwa lengo la kuupotosha umma.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 3, kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa waliachiwa kwa dhamana.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment