CCM YAENDELEA KUTESWA NA UKAWA BAADA YA UCHAGUZI KUPITA, EDWARD LOWASSA AIPASHA TENA UKAWA.
Hatimaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa jawabu la fumbo lililodumu kwa zaidi ya wiki moja sasa kuhusiana na mgawo wa viti maalum baada ya kukamilisha hesabu zake na kuonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata pigo baada ya viti vyake kupungua huku wapinzani wakivuna zaidi.
Kwa mujibu wa mgawo huo uliotokana na matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, CCM imeendelea kuongoza kwa kupata viti 64 huku wapinzani wake, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD vikipata jumla ya viti 46.
Hata hivyo, mgawo huo hauvigusi moja kwa moja vyama vya NCCR-Mageuzi na NLD kwani havikufikia sifa ya chini ya kupata jumla ya kura za ubunge kufikia walau kiwango cha asilimia tano ya kura zote halali za majimbo yote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema kwa mujibu wa Ibara ya 66(1)(B) na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, mgawo unaipa CCM viti hivyo 64, Chadema viti 36 na CUF viti 10.
Akieleza juu ya mgawanyo huo, Jaji Lubuva alisema ni kwa mujibu wa uamuzi wa serikali mwaka 2010 unaotaka idadi ya wabunge wa viti maalum kuongezwa kutoka asilimia 30 ya wabunge wote hadi kufikia asilimia 40.
"Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Viti Maalum ni 113. Kutokana na kuwapo kwa majimbo nane ambayo hayakufanya uchaguzi, mgawanyo wa viti maalum kwa sasa ni 110. Viti vitatu vilivyobaki vitagawanywa baada ya kufanyika kwa uchaguzi katika majimbo hayo," alisema Lubuva.
Kadhalika, Lubuva alisema majina ya wabunge wa viti hivyo maalum yatapatikana katika vyama husika kwa mujibu wa orodha iliyowasilishwa NEC na kila chama.
Kwa mujibu wa Lubuva, mgawanyo wa viti umezingatia idadi ya kura halali za ubunge ambazo kila chama imezipata katika majimbo. CCM waliongoza kwa kupata kura zaidi ya milioni 8.8, Chadema wakifuatia kwa kupata kura 4,627,923 huku CUF wakipata kura 1,257,057. Vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi huo vikiwamo vya NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo ambavyo kila kimoja vilipata mbunge mmoja katika majimbo havikufanikiwa kupata idadi ya chini ya kura zinazotoa fursa ya kuwapo kwa viti maalum ambayo ni walau asilimia 5 ya kura zote.
CCM WAPUNGUA, UKAWA WAVUNA ZAIDI
Katika Bunge lililomalizika, idadi ya wabunge wote wa viti maalum ilikuwa 110.
Hadi kufikia wiki ya kwanza ya Novemba 2010, wakati viti sita vingine vikisubiriwa kutokana na baadhi ya majimbo kusubiri uchaguzi, NEC ilitangaza mgawo ulioonyesha kuwa CCM ilivuna viti 65 ambavyo vilikuwa sawa na asilimia 62.5 ya viti 104 vilivyotangazwa kipindi hicho; Chadema viti 23, sawa na asilimia 22.12 huku CUF ikipata viti 10, sawa na asilimia 9.62. Hivyo, wakati huo wa wiki ya kwanza ya Novemba 2010, kwa pamoja, CUF na Chadema vilipata viti 33, sawa na wastani wa asilimia 31.73.
Hata hivyo, katika mgawo wa sasa uliotangazwa pia katika wiki ya kwanza ya Novemba (jana Novemba 6, 2015), CCM imejikuta ikiwa na viti 64 ambavyo ni sawa na asilimia 58.18 ya viti vyote 110 vilivyotanagazwa jana; Chadema viti 36, sawa na asilimia 32.73 huku CUF ikipata viti 10 ambavyo ni asilimia 9.09 ya viti hivyo. Na kwa ujumla wake, Chadema na CUF vya kambi ya Ukawa vimepata viti maalum vya jumla ya asilimia 41.82.
Kwa ujumla, mgawo wa viti maalum wa asilimia 58.18 walioupata CCM jana umeonyesha kuwa chama hicho tawala kimeporomoka kwa takriban asilimia 4.32 kulinganisha na mgawo uliotangazwa kipindi kama hiki mwaka 2010; huku Ukawa wakivuna zaidi kwani asilimia 41.82 walizopata ni sawa na ongezeko la asilimia 10.09 kulinganisha na mgawo uliotangazwa wiki ya kwanza ya Novemba 2010.
BUNGENI PATAKUWA HAPATOSHI
Kufuatia mgawo wa viti maalum kwa kila chama uliotangazwa jana, maana yake CCM iliyokuwa tayari imeshajizolea wabunge 183 waliotokana na ushindi walioupata kwenye majimbo, sasa watakuwa na jumla ya wabunge 247.
Idadi hii ni mbali na wabunge wengine watokanao na nafasi 10 za uteuzi alizo nazo Rais Dk. Magufuli na pia wengine wanaoingia bungeni kutokana na nafasi zao, wakiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, kambi ya Ukawa ambayo tayari ilishakuwa na wabunge 74 waliotokana na ushindi kwenye majimbo (Chadema 34, CUF 39 na NCCR 1), sasa itakuwa na jumla ya wabunge 120. Hiyo maana yake ni kwamba uwiano kati ya wabunge wa CCM na wale wa Ukawa hadi kufikia jana ni 120: 247.
Kwa hesabu hizo, ni wazi kwamba Bunge la 11 chini ya utawala wa serikali ya Rais Magufuli linatarajiwa kuwa na mchuano mkali zaidi wa hoja kutoka kila upande na hivyo kustawisha demokrasia ndani ya chombo hicho ambacho ni mhimili mmojawapo muhimu wa dola.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa katika Bunge lililopita, ingawa wapinzani hawakuwa na idadi kubwa ya wabunge kulinganisha na sasa, bado kulikuwa na hoja kadhaa moto huku wabunge wa kila upande wakionyesha umahiri katika kuibua hoja nzito za kulinusuru taifa kutoka katika vitendo vya ukiukwaji wa sheria kama ilivyodhihirika wakati wa sakata la "Operesheni Tokomeza".
Kadhalika, wabunge katika Bunge la 10 walikuwa mstari wa mbele pia kupiga vita vitendo vya rushwa na ufisadi kama ilivyokuwa katika kuibua na kujadili kiundani kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kashfa nyingine mbalimbali za ufujaji wa fedha katika manunuzi ya umma zilizokuwa zikifichuliwa kupitia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Bunge la 11 linatarajiwa kuanza vikao vyake Novemba 17, 2015.CHANZO: THE GUARDIAN
0 comments:
Post a Comment