JESHI LA POLISI LAMFUKUZA KAZI TRAFIKI BAADA YA VIDEO KUZAGAA IKIMUONYESHA ANAOMBA NA KUPOKEA FEDHA KUTOKA KWA DEREVA WA GARI NDOGO TANGA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji
JESHI la Polisi mkoani Tanga limemfukuza kazi kwa kosa la fedheha aliyekuwa askari wake katika Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo Anthony Temu (46) wa Kituo cha Polisi Kabuku wilayani Handeni.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji, kufukuzwa kwa askari huyo kumetokana na taarifa ya kuomba na kupokea rushwa iliyopatikana kupitia mitandao ya kijamii.
Alisema Novemba 9, mwaka huu saa 7.30 mchana kupitia mitandao ya kijamii, alionekana askari mmoja wa kikosi cha usalama barabarani akipokea rushwa kutoka kwa dereva wa gari alilokuwa amelisimamisha kutokana na makosa ya usalama barabarani.
Alisema; “Katika ufuatiliaji ilibainika kwamba eneo la tukio ni katika kijiji na kata ya Kitumbi iliyopo wilayani Handeni Mkoa wa Tanga katika Barabara Kuu ya Segera- Chalinze … askari aliyebainika kutenda kosa hilo ni F. 785 Anthony Temu na kutokana na uzito wa kosa lenyewe alichukuliwa hatua za haraka za kinidhamu.
“Amekamatwa na tayari mashitaka ya kijeshi yameendeshwa dhidi yake na kutiwa hatiani ambapo amepewa adhabu ya kufukuzwa kazi kwa fedheha … hivi ninavyoongea nanyi hapa ameshafukuzwa kazi si askari tena tangu jana (juzi) jioni.”
Alisisitiza mtuhumiwa huyo ameshakabidhiwa kwa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na kielelezo ambacho ni video iliyokuwa ikirushwa kwenye mitandao ya kijamii ili waendelee kumshughulikia kwa upande wa jinai katika makosa ya kuomba na kupokea rushwa.
Hata hivyo, alisema Polisi mkoani Tanga inawashukuru wananchi hao walioibua taarifa hizo na kuwataka kuliarifu kuhusu matukio yoyote yanayohusisha ukiukwaji wa maadili katika jeshi hilo.
0 comments:
Post a Comment