BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MKUU WA WILAYA YA KINONDONI AWASWEKA RUMANDE MAOFISA 20 ARDHI KWA KUMUUDHI TU JIJINI DAR ES SALAAM.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.  

Dar es Salaam. Kasi ya uimarishaji utumishi wa umma imewakumba maofisa ardhi 20 wa Manispaa ya Kinondoni baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaweka rumande kwa saa sita kwa kuchelewa kuwasili katika ziara ya kutatua migogoro ya ardhi.

Makonda alisema jana kuwa uongozi wa Manispaa hiyo ulitakiwa kutembelea Kata ya Wazo mapema saa 2:00 asubuhi na kutoa maelekezo namna ya kutatua migogoro ya ardhi inayoendelea katika eneo hilo iliyosababisha vifo vya watu saba mwaka jana.

Kwa mujibu wa Makonda, yeye ndiye aliyekuwa akiongoza ziara hiyo, lakini asingeweza kuanza kusikiliza malalamiko ya wananchi mapema bila ya kuwapo kwa maofisa hao ambao walifika baada ya saa tatu zaidi ya muda uliopangwa.

“Hii haikubaliki hata kidogo. Mimi niliwasili kwa wakati, Ofisa Tawala wa Wilaya (DAS) aliwasili kwa wakati na hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni aliwasili kwa wakati.

“Tulilazimika kuwasubiri (maofisa ardhi) kwa saa tatu nzima hadi saa 5 asubuhi kwa sababu bila wao hakuna kitu ambacho kingefanyika,” alisema. Makonda alisema baada ya kubaini muda uliosalia usingetosha kufanya ziara hiyo, alilazimika kuiahirisha na kuamuru kukamatwa maofisa hao kwa kosa la dharau na kukosa heshima kwake yeye kama kiongozi. Alisema uamuzi huo aliufanya ndani ya sheria kama Mwenyekiti wa baraza la ulinzi na usalama la wilaya hiyo.

“Nina imani saa sita hizo walizokaa ndani zitakuwa somo kwao na watumishi wengine wa umma kujali muda,” alisema mkuu huyo wa wilaya kwa njia ya simu.

Alisema ziara hiyo itaendelea leo kuanzia saa 2:00 asubuhi na anaamini watumishi waliopangwa wakiwamo maofisa hao watafika mapema iwezekanavyo katika eneo hilo. Alisema uamuzi wake huo huenda ukatafisriwa kuwa ni mkali miongoni mwa watu, lakini hivyo ndivyo inavyotakiwa katika kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa watumishi wa umma wavivu na wenye dharau.

Alisema Rais Magufuli alieleza wazi wakati wa uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa wananchi wanaitegemea Serikali kutatua matatizo yao, hivyo watumishi wazembe wanatakiwa washughulikiwe mapema kabla hawajauangusha mfumo mzima wa uongozi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 kifungu cha 15 (1), Mkuu wa Wilaya ana mamlaka ya kumkamata yoyote aliyefanya kosa, lakini inaweka ukomo wa nguvu hizo.

Kifungu cha 15 (2) kinaeleza kuwa kiongozi huyo anaweza kutoa amri ya kukamatwa mtu yoyote aliyevunja amani na utulivu na kwamba uvunjifu huo usingezuilika kwa namna yoyote ile zaidi ya kumweka mtu huyo mbaroni, hapo anaweza kuagiza polisi kwa maandishi au kwa mdomo kufanya hivyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alithibitisha kukamatwa kwa maofisa hao, lakini hakuzungumzia zaidi kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.

Hata hivyo, Mratibu wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alipinga uamuzi huo akieleza Makonda alifanya nje ya mipaka ya kisheria.

“Kosa la kuchelewa kazini ni suala linalohusu kazi, hivyo ilibidi sheria za kazi zitumike kulishughulikia na si vinginevyo. Kitendo cha Makonda kuagiza maofisa hao kukamatwa kama waliofanya makosa ya jinai siyo haki na ni mambo ya kikoloni,” alisema Ole Ngurumwa.

Hii ni mara ya pili kwa mkuu wa wilaya kuadhibu watumishi wa umma baada ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Shinyanga, Amani Mwenegoha kumfukuza kazi daktari wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Dk Johanne Mkobwe kwa madai ya kugoma kutoa huduma za matibabu kwa mtoto wa umri wa miezi sita.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: