BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANAFUNZI WA KIKE WALIOSHIKA MIMBAA WAKIWA SHULENI WAPATA FURSA YA KURUDIA TENA SHULENI TANZANIA


Picha ya Maktaba ikimuonyesha mwanafunzi wa kike akikinga maji katika bomba.


SERIKALI imedhamiria kuanza utaratibu utakaoweka mazingira ya wanafunzi waliopata mimba wakiwa shule kurudi shuleni kwa lengo la kuhakikisha hawakosi elimu. 

Aidha, katika kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, kuanzia mwakani inayoeleza kutoa elimu bure, Serikali imewataka wazazi na walezi kwenda kuandikisha watoto kwani ada na michango yote imeondolewa ili kuwezesha watoto wote wapate elimu ya msingi.

Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Paulina Mkonongo alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF).

Mkonongo aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema katika maadhimisho ya mwaka huu yana kaulimbiu “Funguka, Chukua Hatua, Mlinde Mtoto Apate Elimu,” inayosaidia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014.

Alisema sera hiyo inatoa fursa ya elimu kwa watoto wote kuanzia elimu ya awali mpaka sekondari kwa elimu ya msingi kuwa ya lazima na itatolewa bila ada katika mfumo wa umma.

“Aidha, Serikali inazuia utitiri wa michango shuleni ili kuwawezesha watoto wote wapate elimu na kujenga usawa wa kijinsia shuleni, hivyo tunatarajia kupata ushirikiano wa wazazi na walezi ili kuinua udahili na mahudhurio ya watoto shuleni,” alisema Mkonongo.

Alisema mahudhurio kwa wanafunzi na uandikishaji unashuka kwa chini ya asilimia 95 kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia pamoja na michango. Hivyo alitoa mwito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri stahiki wa kuanza darasa la kwanza wanaandikishwa kwani hakuna kikwazo cha ada wala michango.

Pia alisema wanafunzi watakaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wazazi na jamii ihakikishe wanaripoti kwa kuhudhuria darasani ambapo watandaa viongozi wa kusimamia udahili na kuhakikisha kila aliyechaguliwa anahudhuria darasani.

Akizungumzia vikwazo mbalimbali vinavyofanya watoto hasa wa kike kukatisha masomo, Mkonongo alisema ni pamoja mimba na ukatili wa kijinsia kwani wanafunzi wengi wa darasa la kwanza mpaka kidato cha nne wana umri chini ya miaka 18.

Alisema kwa takwimu za mwaka 2013, wanafunzi wa kike walioacha shule kutokana na ujauzito kwa shule ya msingi ni 297 na sekondari ni 3,045. Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali inaangalia utaratibu wa wanafunzi hao kuendelea na shule baada ya kujifungua kwani elimu ni msingi wa kila kitu.

“Katika utekelezaji wa sera hii mpya suala hili litawekwa vizuri na halitakuwa na shida katika utekelezaji wake huku tukihakikisha wale waliowapa mimba wanachukuliwa hatua stahiki ili isijeonekana sasa ni wakati wa kuzalisha watoto wa kike,” alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema hata wakirejeshwa shuleni baada ya kujifungua watakuwa wameathirika kisaikolojia pamoja na kuchelewa muda wa kumaliza shule na hivyo kuwataka wadau kusaidia katika kupeleka mawazo yao juu ya utekelezaji wa suala hilo kama walivyokuwa wakiiomba serikali.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupanua fursa ya elimu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika ngazi zote za kielimu. Akizungumzia ukatili wa kijinsia, alisema ni moja ya visababishi vya utoro shuleni na kudhoofisha taaluma, na kwa takwimu za mwaka 2013, wanafunzi wa shule ya msingi 54,596 na wa sekondari 62,590 waliacha shule kwa sababu ya utoro.

Alisema jukumu la kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia ni la wote kwani kila mtoto ana haki ya kulindwa popote atakapokuwa iwe shuleni, nyumbani, kwenye vyombo vya usafiri, michezoni na njiani anapokwenda na kurudi shuleni pamoja na kumpa mbinu za kujilinda mwenyewe.

Alisema lakini wengi wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na vijana ni wenye mamlaka au dhamana ya kuwalinda au kuwaokoa na vitendo hivyo. Naye Mkurugenzi wa WiLDAF, Dk Judith Odunga, alisema katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia shuleni, wanaomba serikali kufutwa kwa adhabu ya viboko shuleni na walimu kufundishwa au kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala kwani watoto wamelalamika kuchapwa viboko tisa hadi 45.

Pia aliomba kutengeneza mwongozo wa utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 utakaotekeleza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama na kuunda pamoja na kusimamia mabaraza yatokayokuwa yanasikiliza malalamiko ya wanafunzi shuleni.

“Pia tunaomba Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kutunga sheria ya ukatili wa majumbani sambamba na kubadilisha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayohusu ndoa kwa mtoto chini ya miaka 18.

Wiki iliyopita, wakati akizindua Bunge la 11, Dk Magufuli alisema kuanzia Januari mwakani, Serikali yake itaanza kutoa elimu bure kwa elimu ya msingi ambayo ni pamoja na shule ya awali hadi kidato cha nne.

Juzi, Profesa Mchome, alisema wizara yake inaandaa mwongozo utakaotoa maelekezo juu ya muundo, mfumo na utaratibu nyumbufu utakaohakikisha kuwa ifikapo Januari mwakani, elimu ya msingi inatolewa bila malipo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: