SALAMU ZA PONGEZI KWA RAIS MPYA TANZANIA DK JOHN MAGUFULI ZAMIMINIKA KAMA MVUA
DK JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI.
SALAMU za pongezi kwa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayeapishwa leo Dar es Salaam, Dk John Magufuli zimeanza kumiminika nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kwa vyombo vya habari jana, salamu za kwanza zimetumwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Mohammed Abdelaziz wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi.
Katika salamu zake kwa Rais mteule Magufuli, Rais Kagame alisema: “Kufuatia kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kukutumia Mheshimiwa salamu za dhati, pongezi na heri nyingi kwa niaba yangu mwenyewe, Serikali yangu na wananchi wa Rwanda.
“Napenda pia kutumia nafasi hii kukuhakikishia msimamo wetu wa kudumisha na kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili na watu wake.” Rais Abdelaziz alimwambia Rais Mteule Magufuli:
“Kwa niaba ya wananchi wa Saharawi na Serikali ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi, napenda kukupongeza sana kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nakutakia mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu ya nafasi yako hiyo.” Aliongeza: “Sisi tuna uhakika kuwa chini ya uongozi wako wa busara, Tanzania itaendelea kusonga mbele na kupata maendeleo na ustawi mkubwa zaidi.”
0 comments:
Post a Comment