BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALIN YAPATA PIGO KESI YA KUAGA MWILI WA MWENYEKITI WA CHADEMA GEITA ALFONCE MAWAZO JIJINI MWANZA.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (katikati mstari wa mbele) akiwa na viongozi na wabunge wa chama hicho ndani ya chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kusikiliza kesi ya kupinga zuio la kuuga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita,  Alphonce Mawazo, jana. Picha na Michael Jamson 

Mwanza.
Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza jana ilitupa pingamizi la Serikali la kuitaka itupilie mbali kesi ya kutaka kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo na hivyo kutoa fursa kwa familia ya marehemu kufungua kesi ya msingi.

Kesi hiyo ilifunguliwa juzi na baba mdogo wa Mawazo, Mchungaji Charles Rugiko akiiomba mahakama iondoe zuio la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo kukataza kuagwa kwa mwili wa mtoto wake, lakini jana Serikali ikawasilisha pingamizi ikitaka kesi hiyo itupwe kwa madai kuwa haina hoja za msingi.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 10 ya mwaka 2015, ni Kamanda Mkumbo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mawazo aliuawa mkoani Geita Novemba 14, kwa silaha za jadi na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM na watu watano wamekwishafikishwa kortini kwa tuhuma za mauaji hayo lakini songombigo imebaki kwenye kuaga mwili wake kutokana na Serikali kukataa ikisema kuna mlipuko wa kipindupindu na kuwa mwanasiasa huyo hakuwa kiongozi wa kitaifa.

Baada ya kifo hicho, viongozi wa Chadema kwa kushirikiana na familia ya marehemu walihamisha mwili wa marehemu kutoka Geita na kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa Bugando ya jijini Mwanza ambako mwili huo ulitakiwa kuagwa kabla ya kurejeshwa Geita kwa maziko.

Tayari viongozi wakuu wa Chadema na Ukawa, wakiwamo mawaziri wakuu wawili wa zamani na wabunge wote wa Ukawa walikuwa wamekusanyika Mwanza kwa ajili ya shughuli hiyo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilizuia mkusanyiko wa kuuaga kwa madai ya kuwapo mlipuko wa kipindupindu, hatua iliyopingwa na familia ya marehemu kwa kufungua kesi mahakamani.

Mawakili wa Serikali, Seth Mkemwa na Emilly Killiya waliiomba Mahakama hiyo kutosikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa, maombi ya mlalamikaji hayakuwa ya msingi na kwamba si baba mzazi wa marehemu Mawazo hivyo hakuwa na haki ya kufungua shauri hilo.

Mawakili watatu wanaomtetea Mchungaji Rugiko, Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya na Paul Kipeja walipangua hoja hizo wakisema baba mzazi wa Mawazo alishafariki na kuwa mlalamikaji ambaye ndiye aliyemlea Mawazo angewasilisha ushahidi huo mahakamani.

Baada ya kusikiliza hoja za kila upande, Jaji Lameck Mlacha alitupilia mbali pingamizi hilo akisema halina msingi na kuamuru kesi ya msingi ifunguliwe na kuanza kusikilizwa leo.

Kesi ya msingi
Baada ya pingamizi kutupwa, Mchungaji Rugiko alifungua rasmi kesi ya msingi ambayo inaanza kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu.

Kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2015 iliyofunguliwa jana alasiri, inaoimba Mahakama kuondoa amri ya Kamanda Mkumbo kuzuia kuaga mwili wa Mawazo; kutoa tamko kwamba zuio la Mkumbo ni batili na kinyume cha sheria na kumkataza Kamanda Mkumbo kujihusisha na shughuli za mazishi na kuaga mwili wa Mawazo.

Wafuasi wafurika kortini
Tofauti na juzi, wafuasi wa Chadema jana walifurika mahakamani hapo kuanzia saa mbili asubuhi kufuatilia kesi hiyo.

Hatua hiyo ilitokana na ombi la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alilolitoa juzi wakati wa kufungua kesi hiyo la kuwataka wafuasi wa chama hicho kwenda kwa wingi mahakamani hapo.

Kutokana na wingi wa wafuasi hao, polisi waliongezeka maradufu na kutanda katika viwanja vya mahakama huku polisi wenye silaha wakiwa katika magari kila kona ya Mahakama.

Polisi waliwakagua karibu watu wote walioingia na kuwahoji sababu za kufika mahakamani hapo huku askari wengine wakiwa wamejipanga nje ya lango la kuingilia. Mbali ya mahakamani hapo, wafuasi wengine walikusanyika katika Hoteli ya Gold Crest ambako viongozi wa kitaifa wa Chadema walikuwa wamefikia.

Wenje atuliza wafuasi
Kutokana na wafuasi wa Chadema kufurika kwa wingi katika hoteli hiyo, aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje alilazimika kuwatuliza baada ya kuonekana kupandwa na jazba.

Hatua hiyo ilikuja baada ya wafuasi hao kuanza kuimba kwa sauti: “Mwisho kesho, mwisho kesho…” wakimaanisha wanataka suala hilo limalizike leo. 


Akiwatuliza, Wenje alisema: “Makamanda naomba mtulie kila kitu kitakwenda sawa, kwa sasa tutawanyike kwa amani tukutane kesho (leo) mahakamani,” alisema Wenje na wafuasi hao walitii agizo hilo na kuondoka huku wakisema: “Tumechoka mwisho kesho… tumechoka… hatuwezi kukubali.”MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: