SIFA 9 ZA WAZIRI MKUU WA RAIS MTEULE DK JOHN MAGUFULI, AWE NA SIFA KUU YA KUTOKUWA NA CHEMBE YA UFISADI
Baada ya kuchaguliwa kwa Dk. John Magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano, Watanzania wanasubiri kwa hamu kusikia jina la mtu atakayeteuliwa kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Wafuatiliaji na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaamini kuwa Waziri Mkuu ajaye atatoa picha kamili ya dhamira ya Rais mpya, Magufuli, katika utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za kuwania urais wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Maeneo 10 ambayo Magufuli amepania kushughulikia akiingia madarakani ni pamoja kubana matumizi ya serikali, kuongeza mapato ya serikali kuboresha mfumo wa utendaji na ufanisi na kupitia kodi na ushuru unaowaumiza wakulima, wafugaji na wavuvi.
Pia kupitia sheria za kubadilishwa, kuorodhesha kero za wananchi, kuunda serikali ndogo, kumaliza kero za watumishi wa umma, utekelezaji wa ilani ya CCM na kupendekeza muundo wa kitaasisi ili kutekeleza ahadi ya kutoa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji.
Waliowahi kuwa mawaziri wakuu ni pamoja na Julius Nyerere (1961-1962), Rashid Kawawa (1962 na 1972-1977)
Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984), Cleopa Msuya (1980-1983, 1994-1995), Salim Ahmed Salim (1984-1985), Joseph Sinde Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Frederick Sumaye (1995-2005), Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015).
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baada ya Dk. Magufuli kuapishwa jijini Dar es Salaam Alhamisi (Novemba 5, 2015), jina la yule atakayemteua kuwa Waziri Mkuu wake na kuliwasilisha bungeni ili lipigiwe kura, litahusisha mtu mwenye sifa walau tisa zitakazoendana na matarajio ya serikali yake.
UADILIFU
Ili Dk. Magufuli atekeleze ahadi zake na hasa ile ya kupambana na ufisadi na rushwa, ni lazima awe na Waziri Mkuu asiyekuwa na chembe ya kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, ikiwamo ya awamu ya nne ya uongozi wa nchi hii, kuliibuka kashfa kadhaa za ufisadi na rushwa kiasi cha kuitikisa serikali ya Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake.
Kashfa hizo ni pamoja na ile ya uchotwaji fedha katika akaunti ya Benki Kuu ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ukodishwaji wa mitambo ya umeme ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ripoti chafu ya Msimamizi na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) na ile ya ufisadi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu (BoT).
Lowassa aliwajibika kufuatia kashfa ya Richmond mwaka 2008 wakati Pinda alinusurika kwenye kashfa ya Escrow baada ya kusafishwa na Bunge.
Hali hiyo inafanya sifa mojawapo kubwa ya Waziri Mkuu ajaye kuwa ni uadilifu na usafi wa kiwango cha juu, tena usiotiliwa shaka na yeyote.
UKANDA
Kwa kuwa Dk. Magufuli anatoka mkoa wa Geita, ambao uko Kanda ya Ziwa, bila shaka Waziri Mkuu ajaye atakuwa na uwezekano mdogo wa kuteuliwa kutoka katika kanda hiyo au zile za jirani.
Pamoja na ukweli kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo zimefanikiwa kupiga vita ukabila, lakini bado suala hilo limekuwa likichukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Wafuatiliaji wa masual ya siasa nchini, wanaamini Rais mteule, Dk. Magufuli, ataangalia jiografia ya nchi na kuhakikisha kuwa msaidizi wake mkuu wa shuguhuli za serikali anatoka sehemu nyingine ya nchi. Na pia anatarajiwa, walau, kutotoka sehemu moja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye anatokea Zanzibar.
KUJIAMINI, MTU WA MAAMUZI MAGUMU
Mtu anayetarajiwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali itakayoongozwa na Rais Dk. Magufuli anatakiwa kuwa na sifa ya kujiamini na uwezo mkubwa wa kutoa maamuzi magumu pale inapobidi.
Kutokana na unyeti wa kazi yenyewe na changamoto zinazokabili taifa kwa sasa, bila shaka Waziri Mkuu ajaye anapaswa kuwa mtu asiyeyumba.
Mathalani, umahiri wake unapaswa kudhihirika kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kwenye bunge na pale serikali itakapokuwa na hoja za kujibu.
Kadhalika, kwa kuwa Waziri Mkuu ndiyo mtendaji mkuu wa serikali, anatakiwa kutoa maamuzi magumu, hasa pale nchi itakapokuwa na masuala nyeti yanayohitaji uamuzi makini na wa haraka.
ASIYEMZIDI RAIS MAGUFULI KWA UMAARUFU
Uzoefu unaonyesha kuwa watu wengi waliowahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu ni wale wanaosifika kwa utekelezaji zaidi. Watu hawa hutakiwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi na umakini mkubwa, lakini bila ya kumzidi Rais aliyeko madarakani kwa sifa au umaarufu.
Rekodi za nyuma zinaonyesha kwa mfano, nyota ya siasa ya Mwalimu Nyerere ilikuwa juu kisiasa licha ya kufanya kazi na mawaziri wakuu tofauti waliokuwa wachapakazi kwelikweli kama Kawawa, Sokoine, Msuya na Salim.
Hata Warioba na Malecela waliposhika wadhifa huo kwenye awamu ya pili chini ya Rais Mwinyi au Sumaye alipofanya kazi kwa miaka 10 na Mkapa, bado nyota za marais wao zilikuwa juu.
UWEZO KUSIMAMIA UTEKELEZAJI
Sifa mojawapo ya Waziri Mkuu mpya chini ya Dk. Magufuli ni uwezo wa kusimamia na utelekezaji wa dhati wa mipango ya serikali.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, yeye hana nafasi na mawaziri wanaoendekeza kauli za ‘mchakato’, ‘tuko mbioni’ wala ‘tuko katika hatua nzuri’, bali anachotaka ni vitendo zaidi katika utekelezaji. Siyo blaablaa, na mwenyewe Magufuli amedhihirisha hilo katika utendaji wake kwenye wizara mbalimbali alizowahi kuongoza, ikiwamo anayomaliza nayo sasa ya Ujenzi.
Dk. Magufuli alijizolea sifa kubwa kutokana na utendaji wake, hasa katika kusimamia ujenzi wa barabara sehemu mbalimbali nchini na bila kusahau alipokuwa Wizara ya Ardhi na ile ya Mifugo na Uvuvi.
Waziri Mkuu mpya bila shaka atatakiwa angalau kufanana au kumzidi Magufuli kutokana na ukweli katika serikali ijayo kuna mengi ya kutekeleza.
Pia anatakiwa kuwa mtendaji mzuri kwani ana kazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
KINARA WA KWELI SHUGHULI ZA SERIKALI BUNGENI
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, miongoni mwa viongozi wanaokumbana na changamoto kali za wapinzani bungeni ni mawaziri wakuu.
Hawa ndio wamekuwa na kibarua cha kuwa vinara katika kukabili shinikizo kutoka kwa wapinzani, hasa katika kufafanua masuala ya utendaji.
Pia kuna kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni, ambacho pia ni aina nyingine ya ‘kitimoto’ kwa viongozi hawa.
Bila kusahau kumekuwa na kashfa na tuhuma nyingi zikiibuliwa dhidi ya serikali, na hapo ndipo umahiri wa Waziri Mkuu huhitajika maradufu. Ni kwa sababu yeye ndiye kioo cha serikali linapokuja suala la masuala nyeti.
KUKUBALIKA NDANI, NJE CCM
Dk . Magufuli wakati akiteua Waziri Mkuu mpya, atalazimika kuwa na mtu mwenye sifa hii ya kukubalika na kuheshimika ndani na nje ya CCM. Hapaswi kuwa mtu mwenye kuzua maswali kwa jamii kutokana sifa na uzoefu wake wa uongozi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mtu huyo, ndiye pia atakayetoa taswira ya serikali ya Dk. Magufuli, hasa katika dhamira ya kutekeleza ahadi zake na pia anatakiwa kulinda maslahi ya chama chake.
Anatakiwa kuwa mtu safi, ambaye jamii itakuwa na imani naye pale atakapochaguliwa kushika wadhifa huo.
MTU ASIYEWAZIA URAIS
Pamoja na dhamira njema ya Rais Kikwete ya kuwatumikia vizuri Watanzania, lakini moja ya matatizo yaliyomkabili ilikuwa ni kitendo cha baadhi ya mawaziri kuunda mitandao ya maandalizi ya urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2005, baadhi ya watendaji wa serikali na wale wa CCM walianza kazi ya kuandaa mikakati na kutengeneza mitandao ya kumrithi Rais Kikwete.
Mitandao hiyo ilisababisha kuporomoka kwa utendaji wa baadhi ya mawaziri na mbaya zaidi, kulitokea kutoelewana na hata kuwapo kwa migawanyiko ya wazi.
Kufuatia hali hiyo, kulizuka mtindo wa baadhi ya mawaziri kubaki na kazi moja ya kuchafua wenzao huku wengine wakihangaika kujijenga kisiasa badala ya kufanya kazi waliyotumwa na rais na matokeo yake kushuka kwa utendaji katika baadhi ya wizara.
Hali hiyo ilisababisha CCM kuwaomba Rais mstaafu Mwinyi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kufanya kazi ya kusuluhisha makundi ndani ya chama hicho.
Ni dhahiri kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya Dk. Magufuli atakuwa ni mtu asiye na makundi wala asiwe na ndoto za wazi za kuwa mrithi wa Dk. Magufuli kwa nafasi ya urais.
UZOEFU SERIKALINI
Dk Magufuli wakati anamteua Waziri Mkuu ajaye atapaswa kuangalia mtu mwenye uzoefu na masuala ya uongozi.
Waziri Mkuu kwa kawaida ndiye mtendaji mkuu wa serikali. Na ndiyo maana ni muhimu akawa na uelewa mpana wa namna serikali inavyofanya kazi na mifumo yake.
Serikali ina mfumo mpana, ambao bila ya mtu kuufahamu vizuri itakuwa ngumu kuongoza.
Mathalani, Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Mizengo Pinda, kabla ya kushika wadhifa huo, alikuwa na uzoefu mkubwa wa utumishi serikalini kwa kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ikulu na kuwa Naibu Waziri na waziri kamili wa masuala ya Tamisemi.
Pia mawaziri wakuu waliomtangulia waliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kabla ya kupata nafasi hiyo. Ni wazi kuwa Rais Dk. Magufuli atazingatia eneo hili ili kumpata mtu makini atakayetimiza dhamira ya kuwavusha Watanzania kutoka katika lindi la umaskini.
Kibarua hiki kiko kwa Rais Dk. Magufuli katika kuteua jina la mtu anayeamini kuwa anamfaa kwa nafasi ya uwaziri mkuu na pia wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakaofanya kazi ya kumpigia kura baada ya kufikishiwa jina hilo katika kikao chao cha kwanza cha Bunge la 11.CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment