UKAWA WAKWAMA KUFANYA MAANDAMANO YENYE LENGO LA KUPINGA UBAKWAJI WA DEMOKRASIA TZ
Dar/Mikoani. Polisi jana waliimarisha ulinzi katika maeneo mengi nchini kukabiliana na maandamano yaliyodaiwa kupangwa na wafuasi wa Chadema nchini kupinga kile walichoita ubakaji wa demokrasia.
Hata hivyo, katika maeneo hayo hapakuwapo na maandamano yaliyoombewa vibali na wafuasi hao na kuzuiwa na polisi.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja, alisema jana kuwa jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachoonyesha viashiria vya uvunjifu wa sheria na kutaka kuvuruga amani.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana wakati wa mkutano wa amani uliofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ya viongozi wa dini wa mkoa huo kuwa ulinzi utaimarishwa hadi Rais mteule, Dk John Magufuli atakapoapishwa kesho.
“Tuliahidi vikosi vyetu vya usalama vitaimarisha ulinzi wakati wa kampeni, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Tumefanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo hadi mchakato huo utakapokamilika kesho,” alisema.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja.
Ulinzi
Katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, polisi waliovalia vifaa vya kudhibiti ghasia walikuwa katika doria tangu saa 12 asubuhi katika maeneo mbalimbali.
Huko mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha alisema jana kuwa Kamanda wa Polisi wilayani hapo, George Kyando amezuia maandamano yaliyokuwa yafanyike asubuhi.
Katibu wa Chadema, Mkoa wa Geita, Soud Ntanyagara alisema waliomba kibali cha maandamano ambayo yangeanzia mjini Ushirombo saa 5.30 asubuhi hadi Uwanja wa Kilimahewa lakini yalikataliwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema hatapokea barua yoyote ya kuomba maandamano kwa kuwa mwelekeo wake ni wa kuvunja amani.
Hata hivyo, Katibu wa Chadema mkoa huo, Calist Lazaro alisema wamesitisha maandamano hayo kwa sababu za kichama na si kwa amri ya kamanda huyo.
Mkoani Mwanza, kiongozi wa operesheni Kanda ya Ziwa Magharibi, Chadema, Tungaraza Njugu alisema maandamano yamekuwa magumu kwa sababu polisi wamekuwa wakisambaratisha makundi ya watu. Malumbano yaliibuka kati ya Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani akisema yeyote atakayethubutu kuandamana atakabiliana na nguvu za Dola huko Katibu wa Chadema Wilaya ya Moshi, Mohamed Ally akisema kuandamana ni haki ya kikatiba ya kila mtu.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment