WALIOWADOSHA MAWAZIRI KATIKA UCHAGUZI MKUU 2015 WAELEZA NAMNA WALIVYOTUMIA MBINU MBADALA YA KUWANG'OA KATIKA SANDUKU LA KURA.
Wabunge wateule waliogombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamefanikiwa kuwaangusha mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne waliogombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Washindi dhidi ya mawaziri hao wameongea na Nipashe Jumapili kwa nyakati tofauti na kuelezea `tamu na chungu’ ya kukabiliana na waliopo serikalini wakati wa uchaguzi.
Mawaziri walioangushwa na kuleta mshangao kwa jamii ni pamoja na ‘mkongwe’ Stephen Wassira (Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika) aliyeng’olewa na Ester Bulaya katika jimbo la Bunda Mjini.
Wengine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri aliyeangushwa na Dk. Godwin Mollel huko Siha, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, akiangushwa na Marwa Ryoba jimboni Serengeti.
Pia yumo Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi aliyeshindwa na Pascal Haonga katika jimbo la Mbozi Mashariki.
DK. GODWIN MOLLEL
Anasema juhudi binafsi na nguvu ya umma iliyodhihirika kupitia sanduku la kura vilifanikisha azma kuu ya mabadiliko jimboni humo.
Anasema umma ulisikia na kuikubali ilani ya uchaguzi ya Chadema inayoungwa mkono na vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hivyo kuiangusha CCM katika uwakilishi wa jimbo hilo.
“Umoja wa wananchi wa Siha kutaka mabadiliko na maendeleo yaliyoshindwa kuletwa na CCM ni siri kubwa iliyosababisha kumwondoa Mwanri,” anasema Dk. Mollel.
Anasema viongozi wa Chadema jimboni Siha walitumia mbinu zote kwa siri ambayo haikuwafikia hata mawakala kutokana na hofu ya kuwafikia CCM.
“Tuliwachukua mawakala kutoka nje ya Siha baada ya wengi waliokuwapo kubainika kwamba walihongwa kutuhujumu,” anasema.
Alisema wanachama wa Chadema jimbo hilo walilinda kura usiku na mchana katika vituo vilivyokuwa na dalili za wizi, na kuilinda ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya aliye msimami wa uchaguzi huo.
ESTER BULAYA
Bulaya anaweza kuitwa shujaa kutokana na mikikimiki aliyoipata hata kufikia uamuzi wa kuihama CCM na kujiunga Chadema.
Wakati Siha walibadili mawakala, kule Bunda waliweka mawakala wenye hofu ya Mungu, kwa mujibu wa Bulaya.
Anasema walifanya hivyo ili kuwa na uhakika kwamba watakataa vishawishi kutoka kwa watu wenye uwezo wa kifedha.
“Niliwatafuta mawakala wanaotaka mabadiliko na wanaotaka maendeleo hapa Bunda, hivyo niliwachagua kwa umakini mkubwa,” anasema.
Anasema kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho alimwomba Mungu na kujiamini na kuomba kura kwa wananchi wa Bunda.
Pia anaeleza kuwa kabla ya kazi ya kupiga kura kuanza aliwaambia mawakala wake kuwa ameshafanya kampeni na hatima ya wananchi wa Bunda ipo mikononi mwao.
MARWA RYOBA
Aligombea ubunge mwaka 2010 na Waziri Kebwe alipoambuliwa asilimia 41 ya kura dhidi ya 54 za Dk. Kebwe.
Baada ya kushindwa alirudi kuendelea na kazi ya ualimu na baadaye alisimamishwa kazi na kuamua kurudi tena katika masuala ya siasa jimboni humo.
Anasema alitumia muda huo kufungua matawi ya Chadema kwenye vijiji vyote vya Serengeti na mwaka 2011 aligombea udiwani katika kata ya Stendi Kuu na kushinda kwa asilimia 70.
“Sikuwa na fedha kabisa, ukizingatia nilikuwa mwalimu na nikafukuzwa, hivyo nilitumia kiinua mgongo nilichopewa cha Shilingi milioni tisa kati ya hizo, milioni mbili nikaipatia familia yangu na milioni saba nikawekeza kwenye kampeni,” anasema Ryoba.
Anasema aliwaandaa mawakala wake kisaikolojia na kuwatumia vema Red Brigade kutimiza wajibu wao ipasavyo hasa katika kulinda kura.
PASCAL HAONGA
Anaeleza kuwa kazi ya kumwondoa Zambi ilikuwa ngumu, hivyo mbali na kufanya kampeni katika majukwaa alifika nyumba hadi nyumba.
Anasema alikuwa na mawakala waaminifu waliokataa kurubuniwa kwa fedha, bali kusimamia haki kwa wananchi wa Mbozi.CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment