JAKAYA KIKWETE AIBUKIA AFRIKA YA KUSINI KATIKA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA NA CHINA.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, wakiangalia mfano wa ndege ya kivita wakati walipotembelea mabanda ya maonyesho ya Mkutano Mkuu wa Tano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China, uliofanyika Jijini Johannesburg, Afrika Kusini juzi. Picha na OMR
Dar es Salaam. Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ameibukia kwenye Mkutano wa Tano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Katika mkutano huo ambao Rais John Magufuli anawakilishwa na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, Kikwete amealikwa kama rais mstaafu.
Marais wengi wa Afrika, wako nchini Afrika Kusini kwa mwaliko wa Serikali ya China na Afrika Kusini ambao wanakutana na Rais wa China, Xi Jinping anayefanya ziara barani Afrika na kuhudhuria mkutano wa ushirikiano wa Afrika na China.
Mkutano huo una lengo la kudumisha maendeleo ya pamoja kati ya Afrika na China na zaidi, kuibua maeneo ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea.
Pia, mkutano huo unaangalia ushirikiano kwa mataifa ya Kusini mwa Afrika na zaidi kuleta maendeleo ikiwamo masuala ya kisiasa, miundombinu, kutumia masoko miongoni mwa mataifa ya Afrika na kuimarisha nafasi za kibiashara.
Mpango huo wa ushirikiano kati ya China na Afrika unaoitwa FOCAC, uliasisiwa Oktoba mwaka 2000 mjini Beijing na lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano wa Afrika na China.
Tangu kuanzishwa kwake, mikutano mbalimbali imefanyika ukiwamo wa mawaziri na mmoja wa wakuu wa nchi.
Mkutano huo umekuwa kiungo muhimu kwa mataifa ya Afrika katika nyanja mbalimbali za ushirikiano wa kibiashara.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa China, Xi alisema Afrika ni mshirika mzuri na China haioni kwanini isidumishe ushirikiano huo.
Alisema nguvu ya mataifa ya Afrika na China ikiimarishwa, itasaidia kupambano dhidi ya ugaidi unaoitishia dunia, mabadiliko ya hali ya hewa na kuporomoka kwa uchumi.
Kutokana na hali hiyo, uchumi na ushirikiano utakuwa wa mafanikio kwa kuwa China imetaka kuimarishwa baadhi ya maeneo kwa faida na maendeleo ya Afrika.
Katika mkutano huo, unaohudhuriwa na marais wa Afrika zaidi ya 50, Rais Xi alisema Afrika inatokana na Waafrika na masuala yote ya Afrika yatamalizwa na waafrika wenyewe.
Naye mwenyeji wa mkutano huo, Rais Jacob Zuma alisema ushirikiano wa China na Afrika utakuwa wa manufaa.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment