BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI AWASOMBA WATUMISI 70 NDANI YA SIKU 34 TU YA UTAWALA WA SERIKALI YAKE TANZANIA.


Dar es Salaam.
Sekeseke la Rais John Magufuli katika maeneo aliyopitia ndani ya siku 34 tayari limewasomba watu 70 wakiwamo watumishi na wajumbe wa bodi za mashirika au taasisi husika wakidaiwa ama kushindwa kuwajibika au kusimamia maeneo yao.

Walioangukiwa na ‘rungu’ la Rais huyo ni watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Wizara ya Uchukuzi.

Tangu alipoanza kazi hiyo hadi jana ni siku 34 tu, sawa na wastani wa watumishi wawili kila siku.

Rais Magufuli ambaye kwa sasa ameteka sehemu kubwa ya mjadala ndani na nje ya nchi kutokana na kasi yake, alihutubia Bunge na kuahidi kutumbua majipu yote sugu, akimaanisha kushughulikia kuziba mianya ya ufisadi, urasimu na rushwa inazofanywa na watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mapato ya nchi.

Rais Magufuli alitangaza kiama kwa watendaji wa Serikali wasiotekeleza wajibu wao katika kusimamia, kudhibiti na kuwajibika ipasavyo.

Waliokutana na rungu hilo ni wale waliosimamishwa kazi, kufutwa kazi mara moja huku wengine wakipandishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi.

Novemba 9, Muhimbili
Rais Magufuli alifanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kubaini udhaifu mkubwa kiutendaji, hatua iliyosababisha amuondoe kaimu mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo, Hussein Kidanto na kuvunja bodi ya wakurugenzi wa hospitali iliyokuwa na wajumbe 11, akiwamo Kidanto.

Novemba 27, TRA
Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walishusha rungu katika ofisi za TRA na TPA na kumsimamisha kazi Kamishna wa mamlaka hiyo, Rished Bade na maofisa watano ambao ni Habibu Mponenzya wa Kitengo cha Huduma kwa wateja, Hamis Ali Omari wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano na Haruni Mpande.

Wengine ni Eliachi Mrema kutoka kitengo cha Bandari Kavu TPA na Kamishna wa Kodi na Forodha TPA, Tiagi Masamaki.

Siku iliyofuata, Majaliwa aliagiza watumishi watatu zaidi waliokuwa wamehamishiwa Mwanza wasimamishwe kazi TRA ambao ni Anangisye Mtafya, Msajigwa Mwandengele na Robert Nyoni ili kupisha uchunguzi dhidi yao.

Hadi jana, Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi, Richard Kayombo alithibitisha kuwa jumla ya watumishi katika mamlaka hiyo waliochukuliwa hatua hizo ni 36, huku 12 kati yao wakipandishwa mahakamani.

Desemba 7, TPA na Uchukuzi
Katika mwendelezo wa kutembeza rungu hilo, juzi Rais Magufuli kupitia aliwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa TPA, Awadhi Masawe pamoja na watumishi wengine wanane.

Majaliwa aliagiza waliosimamishwa kazi kwa kuhusishwa na ukwepaji kodi wa makontena 2,387 wanapaswa kukamatwa mara moja, kuhojiwa na hatimaye waisaidie Bandari kujua makontena yasiyolipiwa kodi yalipaswa kutozwa kiasi gani cha fedha.

Aliwataja viongozi hao wa TPA kuwa ni Meneja Mapato ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu kitengo cha Fedha, Shaban Mngazija; aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD) ambaye sasa amehamishiwa Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi, Rajab Mdoe; Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Ibin Masoud; na Meneja Bandari Msaidizi ( Fedha), Apolonia Mosha.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataja wengine wanane waliosimamishwa kazi Bandari Kavu kuwa ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante na James Kimwomwa ambaye alihamishiwa Mwanza lakini kuanzia sasa anasimamishwa kazi akiwa kwenye mkoa huo.

Bodi ya wajumbe wanane iliyovunjwa na Rais Magufuli jana ilikuwa ikiongozwa na Profesa Joseph Msambichaka huku wajumbe wakiwa Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson; Mhandisi wa Ujenzi, Musa Ally Nyamsingwa; Mtaalamu wa Manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya Posta, Donata Mugassa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.

Wajumbe wengine ni Flavian Kinunda, Mhandisi Gema Modu, Dk Francis Michael na Crescentius Magori. Hadi sasa jumla ya watumishi waliokutana na rungu la Rais Magufuli TPA ni 22.

Maoni ya wachambuzi
Kutokana na hatua hizo za muda mfupi, Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema hakuna namna nyingine, lazima Rais Magufuli aendeleee na kasi hiyo. “Kama kuna mwizi au mzembe basi anatakiwa kuacha mara moja, najua inaweza kuathiri baadhi, lakini hali hiyo baadaye wataizoea tu,” alisema.

Profesa Shumbusho alisema kuna kundi la viongozi waliokuwa na mchezo wa kuendesha nchi kwa ujanja ujanja na ndiyo sababu ilijengeka dhana ya Watanzania wamerogwa, kwa kuwa wanamiliki rasilimali nyingi, lakini umaskini unazidi.

“Mwalimu Julius Nyerere hakuna aliyekuwa amemzoea na wote walijua msimamo wake, sasa inawashtukiza kwa Rais Magufuli kwa sababu muda umepita, Rais ukionekana na wewe mpigaji watakusogelea tu, lakini ukiwa tofauti hakuna ujanja ujanja, uwajibikaji wa watumishi unategemeana na Rais anawaongozaje,” alisema Profesa Shumbusho.

Mwanaharakati wa masuala ya Haki za Binadamu na Haki za Kiraia kutoka Mtandao wa TGNP, Gema Akilimali, alisema anachokifanya Rais Magufuli kinahitaji kupongezwa na aendelee na kasi hiyo hiyo.

Alisema taifa lilikuwa limeyumbishwa na wachache huku wanyonge ambao ni watu wa hali ya chini wakibakia kwenye umaskini.

“Nchi ilikuwa imekosa nidhamu, yaani watumishi walijisahau sana, walifanya lolote wakijua hakuna anayeweza kuwaadhibu, ukwepaji kodi ulikithiri, hivyo anawaonyesha jinsi gani alivyo makini na hilo,” alisema.

“Malalamiko hayo ya ufisadi na urasimu wa watendaji yalikuwapo kando kwa hivyo ameamua kuanza nayo, lakini pia ndiyo sehemu sahihi ilikuwa na ugumu, udhaifu wa makusanyo ya kodi, nadhani yuko sahihi aendelee kutikisa huo uozo kwanza.”

Hata hivyo, Akilimali alisema Rais Magufuli anatakiwa kuchukua hadhari mapema ya kuendelea na utaratibu huo na badala yake atengeneze msingi wa kisheria itakayomsaidia kwa siku zijazo. “Anatakiwa kulishawishi Bunge litengeneze sheria zitakazomsaidia kufanya kazi ili watumishi wabakie kwenye msingi anaoutaka, kwa utekelezaji, usimamizi, uwajibikaji na utunzaji wa rasilimali lazima sheria ziandaliwe,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wenye Ulemavu, Stella Jairos alisema Rais Magufuli yuko sahihi kwa sasa kwani hakuna namna nyingine ya kurejesha nidhamu ya watumishi wa umma.

Alisema kasi ya Magufuli itakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania wa hali ya chini kwa kuwa walikuwa wamekosa matumaini ya kunufaika na rasilimali zao. “Nchi ilikuwa imepoteza mwelekeo , walikuwa wamebweteka sana, lakini sasa nidhamu itarejea.”
Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: