UJUMBE KUTOKA KWENYE KATUNI ALHAMISI DECEMBA 17/ 2015, SERIKALI ISIRUDI NYUMA KUBANA MATUMIZI YA MASHANGINGI (VX-V8).
Ahadi ya Rais Dk. John Magufuli, ya kudhibiti matumizi ya magari ya aina ya Toyota Land Cruiser VX-V8 maarufu kama `mashangingi,’ imeanza kutekelezwa kwa vitendo baada ya kutolewa agizo la kuimarishwa zaidi kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) ili waanze kufanyia matengenezo magari ya serikali.
Agizo hilo linaloendeleza dhamira ya Serikali ya awamu ya tano katika kubana matumizi yasiyo ya lazima ili mwishowe fedha zinazookolewa zielekezwe katika kuboresha huduma za jamii, lilitolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani.
Wakati akilihutubia Bunge, Novemba 20, mwaka huu, Rais Magufuli aliahidi kuwa serikali yake itadhibiti matumizi ya mashangingi ili kubana matumizi.
Mhandisi Ngonyani amewataka Temesa kuongeza ubunifu na katika kipindi kifupi kijacho wahakikishe magari ya serikali yanatengenezwa kwao.
Aliwataka Temesa kuhakikisha wanaongeza wataalam katika karakana zao ili kutimiza lengo hilo.
Agizo hilo limetokana na utaratibu wa miaka ya karibuni wa magari kutengenezwa gereji binafsi.
Hatua ya serikali ni ya kuungwa mkono kutoka na ukweli kuwa suala hilo limekuwa likiigharimu fedha nyingi.
Twafahamu kuwa suala la kubana matumizi ya mashangingi limekuwa gumu.
Mathalani, mwaka 2008, Waziri Mkuu wa zamani, Mizengo Pinda, baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, alitangaza dhamira yake ya kupunguza matumizi ya magari hayo.
Hata hivyo, hadi anamaliza muda wake wa uongozi suala hilo lilionekana dhahiri kumshinda.
Utelekelezaji wa kubana matumizi ya magari hayo unahitaji dhamira ya dhati kutoka kwa viongozi wa serikali na watendaji.
Pale Rais Magufuli atakapoendelea kuwa mkali kubana suala hilo, ndiyo tutapata mafanikio.
Bila shaka Serikali ya awamu ya tano inapaswa kurudisha kumbukumbu nyuma wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Katika kipindi hicho, viongozi wa serikali walitumia magari madogo aina ya Peugeot, Nissan n.k.
Pale walipohitaji safari, kulikuwa na magari machache aina ya Land Rover ili kusaidia viongozi wa serikali kufika sehemu mbalimbali.
Katika miaka ya karibuni, hali imekuwa tofauti, kwani tumeshuhudia baadhi ya viongozi licha ya kuishi karibu na vituo vyao vya kazi, bado wamekuwa wakipewa magari hayo ya kifahari.
Serikali inapaswa kuwa makini katika jambo hili kwani litasaidia kupata fedha nyingine za kufanyia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hatuhitaji kwenda hata nchi za nje kujifunza juu ya mfumo wa kubana matumizi ya magari, bali tujikumbushe tu wakati wa enzi ya Mwalimu Nyerere kuwa utaratibu gani ulitumika.
Hali ya huduma za jamii ni mbaya sana, hapo tunazungumzia afya na elimu.
Pamoja na jitihada za serikali kutatua matatizo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini ni hali mbaya katika hospitali nyingi za wilaya na mikoa.
Pia shule nyingi za serikali nazo ziko kwenye hali mbaya kutokana ukosefu wa fedha.
Gharama ya kununua gari moja aina ya Toyota Land Cruiser ni Dola 200,000 (sawa na Sh. milioni 423).
Kwa sasa serikali inakadiriwa kuwa na magari 2,778 ya aina hiyo ambapo gharama ya gari moja kwa kiasi kikubwa ingesaidia kuboresha huduma za kijamii. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment