AFUNGWA MIEZI 24 JELA KWA KUIIBIA KAMPUNI Sh27,000.
Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imemuhukumu mshtakiwa wa kwanza, Charles Minja (36) kifungo cha miezi 24 baada ya kupatikana na hatia ya kuiibia Kampuni ya Utalii ya Leorpard Tours Sh27,000.
Kampuni hiyo iliwafungulia kesi, Minja na Silver Justin (35) kwa kuisababishia hasara ya Sh800 milioni kati ya 2011 na 2013 kwa kuacha kuwapeleka watalii eneo la makumbusho la Olduvai Gorge.
Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Augustino Rwizile alisema baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili, imemuachia huru mshtakiwa wa pili, Justine baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani.
Alisema mshtakiwa Minja alikiri kujipatia kiasi hicho cha fedha baada ya kununua risiti ya kughushi aliyoiwasilisha kwenye kampuni yake kwa Sh10,000.
Hakimu Rwizile alisema Mahakama inamtia hatiani kutokana na udanganyifu alioufanya ambao ni kinyume na sheria.
“Kama Mahakama hatujaridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwa washtakiwa waliiba Sh800 milioni kwa sababu haijaonyesha ushahidi wa moja kwa moja,” alisema Hakimu Rwizile na kuongeza:
“Isipokuwa, Mahakama inamtia hatiani Minja kwa kosa la kughushi risiti na kujipatia Sh27,000 kinyume cha sheria.” Kabla ya kutolewa kwa hukumu, Wakili wa upande wa utetezi, Shedrack Mofuru aliiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa madai kuwa ana familia inayomtegemea na ni kosa lake la kwanza.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment