BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI APIGA SIMU KITUO CHA TELEVISHENI CHA CLOUDS DAR ES SALAAM


Rais Magufuli.


Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza, Rais John Magufuli amepiga simu Kituo cha Televisheni cha Clouds kwa ajili ya kuwapongeza watangazaji wa kipindi cha 360 kwa kazi nzuri.

Jana, ikiwa siku ya Alhamisi ambayo Mwananchi ilibaini Rais Magufuli amekuwa akifanya au kutangaza matukio makubwa, alipiga simu ya mkononi ya Hudson Kamoga, ambaye ni meneja wa kipindi hicho kinachorushwa moja kwa moja kila siku kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi 4.00.

“Mimi nawapongeza sana kwa kweli. Bahati nzuri nimeshashika majina yenu. Wewe ni Hudson, halafu mwingine anaitwa Baby (Kabaye) na mwingine anaitwa Sam (Sasali),” alisema Rais akiwa amewekwa hewani na watangazaji hao ambao walikuwa wakionekana kushangazwa na kitendo hicho cha Rais. “Mnavyozungumza na mnavyochambuaga magazeti yenu hapo mna aina yake ya tofauti. Kwa kweli it is really very impressive (inavutia sana).”

Wakajibu kwa pamoja: “Tunashukuru sana mheshimiwa.”

Rais akaendelea kusema: “Nimeamua kuwapigia ili kuwapongeza mimi ni shabiki wenu mzuri kweli.”

Wakajibu tena kwa pamoja, “Asante sana mheshimiwa,” huku wakipiga makofi.

“Lakini bahati nzuri pia wote wazuri… Sam unanifurahisha na huyo Baby.”

Huku wakielendelea na mazungumzo, Hudson akamuuliza Rais Magufuli kuhusu Kampeni ya Clouds ya kuwataarifu wananchi kuhusu fursa kumi ambazo wakizitumia na kuweka nguvu nchi inaweza kufika mbali kwa maendeleo.

Rais alimjibu: “Niliangalia lakini bahati mbaya hizo fursa kumi mlitoa kwa wanawake tu, wanaume hamkuwapa zawadi.”

Hudson alimjibu, “kwa sababu mwanamke akiwezeshwa anaweza na kwa sababu tunaelekea kwenye uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50, tukianza kumtengeneza mwanamke tunaweza tukafika mahali pazuri sana”.

Rais Magufuli akamjibu: “Basi mimi nawapongeza sana.”
Lakini kabla ya kukata simu, Rais Magufuli alisema: “Huyu hapa mke wangu (Janeth Magufuli) awasalimu, na yeye ni shabiki wenu.” Kabla ya kuanza kuongea, watangazaji hao walishangilia na kumsalimu mke wa Rais kwa sauti wakisema “shikamoo mama”. Alipopokea simu alijibu, “habari zenu jamani, marahaba,”

Wakamuuliza kwa pamoja, “habari ya asubuhi”

Mama Janeth akajibu, “mzuri”.

Baby akasema: “Tumefurahi kuzungumza na wewe mama.”
Mama Janeth akajibu huku akicheka, “Yaani na sisi huwa tunafurahi sana na huwa tunawashabikia sana. Asanteni jamani huwa mnatupa faraja huwa tunacheka na mzee wangu hapa (Rais Magufuli).”

Akielezea kuhusu ilivyokuwa hadi kupigiwa simu na Rais Magufuli, Kamoga alisema hawakutegemea kupigiwa simu na Rais, lakini kabla ya kuwapigia alimtafuta bosi wao, Ruge Mutahaba na kuomba azungumze na vijana wa kipindi cha Clouds 360. 


“Lakini bosi hakuwepo akampa namba yangu ya simu na kumwambia amwambie muongozaji wa kipindi atuarifu kuwa tutapigiwa simu na tukipigiwa tupokee,” alisema Hudson. “Sasa dakika chache kabla ya kwenda kwenye mapumziko mafupi nikaona simu yangu inaita na imeandika namba mpya. Basi nikapokea na kusikia sauti kama ya Rais Magufuli.

“Sikuamini nilihisi kama ni mchezo tu. Kidogo nimuulize wewe nani, lakini nikaacha ndipo akaanza kuzungumza na sisi.”

“Kwa kweli tumejisikia vizuri sana na jambo hili kwetu ni motisha sana, lakini pia tuna deni kubwa kwa Watanzania na Serikali kwa kuendelea kufanya kazi nzuri hasa ya kuibua mambo na kuyatafutia suluhu.”MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: