Dar es Salaam. Rais John Magufuli juzi alitangaza mabadiliko makubwa kwenye nafasi za ukuu wa miko akiwaacha makada 12, ambao wachambuzi wameeleza kuwa wametemwa kutokana na sababu kuu nne.
Hata hivyo, wengine wamesema sababu za kutemwa au kuteuliwa bado zinabaki kuwa hisia kwa kuwa uteuzi wa wanasiasa hauna vigezo maalumu.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao waliohojiwa na Mwananchi kuhusu uteuzi huo, sababu hizo ni utendaji, uzoefu, rika na umakini, ambazo hazitofautiana na vigezo ambavyo Rais Magufuli alivitaja kuwa angevitumia kuteua makada hao wakati alipoongea na wazee wa Dar es Salaam hivi karibuni.
Viashiria hivyo ni jinsi viongozi hao walivyokabiliana na ugonjwa wa kipindupindu, upungufu wa chakula, migogoro ya ardhi na upungufu wa madawati shuleni.
Katika uteuzi wake juzi, Rais Magufuli aliteua wakuu wa mikoa wapya 13 na kuwaondoa 12 waliokuwa kwenye mikoa ya Tabora, Geita, Kigoma, Tanga, Singida, Mbeya, Morogoro, Katavi, Mara, Simiyu na Shinyanga.
Akizungumzia uteuzi huo, Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema anaamini vigezo alivyobainisha Rais Magufuli ndiyo vimetumika kuwachambua.
“Kwa mfano, migogoro ile ya Morogoro bila shaka itakuwa imewaathiria baadhi ya wakuu wa mikoa ukiwamo Morogoro,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Gaudence Mpangalla wa Chuo Kikuu cha Ruaha alisema kabla ya kuondolewa kwa wakuu hao wa mikoa, Rais Magufuli alitumia muda mrefu kuwachunguza ili kujiridhisha kabla ya kupata watu wanaoweza kwenda na kasi yake.
“Nadhani kwa sasa ameona nani anamfaa na nani ambaye hawezi kuendelea naye. Ingawa kutambua sababu za kuwaondoa inakuwa vigumu, hata aliowateua lazima waendane naye, majukumu yanajulikana ila zaidi ni kuwa wabunifu na wachapakazi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala bora, Richard Mbunda alifafanua sababu hizo nne alizosema zilichagiza kiongozi huyo kuwaondoa 12.
Mbunda alitaja kigezo cha kwanza kuwa ni rekodi ya utendaji wa kiongozi mmoja huku akimtolea mfano Paul Makonda aliyepandishwa kutoka ukuu wa wilaya kuwa mkuu wa mkoa baada ya muda mfupi kuwa amebebwa na kigezo cha ubunifu.
Pili, Mbunda alitaja kigezo kingine kuwa ni uzoefu wa mtendaji uliosaidia kuchochea maendeleo katika maeneo yao.
“Kwa mfano, kuna viongozi kama Joel Bendera na Saidi Meck Sadiki ni wazee wenye uzoefu,” alisema Mbunda.
Tatu, Mbunda alitaja kigezo cha kuchanganya rika kwa viongozi hao huku akiwatolea mfano Makonda (Dar es Salaam) na Martin Shigela (Tanga).
Hata hivyo, mhadhiri huyo alisema: “Kilichoonekana katika uteuzi huo, Rais hakuzingatia suala la uwiano wa kijinsia, lakini si hoja kama ameangalia watu wa kumsaidia zaidi katika kasi yake.”
Mbunda alitaja sababu nyingine aliyozingatia kuwa ni umakini, akisema mazingira hayo yameonekana katika uteuzi wa wakuu wa mikoa wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika mikoa ya mipakani.
“Kwa kuangalia asili ya maeneo hayo, ilistahili kabisa kupeleka watu kama hao, kwa sababu changamoto za maeneo hayo zinahusu masuala ya kiusalama zaidi,” alisema mhadhiri huyo.
Vigezo vya Magufuli
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam takribani wiki tatu zilizopita, Rais Magufuli alitaja vigezo ambavyo wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri wanatakiwa kuvitumia kujipima.
Vigezo hivyo ni kuimarisha mapambano dhidi ya kipindupindu, kuondoa kero ya madawati, migogoro ya ardhi, upungufu wa chakula na matumizi sahihi ya fedha za umma.
Hata hivyo, Dk Bashiru Ali wa Idara ya Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema hakuna vigezo vinavyotambuliwa rasmi kutumika kwenye uteuzi wa viongozi kisiasa au kuwaondoa wa zamani.
Alisema kuondolewa kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro hakuwezi kuwa ushahidi wa moja kwa moja kuwa kunatokana na migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Migogoro iko. Hata Manyara ipo, si Morogoro pekee. Kwa hivyo huwezi kutumia kigezo hicho kama sababu iliyomtoa moja kwa moja mtu,” alisema.
Migogoro ya wakulima na wafugaji pia iko mkoani Dodoma.
“Kuhusu uteuzi wa Rais, tunaweza kuona viashiria kadhaa vya ukada, uwezo wa mtu, uzoefu au fadhila lakini itabakia kuwa hisia tu, kwa mfano labda mpakani wamepelekwa wanajeshi wastaafu kwa sababu kumekuwa na changamoto ya biashara za magendo, dawa za kulevya.
Lakini ulinzi ni tatizo maeneo mengi, kwa hivyo inabakia kuwa hisia tu,” alisema.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ SABABU 4 NDIZO ZILIZOSABABISHA KUNG'OLEWA KWA WAKUU WA MIKOA 12 WA JAKAYA KIKWETE HIZI HAPA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment