TFDA, TBS UKO WAPI USALAMA WA TAULO ZA KIKE ?
Amina Juma,
By Amina Juma , Mwananchi
Afya bora ni jambo la msingi katika maisha ya kila mwanadamu, kila mtu mwenye akili timamu anafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha anakuwa katika afya iliyo bora.
Lakini wakati mwingine, ni vigumu kwa mtu peke yake kuisimamia afya yake bila kuwepo kwa mkono wa Serikali au mamlaka husika zilizopewa dhamana ya kuhakikisha kwamba bidhaa zinazoingia nchini ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Kuna Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na pia kuna Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambazo kwa pamoja zinatakiwa kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia nchini ni bora na salama kwa afya ya mtumiaji.
Hata hivyo kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa bidhaa kadhaa na leo nitazungumzia kilio cha kinamama kuhusu taulo wanazotumia.
Sitapenda kutaja aina za taulo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wanawake kwa kuwaletea madhara mbalimbali mara wazitumiapo. Nataka mamlaka husika ziamke na kuzifanyia vipimo mbalimbali vya kitaalamu taulo hizo kwani zinatuathiri.
Nimeandika haya baada ya kuzungumza na wanawake wengi ambao wanasema kwamba wameamua kurejea taulo asili baada ya kupata madhara walipotumia taulo hizo.
Wapo wanaolalamikia kupata matatizo muwasho uliopitiliza mara wanapozitumia, lakini wapo ambao kiwango chao cha kawaida cha mzunguko hupungua au kukatika ghafla pale watumiapo aina fulani za taulo hizo. Kibaya zaidi wapo wanaolalamikia kuumwa mgongo baada ya kutumia taulo hizo kwa muda wa miezi miwili au mitatu tu.
Kwa sasa madukani kuna aina zaidi ya 20 ya taulo hizo za wanawake na asilimia kubwa ya wanawake hususan wa mijini wamekuwa wakizitumia. Ni kweli taulo hizi zinatuweka safi kwa muda wote lakini baadhi yake zinatishia usalama wa afya zetu.
Zipo nyingine ukizifungua tu kwa ajili ya matumizi zinatoa harufu kali ya manukato ambayo inasababisha chumba chote kujaa harufu ambayo huwa najiuliza inaweza kuwa salama kweli kwa sehemu ambayo taulo hili linakwenda kuwekwa?
Mara kwa mara wataalamu wa afya wamekuwa wakikataza matumizi ya manukato katika sehemu hizo lakini kwa taulo hizi inakuwaje?
Wataalamu wa afya pia wanaelekeza taulo hizi kubadilishwa kila baada ya saa nne hadi saba na wanawake wamekuwa wakifuata maelekezo hayo bila kupata nafuu yoyote.
Inadaiwa taulo hizo husafishwa kwa kutumia kemikali ijulikanayo kama Dioxin ili kuzifanya ziwe nyeupe na zionekane safi wakati wote.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kemikali ya Dioxin ni hatari kwa afya ya binadamu kwani inaweza kuleta madhara kwenye ini na kulizuia kufanya kazi vizuri, lakini pia kemikali hii inaweza kuathiri kinga ya mwili.
Mbali na athari hizo WHO inasema kuwa kemikali hiyo pia inaweza kuathiri mfumo wa uzazi wa mwanamke na hata kumhatarishia kupata saratani ya kizazi.
Hakika katika matumizi ya taulo hizi tunahitaji msaada wa mamlaka zinazohusika wazipime kwa kina ili kututoa hofu maana wanawake walio wengi na wanaojali afya zao wameamua kurejea kwenye matumizi ya taulo ya asili.
Tafadhali TFDA na TBS msiturudishe kwenye matumizi ya taulo za asili tunaomba mzifanyie utafiti wa kina hizi zinazoingizwa nchini ili kuepusha madhara.
0 comments:
Post a Comment