Na John Nditi, Morogoro.
SERIKALI mkoani Morogoro imesema itachukua hatua kali zikiwemo za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wafugaji wavamizi, wakulima na wavuvi ambao wamerejea tena kuendesha shughuli za kibinadamu baada ya kuvamia ndani ya bonde la Hifadhi ya Taifa na Pori Tengefu la Bonde la Kilombero.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe, alitoa kauli hiyo juzi mjini Ifakara, Kilombero baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kuwezesha umilikishaji ardhi kwa kutumia ndege ndogo akiwa na timu ya wataalamu kutoka wizara mbalimbali zikiwemo Maliasili na Utalii na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Alisema Serikali haitaweza kuendesha operesheni ya kuondoa mifugo kila mwaka ndani ya bonde la Kilombero, hivyo itatumia utaratibu wa kila siku kukamata wafugaji wavamizi, wakulima na wavuvi wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya bonde hilo ili kudhibiti uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kujitokeza.
Mkuu wa mkoa alijionea uvamizi huo akiwa angani wakati wa ukaguzi wa bonde la Kilombero, ambapo mifugo walionekama wakiwa wamehifadhiwa karibu na kingo za mto Kilombero, wakulima wakiendesha shughuli za kilimo na wavuvi wakiwa wamejenga kambi zao katika bonde hilo.
Kutokana na hali hilo, ameagiza watendaji wa wilaya ya Kilombero na Ulanga na vyombo vya ulinzi na usalama katika wilaya hizo kusimamia wajibu wao wa kila siku wa kuwaondoa wafugaji, wakulima na wavuvi hao.
Tayari amepiga marufuku uingizaji wa mifugo kutoka nje ya mkoa huo na kuagiza kukamatwa kwa yoyote atakayebainika akifanya hivyo bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Alisema amri hiyo pia inahusu mifugo kutoka wilaya moja hadi nyingine, kijiji kimoja hadi kijiji kingine huku akiongeza kuwa, utekelezaji wa upimaji wa ardhi yote ya vijiji na upangaji wa matumizi ya ardhi katika maeneo yaliyolengwa umekamilika.
Naye Mratibu wa Taifa Mradi wa Kilombero and Lower Rufiji Wetlands Ecosystem Management Project (KILORWEMP), Pellage Kauzeni alisema changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mradi huo zinazoendelea kutatuliwa na kikundi kazi cha wataalamu mbalimbali waliopo kwenye mradi huo.
Pamoja na kutatua changamoto hizo, Kauzeni alimwomba Mkuu wa Mkoa kushiriki katika kusaidia kazi ya kupanga matumizi bora ya ardhi ili ifanikiwe na kupata maeneo ya ardhi ya makazi, ardhi ya kilimo, ardhi ya akiba, ardhi ya hifadhi na ardhi malisho ya mifugo katika wilaya hizo tatu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Dk Aunette Kitambi alikiri kuongezeka tena kwa mifugo inayoingia kinyemela wakati za usiku na kujificha maeneo ambayo hayafikiwi kwa urahisi.
Dk Kitambi ambaye pia ni Ofisa Mifugo wa halmashauri hiyo, alisema mifugo hiyo inatoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma, wakati mingine ikitokea wilayani Ulanga.
Alisema baadhi ya watendaji wa serikali za vijiji na kata za Mofu na Ikwambe walikamatwa wakituhumiwa kupokea wafugaji wavamizi na kesi zao bado zipo kwenye mahakama za mwanzo kwa kipindi kirefu bila kufikiwa maamuzi.
Mwaka 2002, katika operesheni maalumu iliyoendeshwa katika bonde la Kilombero Serikali ilifanikiwa kuondoa mifugo zaidi ya 450,000.
0 comments:
Post a Comment