BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKUU WAPYA WA MIKOA WAKUBALI KULA KIAPO NA KUWA TAYARI KUTII MAAGIZO SITA YA RAIS DKT JOHN MAGUFULI

Dar es Salaam. Wakuu wapya wa mikoa jana walikula kiapo mara mbili, huku Rais John Magufuli akiwapa amri saba, ikiwamo ya kuwataka kuhakikisha wanaondoa malipo ya mishahara ya watumishi hewa ndani ya siku 15.

Rais Magufuli alitoa maelekezo hayo katika hotuba yake fupi mara baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa 26 aliowateua juzi kwenye hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba hiyo, Rais aliwataka wawakilishi wakuu hao kupambana na ujambazi, kusimamia ilani ya uchaguzi ya CCM, kutatua kero za wananchi, kuzuia vijana kucheza mchezo wa pool table na kusimamia utekelezaji wa elimu bure.

“Nataka mkawajibike kwelikweli na mimi nimeona bora niwambie mapema,” alisema Rais Magufuli ambaye ameingia madarakani na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

“Mnakwenda kufanya kazi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi. Hamuendi mikoani kutangaza siasa, mnakwenda kutimiza wajibu wenu kwa ajili ya wananchi.”

Februari 13, Rais Magufuli alitaja vigezo ambavyo angetumia kuwapima wakuu wa mikoa na wilaya, akiwataka kuzingatia suala la upungufu wa madawati, upungufu wa chakula na migogoro ya ardhi.

Lakini jana alitoa maagizo ambayo magavana hao watatakiwa kuyatekeleza.

Katika uteuzi huo uliotangazwa Jumapili iliyopita, nusu ya wakuu wa mikoa wa zamani walitemwa na akapandisha wakuu watano.

Katika uteuzi huo, sura nne miongoni mwa wakuu hao wa mikoa waliotumia saa moja kuapa kuanzia saa 3:40 hadi saa 4:40 asubuhi, ni za majenerali wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao walikuwa kivutio kutokana kutembea kwa ukakamavu wakati wakienda kula kiapo huku wakitumia maneno “ndiyo mkuu, ndiyo kamanda”.

Wastaafu hao ni meja jenerali Salum Kijuu (Kagera), Meja jenerali mstaafu Raphael Muhuga (Katavi), Meja jenerali Ezekiel Kyunga (Geita), Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga (Kigoma) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Zelote Steven (Rukwa).

Wakuu hao walikula kiapo cha kwanza mbele ya Rais na cha pili waliapa kwa pamoja kwa kutumia dakika nane, baadaye walisaini hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, inayotolewa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kiapo hicho ni cha kuahidi kutofanya mambo kadhaa hususuan kutumia cheo kwa maslahi binafsi, kulinda rasilimali za nchi; kutotoa wala kupokea rushwa, zawadi au fadhila; kutotoa siri za Serikali na kuwa wazalendo.

Ujambazi
Katika kukabiliana na ujambazi ambao umekuwa ukitikisa kwenye barabara zinazopitia misitunia, Rais alisema kuanzia sasa hatarajii kuona wanaotumia usafiri wa mabasi katika mikoa ya mipakani kama Kagera, Geita, Katavi na Kigoma wakisindikizwa na polisi kwa hofu ya kuvamiwa na abiria kuporwa mali zao.

Alisema kwa nchi inayojitawala kwa miaka 50 ni aibu kwa kwa raia wake kusindikizwa na polisi.

“Kusindikizwa na polisi maana yake hakuna usalama,” alisema amiri jeshi huyo mkuu na kuwataka wakuu hao kuimarisha ulinzi ili wananchi wawe salama.

Alisema atashangaa kama mtu mwenye cheo cha meja jenerali kama Salum Kijuu atashindwa kusimamia mkoa mmoja wa Kagera.

“Kwa bahati mbaya sikuwauliza (kabla ya kuwateua), labda hilo ndilo mnaweza kunisamehe, lakini nimeamua kuwateua nikiamini kwamba mtaniwakilisha vizuri mtakapokuwa katika mikoa yenu,” alisema Rais Magufuli katika hotuba hiyo ya dakika 24.

“Nilitegemea wengine mngekataa kuja kuapishwa, ila kwa kuwa mmesaini, mmeingia katika mtego wa kufanya kazi, na mimi niwape pole maana mnakwenda kufanya kazi kweli kweli.”

Pamoja na kutowataarifu mapema, Rais Magufuli alisema alifanya upembuzi wa kina kuwapata.

“Ndiyo maana nilichelewa sana kuchagua wakuu wa mikoa. Nilikuwa nauliza huyu kweli ataweza? Siku nyingine namfuta siku nyingine namrudisha,” alisema.

Mishahara hewa
Katika agizo la pili, Rais Magufuli alitaka wakuu hao kuhakikisha ulipaji wa wafanyakazi hewa unakoma.

Alisema alitumia “vijana wake” kufanya utafiti katika mkoa wa Singida na Dodoma na katika orodha ya malipo, walibaini kuw mwezi Desemba 2015 na Januari 2016 kulikuwa malipo ya mshahara kwa watumishi 202 wasio waajiriwa.

“Tuliwatuma mwezi wa pili na katika mikoa walizitizama halmashauri 14 zenye wafanyakazi 26,900 na kubaini wafanyakazi 202 wanalipwa mishahara,” alisema.

Huku akitoa karatasi kutoka kwenye mfuko wa suti yake nyeusi, Rais Magufuli alisema: “Kati ya wafanyakazi 202, walioacha kazi walikuwa sita, waliokufa na kufungwa 27, waliofukuzwa kazi wanane, wastaafu 158 na wenye likizo bila malipo walikuwa watatu.”

Alisema kama uozo huo unafanyika katika halmashauri 180 zilizopo nchini maana yake nchi nzima kuna malipo watumishi hewa 2,700 kama kila mmoja analipwa Sh1 milioni.

“Kwa mwezi tunaweza kuwa tunapoteza Sh2 bilioni,” alisema.

Alisema nchi nzima kuna watumishi 500,000 wa Serikali ambayo hutumia Sh550 bilioni kwa ajili ya kuwalipa, lakini mwezi uliopita Serikali ilitumia Sh850 bilioni kulipa mishahara pamoja na madeni ya nyuma.

“Najua mtawapa maelekezo wakurugenzi na wakuu wa wilaya ila mimi ninawapa siku 15 hawa wakurugenzi wawe wameondoa malipo ya mishahara hewa. Kama mwezi unaokuja kutakuwa na malipo ya mishahara hewa, mkurugenzi ajihesabu kazi hana na tutampeleka mahakamani,” alisema.

Elimu bure
Pia, Rais Magufuli aliwataka wakuu wa mikoa kusimamia sera ya elimu bure kwa kuhakikisha shule zinakuwa na madawati na majengo ya kutosha kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi huku madarasa na madawati yakiwa changamoto kubwa.

“Wapo watakaowalaumu, lakini nyinyi chapeni kazi. Fanyeni kazi kwa sababu tuna imani na nyinyi msituangushe,” alisema.

Rais Magufuli pia aliwataka kuhakikisha vijana wanafanya kazi ikiwa ni pamoja na kuwazuia kucheza mchezo wa pool table.

Wakuu wa mikoa wanena
Wakizungumza mara baada ya kuapishwa, Meja Jenerali Kijuu alisema kazi ya kwanza atakayoifanya ni kusoma mazingira ya mkoa wa Kagera, kupitia changamoto na kupanga jinsi ya kuzitatua.

“Hilo la ujambazi nitapambana nalo na nitahakikisha hali inakuwa shwari. Kagera watafurahi wenyewe maana limekuwa eneo la hatari kwa wasafiri sasa chini ya utawala suala hilo wangu litakuwa historia,” alisema.

Kwa upande wake Meja Jenerali Muhuga alisema: “Nitatumia vyombo vya dola kuimarisha ulinzi na usalama Katavi, kukomesha uhamiaji haramu, uvunaji wa miti na ujangili. Nitahakikisha wananchi hawasindikizwi tena na polisi.”

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amosi Makalla alisema atahakikisha anatatua kero za wananchi, ikiwa ni pamoja na kusimamia Sh50 milioni zitakazotolewa na Serikali kwa kila kijiji, jambo ambalo pia lilisisitizwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu.

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema alisema atasimamia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwashughulikia watakaokiuka taratibu, kanuni na sheria.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango-Malecela alisema atahakikisha anasimamia sera ya elimu bure kutumia uzoefu wake katika elimu. Katika shughuli hiyo ya kuapishwa, mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisababisha minong’ono baada ya kushikwa na kigugumizi wakati anakula kiapo pamoja, huku Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola akibeba vitabu vyote vya kiapo na kuondoka navyo, jambo lililosababisha Rais Magufuli kuangua kicheko.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: