BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DIWANI WA HALMASHAURI YA NZEGA NAMNA ALIVYOZIMIA SIKU MBILI KISHA KUNUSURIKA KUZIKWA KABURINI.


Madebe Ginasa akiwa katika baadhi ya vikao vya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Nzega, mkoani Tabora. Picha na Shija Felician

Kahama.
Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, unapotaja jina la Madebe Ginasa au Madebe Nhale hupati shida ya kuelezwa
ni nani kutokana na mashabiki wa ngoma za jadi.


Jina hilo ambalo limekuwa likivuma tangu miaka ya 90 hadi sasa lipo kwenye orodha ya historia ya wasanii nchini kutokana na msanii huyo wa ngoma za jadi kufanya mabadiliko kutoka ngoma za asili na kuanza kupiga miziki ya asili.


Katika makala haya, Madebe ambaye kwa sasa ni Diwani wa
Kata ya Mwasala, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega anaelezea historia yake ndefu jinsi alivyoanza mpaka kufikia umaarufu alionao kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa hasa ya Shinyanga, Tabora, Simiyu na Mwanza.


Basu Nhale, ni kaka yake ambaye anaeleza kwamba Madebe baada ya kuzaliwa na kufikisha umri wa miezi mitano, aliugua kama watoto wengine na bahati mbaya alizimia huku wakiamini amekufa.

Nhale anasema baada ya siku mbili tayari wakiwa wamekamilisha taratibu za maziko, alipita mzee mmoja na kwenda mpaka ulipokuwa umehifadhiwa mwili.

Anasema baada ya mzee huyo anayemtaja kwa jina moja la Mnengela kufika mahali ulipohifadhiwa mwili huo alitoka na kuwaambia waombolezaji kuwa: Mkwizonjika umunho ng’wenoyo alimhola atenazumaleka (Msimzike mtu huyo hajafa).

Nhale anasema mzee huyo aliendelea kuwaeleza: “Unene natenabogota wakupija omunho ng’wenoyo (Mimi sina dawa ya kumponyesha mtu huyo).”

Baada ya hapo watu waliokusanyika kwenye msiba huo waliingiwa na taharuki, wakati huo kaburi tayari lilikuwa limechimbwa kwa maziko.

Hata hivyo, Nhale anasema waliahirisha mazishi huku wakiwa wamepigwa butwaa, mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Manengelo aliingia kwenye chumba hicho na kumtengenezea dawa mpaka akazinduka, ndiyo ukawa mwanzo wa maisha ya Madebe.

Alivyozama ngomani

Madebe ambaye alizaliwa 1976, ni mtoto wa sita kati ya wanane wa Nhale, akiwa na umri wa miaka saba alikuwa na kazi ya kuchunga ndama wa familia, akiwa machungoni alipita mzee mmoja aliyemtaja wa jina la Mwanabungu.

Madebe anasema Mwanabungu alimkuta akichunga ndama, akamtaka waende kuangalia ngoma ya jadi iliyokuwa ikichezwa eneo jirani hiyo likuwa miaka ya 80.

Baada ya kuwasili kwenye ngoma, Mzee Mwanabungu alimfunga nyasi na majani ya miti na kumuombea nafasi aingie kucheza, alipoingia uwanjani alipata mashabiki wengi na kutuzwa fedha.

Pia, Madebe anasema baada ya kuonja utamu wa fedha alianza kwenda sehemu mbalimbali kucheza wakati huo akiwa na umri wa miaka minane. Anasema aliambatana na kaka yake Basu ambaye alikuwa na jukumu la kumpakia kwenye baiskeli.

Anasema baada ya jina kuanza kushika chati, alitengeneza ngoma zake mwenyewe, kaka yake huyo alikuwa na mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe ambao ndiyo ulitumika kubeba ngoma kwenda maeneo mbalimbali.

Wakati jina la Madebe likizidi kupanda chati alishindwa kwenda shule na kwamba, zaidi hiyo ilichangiwa na kuugua miguu akiwa darasa la pili. 


Anaongeza kuwa ngoma ilichanganya na kuwa na wafuasi wengi huku akiwa na umri mdogo kati ya wapiga ngome wengine. 

“Baada ya hapo nilikwenda kwa Mzee Ginasa kuzaliwa upya kwa ajili ya ngoma, ngoma yangu ikawa ya Bagalu na nikaanza rasmi kuwa malenga nikiwa na umri wa miaka 12, nilianza kushindanishwa na malenga wazee akina Ng’wananhome, Shiganzasumbi, Tagala ambao walikuwa ni wazee malenga maarufu kwa wakati huo mikoa ya Kanda ya Ziwa,” anasema Madebe.

Anasema licha ya kupambana na wazee hao, aliwashinda na jina lake lilizidi kuvuma kila kona hasa kwa sababu ya umri mdogo kuliko wote na kwamba, kuwashinda wazee kama hao alianza kupata fedha kwa kuitwa kwenye mashindano mbalimbali ambayo hufanyika kila mwaka wakati wa msimu mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Ushiriki kwenye siasa
Siku zilivyozidi kusonga mbele, Madebe aliendelea kupata umaarufu maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, Paschal Ntale ambaye wakati huo alikuwa mwamuzi wa mashindano ya ngoma, anasema Madebe alikuwa anashinda sana.

Ntale anasema kuna siku wakiwa wanacheza na Shiganzasumbi walishindwa vibaya, ikawalazimu kujificha kwenye mabanda baada ya wachezaji wao kuwakimbia na kubaki wawili baada ya kupata hofu kuwa wakitoka wangezomewa.

“Ilinibidi nimtoe Madebe usiku, watu wamesambaa tulishindwa vibaya siku hiyo. Baada ya hapo tuliamua kusaka dawa ya bahati ya kujaza watu ambayo tulifanikiwa kurudisha heshima, kwani tuliendelea tena kuwashinda malenga wakubwa,” anasema Ntale.

Anasema umaarufu huo ulienea hadi serikalini, hivyo Madebe akaanza kuitwa na viongozi wa wilaya na mkoa kwenye sherehe mbalimbali zikiwamo za Mwenge, wakati huo akawa ameingia kwenye siasa kwa kupiga nyimbo za CCM.

Madebe anasema ilizidi kumpa umaarufu ndani ya chama na Serikali na akawa kada wa CCM, baada ya kuanzisha Jimbo la Puge mwaka 2015, ilizaliwa Kata ya Mwasala ambayo aligombea na kushinda kuwa diwani.

Miujiza ya Madebe
Baada ya kuzaliwa upya kwenye umalenga wa ngoma, ‘baba yake’ huyo wa dawa, Mzee Ginasa alimuachia miujiza wakati wa kucheza ngoma za jadi ambazo zinamuwezesha kuita nyuki wa kusambaratisha watanzamaji wa mpinzani wake.

“Uwezo huo wa kuita nyuki mpaka sasa ninao, niweza kuita nyuki sasa hivi zikawasambaratisha. Pia, nilikuwa na uwezo wa kulima mahindi na karanga wakati nacheza ngoma na watu wakavuna hapohapo na kula, hiyo ndiyo miujiza niliyokuwa nayo wakati nikicheza ngoma,” anasema Madebe.

Kulingana na mabadiliko ya vizazi, wazee wa zamani wamepungua Madebe anasema mambo hayo kwa sasa yanakosa mashabiki kutokana na kupungua kwa msisimko baada ya malenga wengi kuzeeka, wengine kufariki dunia bila kuacha nyezo kwa wafuasi wao.

Kutokana na hali hiyo, Madebe hivi sasa ameachana na ngoma hizo na ameungana na wasanii wengine kupiga miziki ya asili, tayari ametoa CD mbili ambazo zimempa umaarufu katika Tasnia ya Muziki wa Asili nchini.

Safari ya Botswana
Baada ya kuvuma kwenye miziki ya asili, Madebe alikutana na msanii maarufu Afrika, Dikakapa-Tsala ambaye alimtaja baada ya kufanya naye shoo nchini na kumpa mwaliko kwenda kupiga naye shoo tatu Botswana.

“Kabla ya kwenda Botswana nilitafuta walimu wa kunifundisha kuongea Kiingereza kwa muda wa miezi mitano, nikajua kuzungumza lugha hiyo ambayo mpaka sasa naweza kuzungumza licha ya kuishia darasa la pili,” anasema Madebe na kuongeza:

“Huyu Dikakapa-Tsala alikuwa mtumishi wa Serikali Idara ya Usalama wa Taifa, lakini baada ya kazi anaendelea na shughuli zake za usanii.”

Maisha ya siasa
Hivi sasa Madebe anasema licha ya kuwa diwani, baada ya vikao anaendelea na shughuli yake ya usanii ambayo kiuchumi imemuwezesha kumiliki gari aina ya Noah, zaidi ya nyumba nne, heka 400 za ardhi na mifugo. Watoto wake wengi wanasoma nchi mbalimbali ikiwamo Uganda.

Madebe anasema usanii ndiyo uliompa umaarufu na kupata udiwani, hivyo hawezi kuuacha ataendelea katika maisha yake yote ya siasa.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Jackline Liana anasema Madebe ni diwani mbunifu anayetumia usanii wake kuharakisha maendeleo ya wananchi wake hasa suala la madawati, kwa kutumia sanaa amefanikisha kukamilisha utengenezaji madawati 170 yaliyokuwa yakitakiwa kwenye kata yake. 


Madebe ni baba wa watoto 14, anaishi na familia ya watu 40 wanaomtengemea, anawataka wasanii wengine kutokatishwa tamaa na wizi wa CD unaofanywa na maharamia na kuwataka kuwa wabunifu.CHANZO:MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: