BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MIKATABA MIBOVU, WIZI, RUSHWA NA UONGOZI DHAIFU WAKWAMISHA UFANISI WA UTENDAJI NZURI KATIKA SHIRIKA LA TENESCO TANZANIA


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo


WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema maombi ya kugawa Shirika la Umeme (Tanesco), hayana tija kwani shirika hilo kwa sasa linakabiliwa na tatizo la mikataba mibovu, wizi, rushwa na uongozi dhaifu.

Profesa Muhongo alisema hayo juzi usiku, wakati akifanya majumuisho ya mjadala wa bajeti kwa mwaka 2016/17 na kuwataka wabunge wasishabikie mambo bila kufanya tathmini.

Alikiri kuwapo kwa maombi ya kutaka Tanesco igawanywe, lakini akasisitiza kuwa hilo halina tija kwa sababu shirika hilo linasimamia uzalishaji wa megawati 1,500 kwa sasa, hivyo unaligawa ili iweje.

Alisema litazaliwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mpya, akisema kwa sasa shirika hilo linabadilika na mikataba ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta itakuwa historia na haitaendelezwa tena.

Alikiri kuwapo kwa mikataba mibovu ya uzalishaji umeme na katika kuleta ushindani, alisema Mei 30, mwaka huu, watatangaza miradi mbalimbali ili kuita wawekezaji kwa njia ya uwazi, na kila mmoja kueleza ni mradi gani ana uwezo nao.

Awali akizungumzia suala la kusitisha mitambo ya kufua umeme kwa dharura, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, alisema kwa sasa Tanzania imejipanga katika kutumia umeme wa gesi na ule wa maji, lakini haitarudi kutumia mafuta.

“Mikataba yote ya uzalishaji wa umeme wa mafuta haitaendelezwa, Aggreko, Symbion hawataruhusiwa tena katika mikataba ya dharura,” alisema Dk Kalemani.

Mbali ya Aggreko na Symbion, kampuni nyingine za kufua umeme zinazouza umeme wa mafuta kwa Tanesco ni Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Songas. Akisisitiza suala hilo, Profesa Muhongo alisema umeme wa kutumia mafuta sasa ni historia kwa nchi hii na kwamba Watanzania wataumia kwa sasa, lakini watapata faraja baadaye.

“Umeme unaozalishwa kwa mafuta ni historia kwa nchi hii, ndio maana umeme unakatika kila Jumapili kwa baadhi ya maeneo, lakini ni bora tuumie sasa, tupate faraja baadaye,” alieleza Profesa Muhongo akizungumzia miradi mbalimbali ya umeme inayosababisha ukatwe mara kwa mara.

Kuhusu miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Profesa Muhongo alisema hadi kufikia juzi, Hazina wametoa Sh bilioni 80.2 ikiwa ni asilimia 80 ya miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Pili, ili kukamilisha miradi hiyo ifikapo mwezi ujao kama ilivyopangwa.

Alisema Sh bilioni 534 zilizopangwa kwa ajili ya REA Awamu ya Tatu, zote zitapatikana, na anahangaika kupata fedha zaidi za miradi hiyo ambayo imesaidia kuongeza upatikanaji wa umeme.

Alisisitiza kuwa katika fedha za REA, hakuna hata sentimoja kutoka msaada wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani, kama ilivyodai Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Akizungumzia vinasaba katika mafuta, alisema ameitisha kikao Jumanne ijayo kujadili suala hilo ambalo lilizungumzwa sana na wabunge wakati wakichangia mjadala wa hotuba yake.

Alisema kikao hicho kitawahusisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura), wahifadhi wa mafuta, wasafirishaji na wafanyabiashara.

Kuhusu Kampuni ya Dangote kutumia makaa ya mawe badala ya gesi asilia kuzalisha saruji Mtwara, alisema kiwanda na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) walishindwana katika malipo. 


Hata hivyo, alisema kiwanda hicho kiliagiza makaa ya mawe mara moja kutoka Afrika Kusini, na sasa kinatumia makaa ya mawe kutoka Ngapa.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: