BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UNDANI: WALIOMBAKA MSICHANA GESTI NA KUMWINGILIA KINYUME NA MAUMBILE WAFIKISHWA MAHAKAMANI MOROGORO



Na Hamida Shariff, Mwananchi Morogoro.
Morogoro.
Mamia ya wakazi wa Morogoro jana walifurika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa kushuhudia watu sita waliofikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kumbaka binti wa miaka 21, huku wakirekodi video na kisha kusambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii.

Kutokana na hali hiyo, polisi waliimarisha ulinzi, huku wananchi na waandishi wa habari wakizuiwa kuingia kwenye chumba cha Mahakama kusikiliza kesi hiyo iliyosomwa faragha kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na sheria ya makosa ya ubakaji kuzuia kusikilizwa hadharani.
Afisa wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro (SSP), Isaack Katamiti kulia akitoa maelekezo kwa, Iddy Adamu kushoto na Zuberi Thabiti huku wakiwa chini ya ulinzi mkali katika mahakama ya hakimu mkazi Morogoro wakituhumiwa kumbaka msichana (21) eneo la Dakawa na kumwingilia kinyumbe na maumbile bila ridhaa yake kisha kusambaza picha chafu za ngono zilizopigwa katika mfumo wa video mitandao ya kijamii.Picha na Juma Mtanda.

Katika kesi hiyo, washtakiwa Idd Adamu (32) mkazi wa Makambako na Zuberi Thabiti (30) mkazi wa Mbarali mkoani Mbeya walishtakiwa kwa kosa kumbaka na kumlawiti binti huyo, huku wakimpiga picha za video na kisha kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila alimweleza Hakimu Mary Moyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Aprili 27, mwaka huu jioni katika nyumba ya kulala wageni iliyofahamika kwa jina la ‘Titii’ iliyopo Dakawa Wilaya ya Mvomero.

Mbali ya washtakiwa hao, watu wengine wanne walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Ivan Msack kwa kosa la kusambaza picha hizo za video kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo WhatsApp, jambo ambalo ni kosa chini ya Sheria namba 14 (1b) na (2b) ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao ni Rajabu Salehe (30), Ramadhan Ally (26), Musini Ngai (36) na John Peter (26) wakazi wa Dakawa, Mvomero ambao wote kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 28 kwa nyakati tofauti.

Baada ya kusomewa mashtaka yao na kukana, upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila, Edga Bantulaki na Calstus Kapinga uliwasilisha mahakamani hapo hati ya zuio la dhamana kwa washtakiwa hao kwa madai kuwa endapo watakuwa nje, wanaweza kuharibu upelelezi wa kesi hiyo. 


Pia, kuhatarisha usalama wa mlalamikaji na washtakiwa wenyewe kutokana na kesi hiyo kuvuta hisia za watu wengi.

Wakili Ignas Punge anayemtetea Ally, aliwasilisha ombi la dhamana lakini Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi itakapotajwa tena na kutolewa uamuzi wa maombi hayo, hivyo washtakiwa hao kupelekwa rumande. 


Wakati kesi hiyo ikiendelea baadhi ya watu waliokuwa Mahakamani hapo waliangua kilio na mmoja wao ambaye hakutaka kutaja jina alidai baadhi ya washtakiwa waliosambaza picha hizo wana uhusiano na binti aliyedhalilishwa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: