Juma Mtanda, Morogoro.
Timu ya soka ya Muheza United FC ya mkoani Tanga imeshindwa kuendelea na michezo ya ligi ya mabingwa ya mikoa kati ya wapinzania wao baada ya wachezaji 11 kuugua ugonjwa wa kipindupindu na kulazwa katika kituo cha afya cha Sabsaba Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili mjini hapa, Msimamizi wa kituo cha Morogoro kutoka TFF, Charles Ndagala alisema kuwa mchezo kati ya Stend FC ya Pwani na Muheza United FC uliopangwa kufanyika majira ya saa 8 mchana umesogezwa mbele kufuatia wachezaji 11 wa Muheza United kuugua kipindupindu.
Ndagala alisema kutokana na dharura hiyo mchezo huo utapangwa siku nyingine hadi hali ya wachezaji hao watapotengemaa afya zao.
“Timu ya Muheza United FC wachezaji wake 11 wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu hivyo kutokana na dharura hiyo uongozi umesogeza mchezo wao na Stend FC ya Pwani na mchezo kati ya Mbagu FC ya Mtwara dhidi ya Stend Misuna FC ya Singida utafanyika kama ulivyopangwa majira ya saa 10 jioni katika uwanja wa jamhuri Morogoro.”alisema Ndagala.
Ndagala alisema kuwa taarifa zilizomfikia alieleza kuwa mchezaji wa kwanza alianza kupata homa majira ya saa 8 usiku na kukimbizwa kituo cha afya cha Uzima Mwembesongo.
“Mgonjwa wa kwanza aligundulika majira ya saa 8 usiku na wengine wanne kukimbizwa hospitali ya mkoa wa Morogoro ambapo walipimwa na kugundulika kuwa wanaugua ugonjwa wa kipindupinduu.”alisema Ndagala.
Baada ya kugundulika kuugua kipindupindu wagonjwa wengine walikimbizwa moja kwa moja kituo cha afya Sabasaba.
Kocha mkuu wa timu ya soka ya Muheza United FC, John King Kibwna aliwataja wachezaji hao waliolazwa katika kituo cha Afya Sabasaba Manispaa ya Morogoro kuwa ni pamoja na Iddi Bohero, Ramadhan Rajabu, Jerd Stephen, Nirmo Rashid Sendeka, Abdul Mashaka, Pima Omari, Athuman Mwandani, Robert Newa, Iddi Kadabla na Iddi Ramadhani.
Afisa afya wa Manispaa ya Morogoro Dkt Gabriel Malissa alisema kuwa walipokea wagonjwa 11 na wamelazwa katika kituo cha afya Sabasaba na hali zao zinaendelea viziri.CHANZO:MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment